Je, ipi ina faida zaidi, kuoga asubuhi au kabla ya kwenda kulala?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika ulimwengu huu unaozidi kuwa na mgawanyiko , kuna swali moja ambalo labda linatugawanya zaidi kuliko jingine lolote: Je, huwa unaoga asubuhi au usiku? Au labda wewe ni mmoja wa watu ambao hauogi kila siku.

Bila kujali msimamo wako, unaweza kujiuliza je chaguo lako lina athari gani za kiafya katika mwili wako .

Kwa wengi wetu, baada ya kuamka asubuhi na matongo, moja ya mambo ya kwanza tunayofanya ni kukimbilia kuoga.

Watetezi wa kuoga asubuhi mara nyingi hubishana kuwa kutumia dakika 10 chini ya maji ya moto huwasaidia kuamka wakiwa wameburudika na wako tayari kuanza siku.

Hata hivyo, wale wanaooga usiku hubishana kuwa kuoga kabla ya kulala huwasaidia kuondoa uchafu wa mchana kabla ya kuingia katika shuka na kulala kwa utulivu.

Lakini sayansi inasema nini kuhusu ni lipi chaguo bora na lenye manufaa kati ya hizo mbili ?

Maisha ya bakteria

Kuoga husaidia kuondoa uchafu, grisi na jasho kwenye ngozi yetu.

Ikiwa hutaoga kabla ya kulala, mabaki haya hutulia kwenye shuka na foronya zako.

Lakini si hivyo tu. Ngozi yako hujaa vijidudu.

Ukichunguza kwa karibu ngozi yako, utapata kati ya bakteria 10,000 na milioni moja wanaoishi humo. Wanakula mafuta yaliyofichwa na jasho lako.

Ingawa jasho lenyewe halina harufu, misombo ya sulfuri inayozalishwa na bakteria kama vile staphylococcus hutoa harufu.

Kwa hivyo, kuoga kabla ya kulala kunaweza kuonekana kama chaguo la usafi zaidi.

Lakini, kama kawaida, ukweli ni mgumu zaidi kuliko huo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wengi wanapendelea kwenda kulala wakiwa wameoga

"Ukioga usiku, unaenda kulala ukiwa msafi, lakini bado utatoa jasho usiku kucha," anasema Primrose Freestone, mwanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Leicester nchini Uingereza.

Kulingana na Freestone, hata katika hali ya hewa ya baridi, mtu bado hutoka jasho hadi nusu lita kitandani na kuweka seli za ngozi 50,000 kuwa chakula cha wadudu wachafu.

"Bado utaunda jasho ambalo bakteria kwenye ngozi yako huchukua na kusababisha harufu ya mwili. Kwa hiyo, unapoamka asubuhi baada ya kuoga usiku, bado utasikia harufu kidogo, "Freestone anasema.

Faida za kuoga usiku huonekana tu ikiwa unaosha matandiko yako mara kwa mara.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kubadilisha nguo za kulalia mara kwa mara ni muhimu ili kuzuia mkusanyiko wa vijidudu

"Pengine ni muhimu zaidi kuosha shuka zako kuliko kuoga usiku," anasema Holly Wilkinson, mhadhiri mkuu katika Uponyaji wa Jeraha na Microbiome katika Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.

"Kwa sababu ikiwa unaoga na kuacha shuka kwa muda wa mwezi mmoja, bakteria, uchafu na wadudu wa vumbi watakusanyika."

Hili huleta tatizo, kwani huongeza hatari ya mizio.

Inawezekana pia kwamba kulala mara kwa mara na nguo chafu huongeza hatari ya maambukizo ya ngozi, ingawa ushahidi haujathibitishwa.

Husaidia kulala vizuri usiku

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nukuu, Kupanda na kisha kushuka kwa joto la mwili baada ya kuoga maji ya moto usiku kunaweza kuwasaidia baadhi ya watu kusinzia kwa urahisi zaidi.

Baadhi ya wafuasi wa kuoga nyakati za usiku wanasema kwamba huwasaidia kulala vizuri, na kuna ushahidi wa kuunga mkono hili.

Kwa mfano, uchanganuzi wa meta uliolinganisha matokeo ya tafiti 13 uligundua kuwa kuoga kwa dakika 10 na maji au kuoga saa moja hadi mbili kabla ya wakati wa kulala kulipunguza sana muda wa kupata usingizi.

Inawezekana kwamba kuongeza joto la mwili kabla ya kupoa hutoa ishara kwa mwili kujiandaa kwa usingizi, ingawa utafiti zaidi unahitajika ili kuthibitisha hili.

Kwa hiyo, pamoja na habari hii yote, tunawezaje kujibu swali la ikiwa ni bora kuoga asubuhi au usiku?

Freestone anapendelea kuoga asubuhi, kwa kuwa hii itaondoa jasho jingi na vijidudu vilivyokusanyika usiku mmoja kitandani, ili kumuwezesha kuanza siku akiwa msafi.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla