Mjane wa Navalny 'mwenye msimamo na jasiri'

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Robert Greenall
- Nafasi, BBC News
Yulia, mke wa Alexei Navalny, kwa muda mrefu aliishi kwa faragha akisisitiza kuwa jukumu lake kuu lilikuwa la mke na mama sio mwanasiasa.
Lakini kutokana na kifo cha mume wake siku ya Ijumaa na wito wake wa hisia kali ya kutaka haki ipatikane katika Kongamano la Usalama la Munich, amejitokeza kama kiongo muhimu wa upinzani unaoibuka nchini Urusi ambao haukutarajiwa.
Licha ya jukumu lake hapo awali, Bi Navalnaya amekuwa mfuasi muhimu wa mume wake, na alisaidia sana kumtoa Urusi kwa matibabu ya dharura alipotiliwa sumu ya neva inayofahamika kama Novichok mwaka 2020.
Ametambuliwa kama "First Lady" wa upinzani wa Urusi.
Na Alexei mwenyewe aliwahi kusema kwamba hangeweza kuendelea na vita vyake vya kukatisha tamaa na vya upande mmoja dhidi ya Kremlin bila yeye.
Hadithi yao ya upendo wa hadharani na maisha ya familia - wana watoto wawili - imeonekana kama msukumo kwa wafuasi wao.
Yulia Ambrosimova alizaliwa Moscow mnamo 1976, binti ya mwanasayansi anayeheshimika Boris Ambrosimov.
Amesomea na kuhitimu masuala ya uchumi, alikuwa akifanya kazi benki lakini aliacha kazi ili kulea watoto wao wawili Alexei alipopata umaarufu kama mwanasiasa wa upinzani.
Walikutana wakiwa likizo nchini Uturuki mnamo 1998 na kuoana miaka miwili baadaye. Wakati huo hawakutarajia Alexei angepata umaarufu mkubwa kiasi hicho.
"Sikuolewa na wakili tajika au kiongozi wa upinzani. Niliolewa na kijana anayeitwa Alexei," aliambia gazeti la kila wiki la Urusi la Sobesednik mnamo 2020.
Inaonekana Bi Navalnaya alishiriki siasa za Alexei tangu mapema - katika miaka ya 2000 wote walikuwa wanachama wa chama cha kiliberali cha Yabloko.
Lakini aliishi maisha ya faragha hadi mumewe alipotiliwa sumu mnamo 2020, akionekana mara moja moja hadharani au akitoa hotuba.
Mumewe alipoumwa katika jiji la Siberia la Omsk mnamo Agosti mwaka huo, alimwandikia Rais Putin moja kwa moja, akiomba aachiliwe kwa matibabu nchini Ujerumani.
"Kila wakati tulipokuwa huko, nilifikiri 'nilipaswa kumtoa'," aliambia mtengenezaji wa filamu wa Kirusi Yuri Dud.
Navalny aliweza kutoka nje ya Urusi, kwa msaada wa shirika la hisani la Ujerumani.
Yulia alirudi naye Moscow miezi kadhaa baadaye baada ya matibabu yake, na kumwona akikamatwa mara moja. Muda uliobaki wa maisha yake aliutumia gerezani.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Balozi wa zamani wa Marekani nchini Urusi Michael McFaul, ambaye alimtaja Yulia kama mtu "mwenye msimamo na asiye na woga", alisema wakati huo kwamba kutakuwa na shinikizo kubwa kwake kuchukua jukumu la umma, na kwamba alikuwa na "sifa zote".
"Navalny hangeweza kuwa na mshirika bora maishani kuliko Yulia Navalnaya. Anashiriki imani yake, ushujaa wake, kutoogopa kwake," aliuambia mtandao wa NBC wa Marekani.
"Pia amewalea na kuwalinda watoto wao wawili kwa njia ambayo imezua sifa kubwa miongoni mwa wafuasi wa demokrasia nchini Urusi. Bila shaka, Yulia aliokoa maisha ya mumewe msimu uliopita wa majira ya joto."
Bi Navalnaya alisema hivi majuzi hatafuata njia ya Svetlana Tikhanovskaya, kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni ambaye alikuja kuwa mgombea urais baada ya mumewe kufungwa kabla ya uchaguzi wa 2020. Bi Tikhanovskaya anachukuliwa kuwa alishinda kura ambazo zilichakachuliwa kwa niaba ya aliyemaliza muda wake, Alexander Lukashenko.
Lakini hotuba yake huko Munich na hotuba iliyofuata kwa wafuasi kwenye mitandao ya kijamii (kwa Kirusi), zote zilizojaa hisia, zinapendekeza kuwa anaweza kubadilisha mawazo yake.
"Tunachohitaji ni Urusi huru, yenye amani na furaha. Urusi ya ajabu ya siku zijazo mume wangu aliitazamia sana," anasema katika ujumbe wa video.
"Hiyo ndiyo nchi ninayotaka kujenga pamoja nanyi. Nchi ambayo Alexei Navalny alifikiria," anaendelea.
"Hiyo ndiyo njia pekee - hakuna nyingine - aliyojitolea kupigania bila kupepesa macho, na bila shaka haitakuwa bure."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












