Mawasiliano ya siri ya wanyama wa baharini yagunduliwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanasayansi amegundua kwamba viumbe 53 vya baharini hapo awali waliodhaniwa kuwa kimya wanaweza kuwasiliana.
Viumbe hao walikuwa wakituma ujumbe muda wote, lakini wanadamu hawakuwahi kufikiria kuwasikiliza, Gabriel Jorgewich-Cohen adokeza.
Alitumia maikrofoni kurekodi spishi, ikiwa ni pamoja na kasa, wakiwasiliana walitaka kujamiiana au kuanguliwa kutoka kwa yai.
Matokeo yanadai kuandika upya baadhi ya yale tunayojua kuhusu mabadiliko hayo.
Wanapendekeza kwamba wanyama wote wenye uti wa mgongo wanaopumua kupitia pua zao na kutumia sauti kuwasiliana walitoka kwa babu mmoja miaka milioni 400 iliyopita.
Ni madai yenye nguvu katika biolojia ya mageuzi ambayo hujadili iwapo viumbe hai vilitokana na babu mmoja au asili nyingi.
Bw Jorgewich-Cohen, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Zurich, Uswizi alianza kazi yake akiwa na mtazamo kwamba wanyama wa baharini wanaweza kuwasiliana kwa sauti.
Alitumia vifaa vya sauti na video kurekodi spishi 53 zilizofungwa duniani kote, ikiwa ni pamoja na Chester Zoo nchini Uingereza.
Viumbe hao ni pamoja na kasa 50, tuatara, kambaremamba na amfibia.

Chanzo cha picha, GABRIEL JORGEWICH-COHEN
Ilifikiriwa kwamba wanyama hao wote walikuwa bubu lakini Bw Jorgewich-Cohen anadokeza kwamba hawakusikika kwa sababu sauti zao zilikuwa ngumu kutambua.
‘’Tunafahamu ndege anapoimba. Huhitaji mtu yeyote kukueleza ni nini. Lakini baadhi ya wanyama hawa wako kimya sana au hutoa sauti kila baada ya siku mbili,’’ aliambia BBC News.
Bw Jorgewich-Cohen pia alipendekeza kwamba wanadamu wawe na upendeleo kwa viumbe wanaoishi ardhini na wakapuuza viumbe vilivyo chini ya maji.
Video iliyorekodiwa ya wanyama walipopiga kelele ilimruhusu kuunganisha sauti na tabia inayohusishwa - kutofautisha kutoka kwa sauti za bahati mbaya ambazo hazitumi ujumbe.
‘’Kasa wa baharini wataimba kutoka ndani ya yai lao ili kusawazisha kuanguliwa,’’ alieleza.
‘’Ikiwa wataita kutoka ndani, wote hutoka pamoja na wakiwa na matumaini wataepuka kuliwa.’’

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kasa pia hutoa kelele kuashiria wanataka kujamiiana, alisema, akionyesha video za sauti za kasa wanaopandana ambazo ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii.
Bw Jorgewich-Cohen pia alirekodi tuatara wakitoa sauti ili kulinda eneo lao.
Kisha akaanza kuzingatia ugunduzi huo ulichotambua kuhusu mabadiliko ya wanyama wanaofanya kelele.
Mara nyingi visukuku havielezi wanasayansi vya kutosha kuhusu wanyama walioishi mamilioni ya miaka iliyopita hivyo badala yake wanalinganisha tabia za wanyama hai.
Akitumia mbinu inayoitwa uchanganuzi wa filojenetiki, Bw Jorgevich-Cohen alifuatilia uhusiano kati ya wanyama wanaotoa kelele.
Mbinu hiyo inafanya kazi kwa kulinganisha tabia za spishi na kuzipanga kama historia ya majina ya familia yaani kuanzia baba, mama kwendelea.
Iwapo, kwa mfano, binadamu na sokwe wanashiriki tabia kama kupiga kelele, inapendekeza kwamba babu zao pia walitoa sauti.
Alihitimisha kwamba mawasiliano yote ya sauti katika wanyama wenye uti wa mgongo yalitoka kwa babu mmoja miaka milioni 400 iliyopita, ambayo ilikuwa kipindi cha Devonia wakati spishi nyingi ziliishi chini ya maji.
Hiyo inatofautiana na kazi ya hivi majuzi ambayo ilifuatilia sauti za mawasiliano kwa spishi kadhaa tofauti miaka milioni 200 iliyopita.

Chanzo cha picha, PATRICK VIANA
Mwanabiolojia Catherine Hobaiter, ambaye hakuwa sehemu ya utafiti huo, aliambia BBC News kwamba rekodi za spishi hizi 53 ni nyongeza ya kile tunachojua kuhusu mawasiliano ya sauti.
‘’Kulinganisha viumbe kama vile sokwe na binadamu huturudisha nyuma miaka milioni chache,’’ alisema.
‘’Tunahitaji kuona vipengele vya kawaida katika jamaa za mbali zaidi ili kurudisha uelewa wetu katika mamia ya mamilioni ya miaka.’’
Utafiti huo umechapishwa katika jarida la kisayansi la Nature Communications.















