Mfahamu mwanamitindo aliyegeuka kuwa mpiga picha aliyenasa mambo ya kutisha ya Vita vya Pili vya Dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
Kate Winslet alipambana kwa miaka minane kupata wasifu wake kuhusu mpiga picha wa vita wa Marekani Lee Miller, na wiki hii hatimaye ilipata kutolewa nchini Uingereza.
Lee anayezungumziwa ni mzaliwa wa Marekani Elizabeth "Lee" Miller, mwanamke wa ajabu ambaye maisha yake ya kupendeza na mara nyingi yaligubikwa na kazi yake ya upigaji picha.
Miller alikuwa mwanamitindo bora aliyeangaziwa katika majarida kama vile Vogue, Harper's Bazaar na Vanity Fair, lakini pia alikuwa mpiga picha muhimu na mwandishi jasiri wa masuala ya vita ambaye aliandika ukatili wa Vita vya Pili vya Dunia.
Lee Miller alizaliwa mwaka wa 1907 huko Poughkeepsie, mji mdogo wa viwanda takriban kilomita 140 kutoka jiji la New York nchini Marekani. Baba yake, Theodore, alikuwa mhandisi, mvumbuzi na mpiga picha mahiri ambaye alihimiza shauku ya Miller katika upigaji picha, akimnunulia kamera yake ya kwanza, aina ya Kodak Box Brownie, akiwa na umri wa miaka 10.
Miller alianza kujfunza mchakato wa upiga picha kwa kufuatilia kazi ya baba yake. Ni hapo ndipo alipata nafasi ya kujinadi kama mwanamitindo wa baba yake, ambaye alipiga maelfu ya picha yake tangu alipozaliwa hadi mtu uzima.

Chanzo cha picha, Studio Canal UK
Miller, mwanamke mchanga na mchangamfu, alichoshwa na maisha huko Poughkeepsie hali iliyomfanya kumshawishi baba yake kumruhusu kwenda kwa masomo jijini Paris mnamo 1925, akiwa na umri wa miaka 18.
Aliporudi New York mwka 1926, alipata fursa ya kukutana na mwanzilishi wa jarida la Vogue Condé Nast, ambaye alivutiwa sana na ustadi na urembo wa Miller hivi kwamba aliomba kumuangazia katika jarida hilo.
Wakati wa miaka ya 1920 na 1930, Miller alifanya kazi na baadhi ya wapiga picha muhimu zaidi wa mitindo wa zama hizo, wakiwemo Edward Steichen na George Hoyningen-Huene. Hata hivyo, siku zote alipendelea kuwa nyuma ya kamera badala ya kuwa mbele yake.
Ni Steichen ambaye alimtambulisha kwa mwandishi wa Marekani, Man Ray, ambaye alikuwa akifanya kazi kama msanii na mpiga picha wa kibiashara huko Paris.

