Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Ukiona mmoja, usimguse au kula': Marekani yatoa onyo dhidi ya konokono wenye asili ya Tanzania na Kenya
Konokono wakubwa wa Kiafrika wanaweza kuonekana kama wanyama waendao polepole na wasio na madhara.
Lakini, ukweli ni kuwa ni "moja ya konokono hatari zaidi duniani na kwa afya ya binadamu", hii ni kwa mujibu wa mamlaka nchini Marekani ambao wanawinda aina hii ya viumbe vilivyovamia sehemu ya ardhi ya nchi hiyo.
"Ni hatari kwa afya zetu kwa sababu hubeba vimelea vinavyoitwa lungworms, ambavyo vinaweza kusababisha homa ya uti wa mgongo kwa binadamu," Kamishna wa Kilimo wa Florida Nikki Fried alisema katika mkutano na waandishi wa habari mapema mwezi huu katika kaunti ya Pasco, magharibi mwa jimbo hilo.
"Wanakula karibu mimea 500 tofauti tofauti, ambayo inawafanya kuwa tishio la wazi kwenye kilimo na maeneo yetu ya asili."
Mbwa waliopewa mafunzo maalumu ya kunusa na timu ya angalau watu 30 wanafanya kazi ya kuwatafuta katika bustani za Florida ili kutokomeza viumbe hao vamizi.
Tangu wagunduliwe mwezi Juni, maafisa wamekamata zaidi ya konokono 1,400 walio hai na waliokufa katika Kaunti ya Pasco, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.
Konokono wakubwa wa Kiafrika wanaweza kukua hadi inchi nane na kuzaliana haraka. "Konokono mmoja mkubwa wa Afrika anaweza kutaga hadi mayai 2,000 kila mwaka," Jason Stanley, mwanabiolojia katika Idara ya Kilimo ya Florida aliiambia AFP.
Tishio kwa binadamu
Lakini je, binadamu pia wapo hatarini? Ndio kuna uwezekano huo, kulingana na wataalam.
Konokono hawa mara nyingi huwa na minyoo ya panya ambayo, ikiwa itamezwa na binadamu, inaweza kusafiri hadi kwenye shina la ubongo na wanaweza kusababisha homa ya uti wa mgongo.
"Kwa kawaida, haiathiri watu. Lakini ikiwa itaingia kwa binadamu kwa bahati mbaya, minyoo ambayo haijakomaa inaweza kupotea na inaweza kuishia mahali ambapo inaweza kufanya uharibifu mkubwa, kama ndani ya mboni za macho au hata ubongo," Anasema Dk. William Kern, Profesa katika Idara ya Entomology na Nematology katika Chuo Kikuu cha Florida.
Eneo la karantini limeanzishwa ndani ya New Port Richey, hakuna mimea au mimea mingine inayoweza kuondolewa kutoka eneo hilo ili kujaribu kuzuia konokono kuenea zaidi.
Ili kuzuia maambukizi, hata mbwa hufundishwa kutokamata konokono kwenye midomo yao.
Je, hii imewahi kutokea hapo awali?
Ndiyo. Mara ya kwanza walivamia katika miaka ya 1960. Ilichukua miaka saba na mamilioni ya dola kuwamaliza.
Ya pili ilitokea mwaka 2010 na safari hii ilichukua miaka kumi kuwaangamiza kwa gharama ya dola za Marekani milioni 23.
Ikiwa tu hakuna konokono aliyeonekana kwa miaka miwili, mamlaka inaweza kutangaza sehemu hiyo kuwa huru bila konokono hao.
Huko Ulaya, baadhi ya watu huweka konokono hawa kama wanyama wa majumbani, lakini nchini Marekani ni kinyume cha sheria kuwaweka bila leseni. Walakini, maafisa na wataalam wanashuku kuwa uvamizi huu unaweza kuwa kwa sababu ya wafanyabiashara wa wanyama wa kufugwa majumbani.
"Kuna uwezekano mkubwa kwamba mtu fulani aliwaleta kama wanyama wa nyumabani. Tuliowapata katika kaunti ya Pasco wana manyoya meupe badala ya rangi ya kawaida ya kijivu," Dk. Kern aliambia BBC.
Asili yao ni mashariki mwa Kenya na mashariki mwa Tanzania ingawa sasa wanapatikana katika maeneo mengi duniani ikiwemo Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia.
Idara ya Kilimo ya Marekani inasema, "Konokono hawa sasa wapo kwenye visiwa vingi vya Caribbeane, sehemu kubwa ya Amerika ya Kusini na hivi karibuni zaidi walipelekwa nchini Kosta Rika."
Haifai kula
Maafisa wa Florida sasa amewataka watu kuripoti tukio lolote la konokono hawa.
"Ukiona moja ya konokono hawa, usimguse. Tupigie. Wanabeba magonjwa kama homa ya uti wa mgongo," anasema Kamishna Nikki Fried. Pia anatoa onyo kwa wale ambao wangependa kuwaona kwenye sahani kuliko kwenye bustani.
"Jambo muhimu zaidi ni kwamba usile. Hao sio konokono wa kuweka siagi, mafuta na vitunguu."