Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Kauli mbiu ya ‘wanawake tunaweza’ ifike kikomo
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC News Dar es Salaam
Baba yangu alinihamasisha nisome shule ili niwe huru na nifike hatua fulani katika maisha.
Na hivi karibuni nimebaini kuwa lengo la kusoma shule si kupata cheti na kazi bali tunasoma shule ili tupate fedha, ukiajiriwa au kufanya biashara unatafuta pesa. Si tu kuajiriwa ndiyo kupata fedha au usome ndiyo ufanye biashara.
Hayo ni maneno ya utangulizi ya Cikay Richard mwenye historia ya kufanya kazi tafauti: kuanzia kuwa mtaalamu mwelekezi wa masuala ya uongozi, maenedeleo ya kimataifa, uwekezaji & uwezeshaji wa biashara na uongozi usio wa kutengeza faida ya kifedha.
Ni mwanzilishi na mshirika Rehoboth Advisory, Afisa mtendaji wa kampuni ya Lyra Africa Tanzania, na mtaalamu mwelekezi wa zamani wa EY - Switzerland, Mkurugenzi mtendaji wa European Business Group Tanzania katika ubalozi wa Ireland.
“Unaweza usisome na ukapata fedha lakini fikra ambazo ungeweza kupata kutoka shuleni utazikosa”.
Katika maisha yetu ya kila siku, ni muhimu kuishi kwa malengo; ni muhimu kuwa na mpango mkakati kuhusu elimu ya fedha binafsi, kazi na familia.
Kuwa na usimamizi mzuri wa fedha ni jambo muhimu sana.
Ni Lazima kuwa na mpango kazi wa maisha yako na fedha zako pia na kuweka akiba ya fedha yako.
Ukishapanda basi unakuwa anajua anaelekea wapi, huwezi kupanda tu basi bila kujua uelekeo wako.
Ni vyema kuelewa mpango kazi na suala unalotaka kutekeleza pamoja na matokeo yake.
Mimi ni kiongozi ninayeongozwa na malengo.
Kuwa na lengo ni kujua unakwenda wapi, unataka kufanya nini unataka kufanyaje hilo jambo ndiyo huo uongozi bora.
Ninaongozwa kwa malengo chanya katika jamii, sifanyi kazi ilimradi nifanye kazi ila kazi iwe na athari chanya katika jamii yetu.
Uthubutu na kujiamini.
Uthubutu na kujiamini, ni suala ambalo ninalipenda tangu nikiwa mdogo na nina uwezo wa kulifanya kwa weledi.
Nimeongoza makampuni na mashirika mbalimbali pamoja na harakati mbalimbali za maendeleo pia zimenipa uwezo na weledi katika nafasi ya uongozi.
Elimu imechangia makuzi yangu, kama mtoto wa kike nililiyeelimika, elimu imenisaidia kufungua mlango mmoja ama mwingine.
Mfano kwenye utashi wangu wa kujieleza na kujitambua, hayo ni matunda ya kupata elimu.
Elimu haikupi tu cheti bali inakufundisha mambo mengi katika maisha kwa kusaidia katika kumuweka mtu katika nafasi fulani.
Wanawake tayari tumeshaweza
‘Wanawake wakiwezeshwa wanaweza, kwa maoni yangu naona tutoke katika hizi kauli sasa.
Katika kipindi cha mwezi wa tatu, kuelekea sherehe za siku ya wanawake duniani, misemo hii huwa inatawala.
Ila kusema kweli wanawake tunaweza, tunapaswa kusema kuwa ‘wanawake tunaweza na tunafanya na tuko katika wakati wa utekelezaji.’
Si kwamba tunaweza ni kuwa tumeshaweza.
Wanawake wengi niliokutana nao katika kazi, kiukweli wana uwezo mkubwa na wanaweza kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja na hicho ndio kipaji pekee ambacho mwanamke yuko nacho kwa asili.
Wanawake tuna uwezo wa kuongoza kwa kutumia uwezo wetu kwa kujielewa wenyewe na kuelewa watu wengine. Wanawake wana uwezo tofauti sana katika utendaji.
Malezi na makuzi ni muhimu sana katika maisha
Nimelelewa na mama shupavu, mwanamke ambaye aliishi kabla ya wakati wake nadhani. Katika kipindi chake, mama yangu alikuwa wa kwanza kuvaa suruali katika jamii ambayo kuvaa suruali ilikuwa ni mwiko. Yeye alisema nguo haimuoneshi mtu ni wa aina gani na wanawake wanaruhusiwa kuvaa nguo wanazozitaka.
Na alikuwa anahoji kwa nini ni hivi kwa wanawake na wanaume ni tofauti
Aliweza kutueleza pia sisi kama watoto wa kike, tusikubali jamii ikwambie wewe unaweza wapi na unaweza kufika wapi.
Wanawake wana uwezo wa kujua ni nini wanaweza kufanya na wanaweza kujua wapi wanataka kufika.
Ni vyema, usisubiri mtu akwambie kuwa hapa wanawake wanaruhusiwa na huku wanawake hawaruhusiwi, Hii nyama inaliwa na wanaume tu na wanawake hawaruhusiwi kula.
Heshima ni muhimu na kuheshimu mtu ni muhimu mila na desturi pia ni muhimu lakini pale ambapo mwanamke amewekwa pembeni, usiwe muoga wa kusimama na kuzungumza.
