Bernard Kamungo: Kutoka kambi ya wakimbizi Tanzania hadi kucheza dhidi ya Messi

Chanzo cha picha, FC Dallas
Bernard Kamungo alizaliwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu nchini Tanzania, Kamungo hakujifunza kucheza soka na mpira. Au mpira wowote ambao ungeutambua mara moja.
"Hatukuwa na pesa za kununua mpira," Kamungo anakumbuka. "Ilitubidi kutengeneza mpira wetu wenyewe kwa kutafuta njia na mabegi, au kitu, kutengeneza kitu kinachofanana na mpira. Na kisha mimi na marafiki zangu tunaweza kwenda mitaani na kucheza dhidi ya watu wengine.
Hapo zamani, Kamungo hakuwa na ndoto ya kucheza kitaaluma. Taa zenye kung'aa na sehemu zilizopambwa kwa kiwango hicho zilionekana kuwa mbali sana kuweza kuguswa. Ilibidi ajikite pale alipokuwa.
"Nilichokuwa nikijaribu kufanya ni kuishi tu," alisema. "Kucheza soka ilikuwa kwa ajili ya kujifurahisha."
Bahati ya Kamungo ilibadilika alipoingia miaka yake ya ujana. Kwa msaada wa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji, yeye na familia yake walihamia Abilene, Texas. Alikuwa na mali chache na Kiingereza kidogo, lakini yote hayo hayakuwa na maana. Kamungo alifurahishwa na mambo ya msingi.
"Ilikuwa ajabu kwangu kwa sababu tulipofika Abilene, familia yangu inaweza kupata kitu cha kutulisha. Na hiyo ndiyo yote niliyokuwa nikitafuta. Huko Tanzania, ilikuwa vigumu kwa wazazi wako kupata kitu cha kukulisha. Wakati mwingine unakula mara moja kwa siku na ndivyo ilivyokuwa. Lakini tulipofika Abilene, nilianza kula kama kawaida, sasa ningeweza kula mara tatu au nne kwa siku, chochote nilichotaka. Ilikua bora mara moja."
Safari ya Bernard Kamungo inaanzia kwa kaka yake, Imani Kamungo, ambaye aliamini kipaji cha soka cha mdogo wake.
Bernard alicheza soka katika Shule ya upili ya Abilene. Alikuwa nyota wa timu hiyo baada ya kujifunza mchezo huo kwenye mitaa ya kambi ya wakimbizi nchini Tanzania, ambapo familia yake iliondoka kwenda Texas wakati Bernard alipokuwa na umri wa miaka 14.
Miaka minne ya kutawala katika safu ya shule ya upili ilimfanya Imani aamini kwamba mdogo wake alikuwa amekusudiwa kufanya kitu kingine zaidi.
Bernard hakukubali: "Wakati huo, sikuwahi kujiona nikiwa mchezaji wa soka wa kulipwa."
Licha ya kusita kwa Bernard, Imani alimsajili kwa majaribio ya wazi na North Texas SC, timu ya akiba ya FC Dallas.
"Niliamini angeweza kuwa bora zaidi lakini hakuweza kujiamini. Kwa hiyo nilimsukuma kila siku.” alisema Imani.
Bernard aliwavutia waandaji wa jaribio hilo na akapata kandarasi. Kisha, alifunga dakika chache kwenye mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo "Bao hilo lilinifanya nilie."
Msimu uliofuata, aliiongoza timu hiyo na kuwa mfungaji bora na hatimaye akapata kandarasi ya timu ya wakubwa ya FC Dallas. Kuanzia soka ya shule ya upili hadi ligi kuu chini ya miaka miwili: "Nilitaka kuhakikisha kwamba anafikia kiwango cha juu lakini sikujua ingekuwa haraka namna hii.

Chanzo cha picha, FC Dallas
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
2023 ni Mwaka wa Bernard. Akiwa bado na umri wa miaka 21, alifunga bao la ushindi katika mechi yake ya kwanza nyumbani. Miezi michache baadaye, alifunga bao la ushindi kwenye mchezo wake wa kwanza kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Kombe la Ligi - michuano hii mipya kabisa unaoshirikisha kila klabu kutoka MLS na Liga MX - likawa jukwaa la Bernard kuonyesha jinsi alivyopambana toka mbali. Bao na asisti tatu katika mechi tatu, zilitosha kuonesha uwezo wake wa kuwa moja kati ya mawinga bora kwenye michuano hiyo.
Changamoto iliyofuata kwa Bernard na FC Dallas ilikuwa dhidi ya timu iliyojaa nyota wengi zaidi katika historia ya MLS. Inter Miami, inayowashirikisha wachezaji kama Lionel Messi, Sergio Busquets na Jordi Alba—wachezaji watatu ambao wameshinda kila kitu kwenye ngazi ya vilabu.
Uwanja wa Toyota huko Frisco, Texas ulikuwa uwanja wa mpambano wa hatua ya 16 bora. Bei za tiketi na watazamaji vilipanda hadi viwango ambavyo havija wahi kuonekana katika historia ya klabu hiyo.

Chanzo cha picha, FC Dallas
Haikuwa jambo kubwa sana kwa Bernard. Au Imani, ambaye aliongozana na kaka yake kwenye mchezo huo kwa mara ya kwanza.
Messi alianza kuitanguliza Miami. Mzalendo Facundo Quignon aliisawazishia Dallas. Kisha, ilikuwa wakati wa Bernard.
Jesús Ferreira alimpenyezea Bernard pasi safi kwenye ukingo wa kisanduku cha 18. Kwa utulivu kana kwamba bado yuko kwenye uwanja mdogo katika Shule ya Upili ya Abilene, au mitaa yenye vumbi ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Bernard alimpiga chenga safi beki wa kwanza kabla ya kumkwepa beki mwingine.Shuti la ustadi kutoka kwenye mguu wake wa kulia lilimshinda ustadi kipa wa Miami aliyekuwa na pupa golini na mpira kuingia wavuni.

Chanzo cha picha, FC Dallas
“Ndoto inaendelea,” alisikika mtangazaji wa mchezo huo.
Haukuwa usiku wa FC Dallas. Sare ya 4-4 baada ya dakika 90 ilisababisha mikwaju ya penalti ambapo Messi na wenzake walishinda.
Lakini bado ulikuwa usiku wa akina Kamungo. Imani alikuwa amemwona kaka yake - kaka yule yule ambaye alikuwa amemsukuma kujaribu klabu ya daraja la tatu miaka mitatu tu kabla - akifunga dhidi ya timu inayoongozwa na mchezaji mkubwa zaidi duniani.
“Sijui hata nielezee vipi. Ni moja tu ya nyakati hizo kwa sababu sijawahi kufunga mbele ya Imani. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufunga mbele yake, na ilikuwa dhidi ya Messi.
“Nilimgeukia na nikamwambia tu, ‘Bao hili lilikuwa kwa ajili yako.’ Kwa sababu alinifanyia mengi kufika hapa nilipo sasa hivi. Nina furaha sana ameniona nikifunga.”












