Linda Caicedo: Kutoka kupona saratani hadi kuwa nyota kinda wa Kombe la Dunia la Wanawake

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Saa 11 jioni siku ambayo alisaini Real Madrid mnamo Februari, Linda Caicedo hakusherehekea na familia na marafiki. Badala yake, binti huyo mwenye umri wa miaka 18 alikuwa akimpigia simu mgonjwa mchanga wa saratani aliyekaribia kufanyiwa upasuaji nyumbani kwao Colombia.

Hii Inaonyesha vipaumbele vya Caicedo ambaye ameweza kuwa mmoja wa nyota chipukizi wa Kombe la Dunia la Wanawake la Fifa 2023 uwanjani, lakini mbali na hilo anajua kuna mengi zaidi ya maisha kuliko soka.

Safari yake hadi sasa inajumuisha mchezaji wa kwanza wa kucheza timu ya taifa akiwa na umri wa miaka 14, uchunguzi wa saratani akiwa na umri wa miaka 15, na kuhamia moja ya klabu zinazojulikana zaidi duniani.

Hatua ya hivi punde zaidi ya safari hiyo ilikuja mjini Sydney, ambapo aliingia kama winga wa kushoto na kufyatua glavu za mlinda mlango Yoon Young-geul wakati Colombia ilipoilaza Korea Kusini katika mechi yao ya ufunguzi, na kufanikiwa kuisaidia Colombia kupata ushindi wao wa pili katika mashindano hayo ya Wanawake.

Bao la Caicedo linamaanisha, akiwa na umri wa miaka 18 na siku 153, anakuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kutoka Amerika Kusini kufunga bao katika historia ya michuano hiyo, huku Marta pekee wa Brazil akifunga bao akiwa na umri mdogo.

Kumhusisha Marta wakati wa kulinganisha wanasoka wa kike ni kauli kubwa mno lakini Caicedo anaonekana kuwa mtu sahihi.

Na aliiunga mkono kwa bao la kiwango cha kimataifa dhidi ya Ujerumani huku Colombia wakiwafunga mabingwa hao mara mbili 2-1 siku ya Jumapili.

Caicedo amekuwa msichana wa kuigwa kwa soka la wanawake nchini Colombia, ambao walifuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia mwaka 2011 lakini wamekua na nguvu tangu wakati huo.

Alizaliwa katika mji wa Candelaria, Caicedo alitoka katika malezi duni na hajawahi kusahau dhabihu zinazohitajika ili kufikia hatua hii. Hivi majuzi alisafiri hadi Candelaria na kutoa magunia 100 ya chakula kwa watu wanaohitaji, bila vyombo vya habari.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ana uhusiano wa karibu na meneja wa Colombia Nelson Abadia, ambaye amekuwa akiiongoza timu ya taifa tangu 2017 lakini alihusika kama msaidizi wa kiufundi kutoka miaka mitatu iliyopita.

“Mwaka 2016 nilianza na madaraja ya vijana, nilikuwa na Linda hapa, alikuwa na miaka 12 ndiyo kwanza nilimpeleka timu ya taifa,” alisema Abadia. "Ametokea huko."

Uwezo wa Caicedo ulimfanya acheze kwa mara ya kwanza katika klabu ya Colombia America de Cali mnamo Julai 2019, alipokuwa na umri wa miaka 14. Mnamo Novemba 2019, aliitwa kwa mara ya kwanza timu ya taifa.

Uwezo wake ulisimama mnamo mwaka 2020, katikati ya janga la Covid 19,Caicedo alianza kuhisi maumivu kwenye tumbo lake.

Kufuatia vipimo, aliarifiwa kuwa ana saratani ya ovari. Wiki mbili baada ya utambuzi huo, mnamo Machi 2020, Caicedo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe, ambao ulihusisha kuondolewa kwa moja ya ovari yake.

Caicedo ameweza kupona ugonjwa wake, ambao kwa kiasi fulani msaada kutoka kwa familia yake, na kocha wake wa timu ya taifa Abadia.

"Kulikuwa na mchakato mgumu, namshukuru Mungu niliweza kuushinda," alisema. "Familia yangu ilikuwa nyuma yangu kila wakati na kocha wangu kando yangu alikuwa karibu sana kila wakati.

"Yeye [Abadia] mara nyingi alikuwa akinipigia simu. Nilikuwa nikienda kufanyiwa upasuaji siku moja na nilijisikia vibaya sana, kana kwamba singeweza kucheza soka la kiwango cha juu tena; alisema pumzika, utarudi. Kwa hiyo nataka kumshukuru kocha wangu.

"Kwa watu walio katika nyakati ngumu kama mimi, mimi ni mfano unaweza kushinda hii."

Caicedo alianza matibabu ya mionzi kwa miezi sita baada ya upasuaji, na siku chache baada ya kumaliza matibabu - mara tu alipotangazwa kuwa hana saratani - alirejea kwenye mazoezi.

Alirejea uwanjani akiwa na Deportivo Cali na timu ya taifa. Akiwa mchezaji mwandamizi wa timu ya taifa, pia aliendelea kupata uzoefu katika mashindano ya vikundi vya umri.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Mnamo 2022, Caicedo alicheza vyema katika mashindano manne tofauti ya kimataifa - Mashindano ya Amerika Kusini ya Wanawake chini ya miaka 17, Kombe la Dunia la Wanawake wa U-20 nchini Costa Rica, Kombe la Dunia la Wanawake wa U-17 nchini India, na Copa America Femenina.

Ilikuwa katika michuano hiyo ambapo ulimwengu ulianza kumtazama Caicedo. Akiwa na umri wa miaka 17 alitawazwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo huku wenyeji Colombia wakifika fainali, ambapo walifungwa 1-0 na Brazil lakini alikuwa amefanya vya kutosha kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2023.

Februari 2023, siku chache tu baada ya Caicedo kufikisha umri wa miaka 18, alisajiliwa na Real Madrid, na kuwa mmoja wa wachezaji saba wenye asili ya Uhispania katika kikosi cha Colombia cha Kombe la Dunia.

"Unahitaji kuondoka katika nchi yako ili kubadilika, na uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki na wafanyikazi wa makocha hunisaidia sana," alisema. “Hivi ndivyo nilivyojihakikishia nafasi yangu Real Madrid.

"Nimecheza U17, U20, sasa kuwa kwenye Kombe la Dunia na wachezaji wenye uzoefu kama huu, uzoefu unachangia sana, nimejifunza kwa kila hatua, nahisi Kombe hili la Dunia litakuwa la mwili, ambalo nitajifunza kwa maarifa.

"Bado ni mdogo sana, bado nahitaji kujifunza mengi. Ninapata uzoefu kila siku katika timu hii. Hili ni Kombe langu la kwanza la dunia la wakubwa, nataka kulifurahia. Nina muda mwingi."

Kocha Msaidizi wa Colombia Angelo Marsiglia anaelezea Caceido kama "Mchezaji wa ajabu".

"Anataka mpira, hajifichi kamwe, anatoka sayari nyingine, ya kipekee kabisa," aliongeza