Tunafikiria changamoto zaidi ya fursa
Inabidi kwanza kufikiria changamoto tunazifanyaje ziwe fursa, kwa fikra hizo tungeweza kupata matokeo chanya zaidi. Kuna ofisi ambazo unaweza kwenda sehemu usihudumiwe kama wanaume wanavyoweza kuhudumiwa.
Lakini tukiamua kuongelea maendeleo kwa kuangalia mwanamke anafanya hiki, kufanikiwa basi hata watoto wadogo wa kike wataona na wataiga kila wanachoona. Hata wanaume pia wanapitia changamoto ila jambo la muhimu ni tufikirie fursa zaidi, fikra zetu zitakwenda upande wa chanya zaidi.
Kuna wakati nilipata wazo la kuandaa mkutano la kuleta wawekezaji kutoka ulaya.. watu wengi hawakunielewa, maswali yalikuwa mengi zaidi ya majibu. Kila mtu alikuwa anahoji nitawezaje, lakini nilipambana mpaka nikawaleta wawekezaji 350. Nilijisikia vizuri sana na niliona ni ushindi mkubwa sana.
Ustahimilivu
Ustahimilivu umenisaidia sana katika kazi zangu na ustahimilivu ni jambo muhimu sana kwa wakati wote. Hata kwenye mambo ya familia, usiache mtu akwambie haiwezekani wewe jaribu ushindwe na ujue ulikosea wapi na ujirekebishe wapi.
Kushindwa si chaguo katika yote tunayofanya kusema nimeshindwa hapana. Mimi staki kushindwa ila nimewahi kushindwa mara kadhaa. Lakini nimejifundisha kuwa kuanguka si shida, ila unavyoinuka unainuka vipi?
Mara nyingi nimeanguka mfano kwenye shughuli za kilimo, nimeanguka sana lakini nina aminini kuwa nina mchango katika kushiriki katika kutengeneza chakula cha dunia. Na nimeendelea kuwa na ustahimilivu na kupambana bila kukata tamaa.
Kila mtu anaweza kuweka mizani kati ya familia na kazi
Kazi yangu inanifanya nijivunie sana haswa pale ninapokabidhi kazi yangu na kuhakiksha kuwa nimeifanya vizuri na kwa weledi. Weledi wa kazi yangu umezaa matunda makubwa kwa kuweza kupata kazi nyingi zaidi, watu wengi wanaokuja kufanya kazi na mimi wanakuwa wameshauriwa na mtu mwingine.
Pia kuwa mama, ni jambo linalonifurahisha na mimi kama mama ninajivunia sana. Watoto ni mafanikio katika maisha yangu.
Mimi ni mama mkali ila nafikiri ni muhimu kuwa ni vyema watoto wakalelewa katika malezi bora ambayo wazazi wanawaheshimu watoto na watoto pia wanawaheshimu wazazi. Yaani iwe kwenye pande zote mbili. Hii inasaidia kujenga jamii bora yenye kumcha Mungu na upendo.
Watoto wangu wanakwenda na mimi mpaka kwenye mikutano. Mtoto wangu wa kwanza ameanza kwenda kwenye mikutano na mimi akiwa na umri wa miaka mitatu na sasa ana miaka 17.
Ninaona kuwa jinsi ninavyomshirikisha, na yeye pia anajifunza kuwa kazi inafanyika kwa namna gani, ni muhimu kujiwekea mfumo ambao utafaa kuwa mzani mzuri wa kazi na familia.
Kiongozi mwenye lengo anayejivunia kupokezana kijiti na vijana wengine
Mimi ni mshauri wa kitaaluma ninayefundisha vijana na ninajivunia kuwa sehemu ya kubadilisha Maisha ya vijana.
Ninaamini kuwa njia unayopita leo na mtu mwingine alipita hivyo ni muhimu kuwa na watu hawa watatu katika maisha yako:
1.Mshauri(Mentor)
2.Mfadhili wa kitaaluma (Career sponsor)
3.Kocha (Career coach)
Hawa wote watatu, unaweza kujichagulia au inategemea na mazingira yako ya kazi na weledi wako.
Mfano kocha wa taaluma, ni mtu ambaye anakufundisha vitu ambavyo huna yaani labda umepata wadhifa mpya wa kuwa mkurugenzi, kocha anakusudia kukuongoza.
Wakati, mfadhili wa kitaaluma ni mtu ambaye anakuongelea vizuri kuhusu ujuzi wako, atapendekeza jina lako katika fursa mbalimbali anapozisikia.
Na vilevile kuna namna mbalimbali ya kukutana na hawa watu. Mtu anaweza kuja kwako, kuomba uwe mshauri wake na muhimu kusema kuwa unaweza au huwezi.
Lakini ikumbukwe kuwa hawa watu ni tofauti na suala la ushawishi au inspiration or motivation speaker kwa lugha ya kigeni. Kuona kazi ya mtu mtandaoni hakumaanishi kuwa anaweza kuwa mshauri kwako. Ingawa kuna ule msemo fanya ninachosema na si matendo. Kuna uhitaji wa werevu kuchagua mtu wa kukuongoza.
Kocha wa kitaaluma ni mtu ambaye amesomea na ana cheti kabisa, na wanatoa huduma hizi kwa kulipia. Nina furaha kuwa nimefundishwa kazi na wanawake, nami ninaweza kupokeza kijiti kwa vijana wengine.
Muhimu ni kuwa kiongozi ni muhimu kuwa na lengo ili utoe athari chanya kwa vijana. Ni muhimu kujielewa kwenye kazi, familia, na mpangilio wa kifedha wa jinsi zinavyoingia na kutoka.
Imehaririwa na Florian Kaijage