Putin atapokutana na Xi, kila upande unataka nini?

NASA

Chanzo cha picha, AFP

Kiongozi wa Urusi Vladimir Putin na Xi Jinping wa china wote wanafanya safari nadra nje ya nchi wiki hii na wanatazamiwa kukutana katika mkutano wa kilele nchini Uzbekistan.

Viongozi wa India, Pakistan, Uturuki na Iran (na wengine) pia watakuwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) huko Samarkand kuanzia Septemba 15-16, lakini Kremlin imeangazia mkutano huo na kiongozi wa China kama una "umuhimu maalum" .

Viongozi hao wawili walikutana mara ya mwisho kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi mjini Beijing mwezi Februari, ambapo walitoa taarifa ya pamoja wakisema urafiki kati ya nchi zao "hauna kikomo" na Urusi iliivamia Ukraine siku chache baadaye lakini je, mambo yamebadilika?

BBC inaangalia ni nini hasa ambacho Moscow inatafuta katika mkutano huu, na kile ambacho Beijing inaweza kupata kutoka kwake pia.

Kwa Rais Putin, uhusiano wa karibu na Beijing ni sehemu muhimu ya maono yake katika ulimwengu mpya wa "multipolar" ambapo mataifa kama vile Urusi na China yatafunika ushawishi wa Magharibi kote ulimwenguni.

Sera hii ni sehemu ya msingi ya utawala wake na ameifuata kwa miaka mingi, lakini sasa imekuwa muhimu zaidi kwa Kremlin.

Baada ya Vladimir Putin kuivamia Ukraine, ameepukwa na kutengwa na nchi za Magharibi na hivyo anatamani kuonekana akikutana na viongozi wakubwa na wanaotikisa dunia kama vile Xi Jinping. Ingawa, ni zaidi ya kinachooneka kwa macho kwamba kukutana na kiongozi wa China kuwa ni muhimu sana kwa rais wa Urusi.

NASA

Chanzo cha picha, AFP

Atapendezwa sana na uwekezaji wa China, teknolojia na biashara baina ya nchi mbili, ikizingatiwa kwamba vita vyake dhidi ya Ukraine vimesababisha wimbi kubwa la vikwazo dhidi ya Urusi. Baada ya kuondoka kwa makampuni ya Magharibi, Vladimir Putin ana nia ya kutafuta mbadala na makampuni ya Kichina.

Wakati nchi za Magharibi zinajaribu kupunguza utegemezi wake kwa mafuta na gesi ya Urusi, Moscow itakuwa ikijaribu kuelekeza usambazaji mashariki, hadi China.

Moscow pia inatamani sana kupatiwa silaha kusaidia kampeni yake iliyokwama nchini Ukraine, lakini licha ya matamshi ya kuunga mkono China imekuwa ikihofia sana kuisaidia Urusi katika nyanja hiyo.

Walakini, sera hii ya kutafuta uhusiano wa karibu na China ina mitego kwa kiongozi wa Urusi. Nchi hizo mbili zimesalia kuwa wapinzani wa kijiografia na kisiasa na ndani ya nchi, Rais Putin ameshutumiwa kwa kuruhusu ushawishi wa China kukua katika maeneo ya mashariki mwa Urusi.

NASA

Chanzo cha picha, AFP

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Safari ya Xi Jinping kwenda Uzbekistan (na Kazakhstan) ni safari yake ya kwanza ya kigeni tangu janga la Covid-19 lianze mnamo 2020.

Inafanyika kabla tu ya Mkutano wa 20 wa Kitaifa wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) unaotarajiwa kufanyika Oktoba 16, ambapo Xi anatarajiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa tatu ambao haujawahi kutokea.

Wakati vyombo vya habari vya serikali ya China bado havijatoa maelezo zaidi kuhusu mkutano wowote na Putin, vyombo vya habari vya Taiwan na Hong Kong vinaona kuhudhuria kwa Xi katika mkutano huo kama njia yake ya kuashiria kwa ulimwengu kwamba ana udhibiti kamili wa chama na nchi.

Shirika la Habari la Taiwan linaloshirikiana na serikali pia linaona uwezekano wa "aibu", kwani safari hiyo inaambatana na matukio ya hivi karibuni nchini Ukraine, ambayo yameshuhudia wanajeshi wa Urusi wakiondolewa katika maeneo makubwa waliyokuwa wameyateka hapo awali mashariki mwa nchi hiyo.

Mwanadiplomasia mkuu wa China Yang Jiechi hivi karibuni alithibitisha mshikamano wa Beijing na Moscow katika mkutano na Balozi wa Urusi anayemaliza muda wake Andrey Denisov na Li Zhanshu, afisa wa ngazi ya tatu wa Chama cha Kikomunisti cha China, alifanya "ziara ya nia njema" nchini Urusi mapema Septemba.

Yang na Li wanatarajia China na Urusi kujenga uhusiano zaidi - "watapandishwa kwa kiwango kipya", kulingana na Li.

Beijing, hata hivyo, imekuwa makini kudumisha "msimamo wa kutoegemea upande wowote" kwenye vita vya Ukraine. Inahitaji kuungwa mkono na Moscow huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa udhibiti wa nchi za Magharibi, lakini haitaki kuonekana kuwa karibu sana na Putin.

Huku vita vya Putin nchini Ukraine vikichukua sura mpya na kuzidi kuwa vibaya na kumekuwa na wito kupitia Twitter kutaka ajiuzulu, ombi lililotiwa saini na madiwani kadhaa wa Urusi, mkutano wa Xi na mtu ambaye aliwahi kumwita "rafiki wa karibu" utaangaliwa kwa umakini zaidi.

Je, Xi atajitenga zaidi na kiongozi huyo wa Urusi au atatoa msaada wake ili kuepuka kutengwa zaidi ikiwa Putin atashindwa?