Chanzo cha picha, Getty Images
Miller mara kwa mara alikubali kufanya kazi za upigaji picha za kibiashara kutoka kwa Man Ray ili aweze kuzingatia miradi yake ya kisanii, ingawa picha hizo zilichapishwa Miller hakupewa haki miliki.
Pia alikuwa kiungo muhimu katika ugunduzi wa mchakato wa upigaji picha unaofahamika kama solarization, ambao hutoa “muundo wa picha ambazo baadhi ya sehemu zinazingatia zaidi maumbile ya mwili,” ambayo kwa miaka kadhaa ilihusishwa na Man Ray.
Mnamo 1932, Miller alirudi New York, ambapo alifungua mradi wake wa biashara, Lee Miller Studios Inc., kabla ya kuhamia Misri mnamo 1934 kuolewa na mfanyabiashara tajiri wa Misri Aziz Eloui Bey.
Misri ilimhimiza Lee kuunda picha nyingi za uandishi, ikiwa ni pamoja na kazi yake ya 1937 "A Portrait of Space." Lakini, kukaa kwake Misri kulikuwa kwa muda mfupi, kama vile ndoa yake na Aziz.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupiga picha za vita
Lee alikutana na surrealist wa Uingereza Roland Penrose huko Paris mnamo 1937 na alitumia wakati wa ziara yake kusini mwa Ufaransa, ambao ilijumuisha Man Ray, mshairi Paul Eluard na Pablo Picasso, ambaye alichora picha yake ya kukumbukwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Miller alihamia London na Penrose mnamo Septemba 1939, Uingereza ilikuwa ndio mwanzo imetangaza vita dhidi ya Ujerumani. Kama mpiga picha mwenye tajiriba ya uandishi, London Blitz ya 1940 ilimpa fursa ya kusisimua ya kunasa mambo ya ajabu ya vitani.
Picha zake 22 za milipuko hiyo zinaonekana katika chapisho la Wizara ya Habari la 1941 "Grim Glory: Pictures of Britain Under Fire".
Mnamo 1942 alipata kibali kutoka kwa Jeshi la Marekani kuwa mmoja wa waandishi wachache wa kike wa vita kusafiri na jeshi huko Ulaya.
Miller pekee ndiye aliyepiga picha ya vita na kushuhudia kuzingirwa kwa Saint Malo, ambapo Wamarekani walifanyia majaribio silaha yao mpya ya siri, napalm. Picha za Miller zilichapishwa picha katika jarida la Vogue la Uingereza na Marekani.
Mhariri wa Vogue wa Uingereza Audrey Withers hakutaka tu kuangazia mada za mitindo na urembo, bali pia kuwafahamisha wasomaji wake kuhusu habari zinazojiri na masuala ya kijamii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miller na Withers walifanya kazi kwa karibu ili kubadilisha jarida la mitindo na mtindo wa maisha kuwa kitu ambacho pia kiliangazia kile kinachotokea ulimwenguni, kuchapisha nakala za mitindo pamoja na hadithi na picha kutoka vitani.
Miller daima alilenga kuonyesha ukweli katika upigaji picha wake wa vita. Katika picha zake za ukombozi wa kambi za mateso za Buchenwald na Dachau mnamo Aprili 1945, aliangazia ukatili wa utawala wa Nazi.
Siku moja baada ya kupiga picha Dachau, aliweka picha yake maarufu wakati wa vita, iliyopigwa na rafiki yake na mfanyakazi mwenzake, mpiga picha wa gazeti la Life David E. Scherman. Picha hiyo inamwonyesha Miller akioga katika bafu ya Hitler nyumbani kwake huko Munich, akionekana mchovu lakini ni mrembo, buti zake zikiwa zimetupwa sakafuni na picha ya Führer ikiegemea mabomba.
Baada ya vita, mnamo 1947, Miller alipata ujauzito na kujifungua mtoto wake wa pekee, Antony Penrose, mwandishi wa "The Lives of Lee Miller," ambayo imeangaziwa katika filamu ya Winslet, na kuolewa na baba yake, Roland Penrose.

Chanzo cha picha, Lee Miller Archive
Mnamo 1949 walihama kutoka London hadi Farley Farm katika kijiji cha Sussex Mashariki, ambapo Miller alijitolea katika nyanja ya ndani na kuwa mpishi na mhudumu aliyekamilika.
Picha alizoziona wakati wa vita zilimsumbua kwa maisha yake mpaka aakaanza kutegemea pombe ili kupata utulivu hadi akapatikana na ugonjwa unaotokana na kiwewe cha muda mrefu.
Miller alikufa katika shamba la Farley mnamo 1977, akiacha urithi wa ajabu wa picha ambayo imekuwa mada ya maonyesho mengi.
*Lynn Hilditch ni Profesa wa Sanaa Nzuri na Mazoezi ya Usanifu wa Praxis, Chuo Kikuu cha Liverpool Hope, Uingereza.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












