Mtu anapaswa kunywa maji kiasi gani ili kuweka figo zake salama?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Figo ni moja ya viungo muhimu vya mwili wa mwanadamu, ambavyo vina majukumu mengi ya kuweka mwili katika afya njema.

Madaktari mara nyingi wanashauri kwamba ili kuweka figo kuwa na afya njema, kula kiasi cha chumvi, kuepuka sukari ya ziada na kutotumia dawa za maumivu bila ushauri wa daktari.

Hatua nyingine nyingi pia zinapendekezwa ili kuepuka shinikizo nyingi kwenye figo.

Kwa hivyo ni muhimu kunywa kiasi fulani cha maji ili kuweka figo kuwa na afya? Katika ripoti hii, tutajaribu kupata majibu kwa maswali haya.

Figo hufanya kazi ili kudumisha usawa wa electrolyte katika mwili wetu. Inadhibiti kiasi cha vipengele kama sodiamu na potasiamu.

Dkt. Vivekanand Jha, rais wa zamani wa Jumuiya ya Kimataifa ya Nephrology na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya George ya Afya ya duniani, ni mtaalamu wa magonjwa ya figo.

Anasema, "Figo huondoa vitu visivyo vya lazima kutoka kwa mwili, ambavyo tunavipata kupitia chakula au kwa njia zingine. Na pia vitu ambavyo hutengenezwa mwilini kimetaboliki."

Dkt. Vivekanand Jha anasema, "Figo pia huzalisha aina nyingi za homoni mwilini, ambazo ni pamoja na kutengeneza damu, homoni zinazodhibiti shinikizo la damu na homoni za kudumisha usawa wa elektroliti."

Ni muhimu sana kudumisha usawa wa electrolyte kwa kila mchakato wa kimetaboliki katika mwili wetu.

Kwa mfano, kiasi fulani cha elektroliti kinahitajika kwa kila seli ya moyo kufanya kazi vizuri. Ikiwa elektroliti hazina usawa, kazi ya ubongo inaweza kuathiriwa, ufanisi wa misuli unaweza kupungua na mfumo wa neva unaweza pia kuathiriwa.

Dkt. Garima Agarwal, mtaalamu wa figo katika Hospitali ya Manipal mjini Bangalore, anasema, "Ikiwa figo hazifanyi kazi ipasavyo, basi kutumia vitamini D hakutakuwa na manufaa yoyote. Hata unywe vitamini D kiasi gani, haitaufaidi mwili."

Figo pia huitwa aina ya 'kiimarishaji cha voltage' kwa mwili. Ikiwa mtu hunywa maji zaidi kuliko inavyotakiwa, figo huondoa maji ya ziada kutoka kwa mwili.

Ni kiasi gani cha maji unapaswa kunywa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kila tunapohisi kiu, ni ishara kwamba mwili unahitaji maji
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dk Vivekanand Jha anasema, "Hakuna kiasi maalum cha maji tunachopaswa kunywa kila siku ili kuweka figo zetu kuwa na afya. Mwili wetu wenyewe hutuambia ni kiasi gani cha maji kinachohitajika. Kuhisi kiu ni dalili ya hili."

Anaeleza kuwa maji huendelea kutoka mwilini kwa njia nyingi, kama vile jasho na kupumua. Mbali na hili, kuna baadhi ya taratibu ambazo hazionekani, lakini ndani yao pia maji hutoka nje ya mwili. Katika hali hiyo, angalau 700 ml hadi 800 ml ya maji ni muhimu kwa mtu mzima.

Hata hivyo, mwili haupati kiasi kinachohitajika cha maji kwa kunywa maji ya kawaida tu. Maji pia hufika mwilini kupitia vimiminika kama vile maziwa, maji ya matunda au mtindi.

Pia ni muhimu kutambua kwamba kiasi gani cha maji ambacho mtu anahitaji inategemea umri wake, shughuli za kimwili na mazingira. Ikiwa mtu anaishi katika hali ya hewa ya joto, atahitaji maji zaidi.

Dkt. Shailesh Chandra Sahay, Mkurugenzi wa Idara ya Urology katika Hospitali ya Max, Patparganj, Delhi, anasema, "Mtu wa kawaida anahitaji lita tatu hadi tatu na nusu za maji kila siku. Si lazima kwamba kiasi hiki kinatimizwa tu na maji ya kawaida. Inaweza kutimizwa na aina yoyote ya kioevu. Ikiwa tunadumisha usawa wa maji katika mwili, basi uwezekano wa maambukizi ya mkojo pia hupungua."

"Kwa watu wanaougua ugonjwa wa moyo au figo, kiasi cha maji kinachotumiwa huzuiwa kidogo ili kisiwe na shinikizo kubwa kwa viungo hivyo."

Dkt. Garima Agarwal anasema, "Figo pia husawazisha kiasi cha maji mwilini. Ikiwa umekunywa maji mengi, figo zitatoa nje, na ikiwa unakunywa kidogo, maji yale yale yatahifadhiwa mwilini. Hakuna kiwango maalum cha maji ambacho mtu anapaswa kunywa. Hata hivyo, kwa ujumla mtu mzima mwenye afya njema anapaswa kunywa lita mbili hadi tatu za maji kila siku."

Uhitaji wa maji katika mwili pia unategemea ukubwa wa mwili wa mtu. Kwa mfano, watoto wadogo wanahitaji maji kidogo kuliko watu wazima.

Vidokezo rahisi na vya msingi vya kuweka figo kuwa na afya

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lishe bora ni muhimu ili kuweka figo zako ziwe na afya

Njia ya msingi zaidi ya kuweka figo zako kuwa na afya ni kula lishe bora, kudhibiti uzito wa mwili, na kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Dkt. Garima Agarwal anasema, "Magonjwa ya figo hayapatikani sana katika nchi za Mashariki ya Kati kwa sababu watu huko hutumia chumvi kidogo. Wakati huko India, watu wengi hutumia chumvi nyingi, ambayo huathiri figo."

Wakati mtu hutumia chumvi nyingi au sukari, kuna shinikizo la ziada kwenye figo ili kudumisha usawa. Shinikizo hili linaweza kuathiri utendaji wa figo kwa muda mrefu.

Mbali na hili, watu wengi wanakabiliwa na shinikizo la damu kwa muda mrefu, lakini hawalichukulii kwa uzito. Kulingana na madaktari, shinikizo la damu huathiri moja kwa moja figo, kwa sababu zinapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuweka shinikizo la damu sawa.

Kwa hivyo, ikiwa mtu ana shida ya shinikizo la damu, inapaswa kudhibitiwa kupitia dawa kulingana na ushauri wa daktari.

Dkt. Garima anasema, "Sipingi vitu vya mitishamba, lakini chochote unachokula kuleni kwa ushauri wa daktari au mtaalamu. Usinunue dawa dukani peke yako. Hasa dawa za kutuliza maumivu, kwa sababu zinaweza kudhuru figo."

Ushauri mwingine muhimu ili kuweka figo kuwa na afya ni kuepuka kuvuta sigara, kwa sababu tumbaku na bidhaa zake pia huathiri moja kwa moja figo.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla