Wanasayansi wagundua dawa ya meno inayoweza kurekebisha jino lililooza

Chanzo cha picha, King's College London
Watafiti wanasema dawa ya meno iliyotengenezwa kwa nywele za mtu mwenyewe inaweza kusaidia kurekebisha na kulinda meno yaliyoharibika.
Timu ya watafiti katika Chuo cha King's College London wamegundua kwamba keratini - protini inayopatikana kwenye nywele, ngozi na pamba - inaweza kurekebisha enamel ya jino na kuacha hatua za awali za kuoza.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba wakati keratin inapogusana na madini kwenye mate, huunda mipako ya kinga ambayo inaiga muundo na kazi ya enamel ya jino la asili.
"Keratin inatoa njia mbadala ya matibabu ya kawaida ya meno," anasema Sarah Gamia, mtafiti wa udaktari katika Chuo cha King's London na mwandishi mkuu wa utafiti huo.

Chanzo cha picha, King's College London
"Teknolojia hii inaziba pengo kati ya biolojia na kuwapa madaktari wa meno nyenzo ya kibayolojia ambayo ni rafiki wa mazingira ambayo yanaiga michakato ya asili," aliongeza Sarah Gamia.
"Siyo tu kwamba nyenzo hii inazalishwa kwa njia endelevu kutoka kwa taka za kibaiolojia kama vile nywele na ngozi, pia huondoa hitaji la tiba ya jadi ya plastiki zinazotumiwa katika matibabu ya kawaida ya kurekebisha, ambayo mara nyingi huwa na sumu na ambayo ni tiba ya muda mfupi."
Katika ripoti yao ya utafiti iliyochapishwa katika jarida la Advanced Healthcare Materials, watafiti walisema walitoa keratini inayohitajika kutoka kwa pamba.

"Tofauti na mfupa na nywele, enamel ya jino haiwezi kurejeshwa, ikimaanisha kwamba inapoisha, inapotea milele," anasema Dk Sharif Al-Sharkawi, mwandishi mkuu na mtaalamu wa dawa za meno bandia katika Chuo cha King's College London.
"Tuko katika enzi ya kusisimua ambayo teknolojia ya kibayoteknolojia itaturuhusu sio tu kutibu dalili lakini pia kurejesha utendaji wa kibaolojia kwa kutumia nyenzo za mwili," anaendelea.
Dk. Al-Sharkawi anamalizia hivi: "Kwa maendeleo zaidi ya njia hii na ushiriki ufaao wa tasnia, hivi karibuni tunaweza kuwapa watu tabasamu kwa meno yenye nguvu na yenye afya kwa kutumia kitu rahisi kama kukata nywele.















