Je, Marekani itakwenda umbali gani kuilinda Israel?

Marekani imeahidi uungaji mkono usioyumba kwa Israel wa msaada wa kijeshi. Katika majibu yake ya kwanza kwa shambulio la Hamas dhidi ya Israel, Rais Joe Biden aliweka wazi, "Marekani inaunga mkono Israel."

"Kwa yeyote anayefikiria kutumia fursa ya mgogoro huu, nina neno moja: Usifanye kitu," aliongeza. Onyo hili lililenga waziwazi Iran na washirika wake.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na Syria wameshambuliwa mara kadhaa katika siku za hivi karibuni. Pentagon inasema mifumo ya ulinzi wa anga imenasa katika bahari Nyekundu makombora yaliyorushwa kutoka Yemen, "yawezekana yakiilenga Israeli.''

Marekani tayari ina meli za kivita Mashariki ya bahari ya Mediterania. Kila kundi la meli hizo lina zaidi ya ndege 70 za kivita. Biden pia amewaweka maelfu ya wanajeshi wa Marekani katika hali ya utayari kwenda katika eneo hilo ikiwa itahitajika.

Marekani ndiye mfadhili mkubwa wa kijeshi wa Israel, ikitoa takriban dola za kimarekani bilioni 3.8 msaada wa ulinzi kila mwaka.

Ndege za Israel zinazoshambulia Gaza ni za Marekani, kama vile silaha nyingi zinazotumika sasa. Baadhi ya makombora ya mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel wa Iron Dome pia yanatengenezwa Marekani.

Marekani ilikuwa ikituma silaha hizo hata kabla ya Israel kuziomba. Na siku ya Ijumaa Rais Biden aliliomba Bunge la Congress kuidhinisha ufadhili wa dola bilioni 14 kwa mshirika wake wa Mashariki ya Kati kama sehemu ya mfuko wa msaada wa kijeshi wa dola bilioni 105.

Siku iliyofuata, Pentagon ilitangaza kutuma mifumo yake miwili ya ulinzi wa anga yenye nguvu zaidi Mashariki ya Kati - Terminal High Altitude Area Defense (THAAD) na ulinzi wa Patriot.

Je, ni kweli rais wa Marekani yuko tayari kujiingiza katika vita vingine, katika mwaka wa uchaguzi? Operesheni za kijeshi za Marekani katika eneo hilo zimeonekana kuwa na gharama kubwa - kisiasa, kiuchumi na kwa maisha ya Wamarekani.

Marekani iko tayari kwa vita?

Michael Oren, balozi wa zamani wa Marekani nchini Israel, anaamini Rais Biden tayari amechukua hatua ya kwanza ya kupeleka meli za kubeba ndege katika eneo hilo. "Hutoi aina hiyo ya bastola isipokuwa uko tayari kuitumia," anasema.

Lakini Seth G Jones, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Masomo ya Kimataifa huko Washington, anasema, ''Marekani itasita kujihusisha moja kwa moja kijeshi katika vita vya Gaza.''

''Kuwepo tu kwa meli hizo kuna manufaa bila kufyatua kombora, zinakusanya taarifa za kijasusi na kutoa ulinzi wa anga. Kuingia vitani moja kwa moja utakuwa uamuzi wa miwsho sana," anasema.

Tishio kubwa ni kutoka kaskazini mwa Israel, na haswa kutoka kwa wanamgambo wa kundi la Hezbollah, ambalo wanaitia wasiwasi Israel na Marekani.

Ni kundi linaloungwa mkono na Iran. Ni tishio zaidi kuliko Hamas. Lina takriban roketi 150,000 zenye nguvu zaidi na zinalenga kwa usahihi zaidi kuliko zile zinazotumiwa na Hamas.

Oren anahofia Hezbollah inaweza kuingilia kati wakati Israel "iko ndani Gaza inapambana na imechoka."

Iwapo hilo litatokea, Oren anaamini kuna uwezekano Marekani itatoa silaha zake kubwa za anga kulenga ndani ya Lebanon, ingawa haamini kwamba Marekani itaingia kijeshi ardhini.

Tumaini la Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin wote wamesema Marekani itajibu iwapo hali itakuwa mbaya na wanajeshi wa Marekani watashambuliwa.

Marekani ina haki ya kujitetea, alisema Austin siku ya Jumapili, na haitasita "kuchukua hatua inayofaa."

Jones anasema kama Hezbollah watashiriki katika operesheni kubwa ya mashambulizi kutoka kaskazini mwa Israel, "watarudishiwa mapigo."

Wala Israel haiombi msaada wa moja kwa moja wa kijeshi katika vita vyake na Hamas. Danny Orbach, profesa wa historia ya kijeshi katika Chuo Kikuu cha Hebrew, Jerusalem, anaeleza kwamba mafundisho ya kijeshi ya Israeli yanasema inapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda yenyewe.

Kuna mifano michache ya Marekani kuingilia mzozo kwa niaba ya Israel. Marekani ilituma ulinzi wa anga kuilinda Israel dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Scud ya Iraq, kabla ya uvamizi wake katika vita vya Ghuba vya 1991.

Ziara ya Rais Biden nchini Israel wiki hii ilionyesha kuwa msaada wa Marekani una masharti. Anataka Israel iruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, na hataki kuona Israel ikiikalia Gaza milele. Anasema kufanya hivyo itakuwa "kosa kubwa."

Usaidizi wa Marekani unaweza pia kuwa wa muda mfupi. Yaacov Katz, mchambuzi wa masuala ya kijeshi na mwandishi wa gazeti la Jerusalem Post, anaamini uungaji mkono wa Marekani kwa Israel utakumbana na ukosolewaji mara tu operesheni ya kijeshi itakapoanza huko Gaza na vifo vya raia kuongezeka.

Anadhani msaada unaweza kupungua ndani ya wiki. "Siioni Israel ikipata uungwaji mkono zaidi kutoka Amerika au ulimwenguni kwa mashambulizi ya ardhini ambayo hudumu kwa muda mrefu zaidi."

Marekani inatumai msaada wake wa kijeshi kwa Israel na uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo utatosha kuzuia mzozo huo kuenea.