Kesi ya kumuondoa madarakani Rais wa Marekani Joe Biden ni ya aina gani?

Spika wa Bunge la Marekani Kevin McCarthy kutoka chama cha Republican, Kevin McCarthy ameamuru rasmi uchunguzi wa kumuondoa madarakani Rais wa Marekani Joe Biden, akidai amegundua ufisadi unaomzunguka.

Alisema uchunguzi utajikita katika miamala haramu ya biashara na ikiwa rais Biden alinufaika na biashara za mtoto wake, Hunter Biden.

Kamati ya Republican imekuwa ikichunguza kwa miezi kadhaa lakini haijapata ushahidi thabiti kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi dhidi ya Biden. Wanademokrasia wamekanusha madai hayo dhidi yake.

Madai ambayo kamati ya uchunguzi huenda ikayazingatia:

Pesa kwa familia ya Biden

Kamati ya Uangalizi ya Bunge ilisema katika hati iliyotolewa Agosti - familia ya Biden na washirika wao walipokea zaidi ya dola milioni 20 kutoka nchi kama vile China, Kazakhstan, Ukraine, Urusi na Romania.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutoka Republican, James Comer alieleza kwamba Hunter Biden alipokea mamilioni ya dola kutoka kwa matajiri kwa kutumia ushawishi wa Joe Biden, ambaye alikuwa makamu wa rais wakati Barack Obama alipokuwa rais. Lakini Comer bado hajatoa ushahidi.

Katika tangazo jingine la Agosti 9, Comer alieleza kwamba Joe Biden alikula katika mkahawa wa kifahari huko Washington DC na matajiri kutoka ulimwenguni ambao walikuwa wametuma pesa kwa mwanawe.

Kamati ilipata jumbe tatu tofauti kulingana na rekodi za benki. Lakini, kamati imeshindwa kuona malipo yoyote maalumu kwa Joe Biden. Pia, haikuweza kupata ushahidi kwamba Biden alinufaika moja kwa moja na matajiri hao.

Uchunguzi uliochapishwa na Washington Post Agosti - uligundua kuwa ni milioni saba tu ndio zilikwenda kwa familia ya Biden, hasa mtoto wa Biden, Hunter. Lakini Comer na wabunge wengine wa chama cha Republican wameishutumu familia ya Biden kwa kupata dola milioni 20.

Jina la Joe Biden

Mshirika wa zamani wa biashara wa Hunter Biden, Devon Archer, alisema Joe Biden alizungumza kwa simu takriban mara 20 katika kipindi cha miaka 10 na washirika wa kibiashara, wakiwemo raia wa kigeni.

Lakini, Devon alieleza kwamba simu zote zilikuwa za mazungumzo ya kawaida na shughuli za biashara za Hunter Biden hazikutajwa hata mara moja.

Warepublican wanasema taarifa za simu zinakinzana na madai ya Joe Biden kwamba hakuwahi kujadili shughuli za biashara na Hunter.

Ushahidi wa Devon Archer ulishindwa kueleza mgongano wa kimaslahi wa Biden, ripoti ya bunge ilieleza.

Mpango wa rushwa

Warepublican pia wanachunguza habari zisizo rasmi ambazo FBI ilipokea kwamba Joe Biden alijaribu kuzuia uchunguzi unaoendelea kuhusu Burisma, kampuni ya nishati ya gesi ya Ukraine ambapo Hunter Biden ni mwanachama wa bodi.

FBI ilipokea habari kwamba Joe Biden aliishinikiza serikali ya Ukraine kumwachisha kazi mwendesha mashtaka mashuhuri aliyehusishwa na uchunguzi huo.

Habari hizo ziliibuka wakati wa kesi ya kumfungulia mashtaka Rais wa wakati huo Donald Trump - 2019.

Seneta wa chama cha Republican Chuck Grassley, ambaye alipata hati ya FBI, alifichua maelezo hayo mwezi Julai.

Kulingana na hati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa kampuni ya Burisma, Mykola Zlockewski alisema kuwa alilipa dola milioni 5 kwa Joe Biden na Hunter Biden.

Idara ya Haki, ambayo ilichunguza madai hayo kwa muda wa miezi minane chini ya Trump, ilipuuzilia mbali madai hayo kuwa hayana uthibitisho.

Mykola Zlockewski baadaye alikanusha madai hayo. Alisema hakuwahi kuwa na mawasiliano na Joe Biden au wafanyakazi wake. Joe Biden hakumsaidia yeye wala kampuni yake alipokuwa rais wa kampuni hiyo. Aliyasema haya yote katika mahojiano yaliyotolewa na mwakilishi wa Democrat, Jamie Ruskin.

Devon Archer pia alieleza kwamba hakuwa na ufahamu wa malipo hayo.

Uingiliaji wa mahakama

Warepublican wanasema Idara ya Haki iliingilia kimakusudi uchunguzi wa miaka mingi wa malipo ya kodi ya Hunter Biden. Warepublican walitoa ushahidi kutoka kwa wafichuzi wawili wa Huduma ya Mapato ya Ndani (IRS).

Wafichuaji hao walisema katika ushahidi mapema mwaka huu kwamba Idara ya Haki ilikuwa ikipunguza kasi ya uchunguzi na kufunga njia.

Warepublican walisema ushahidi uliotolewa na wafichuaji ndio msingi wa kusema kwamba Idara ya Haki ilichukua hatua kwa niaba ya Biden katika uchunguzi wa Donald Trump, lakini haikujali katika kesi ya Hunter.

Hata hivyo, Idara ya Haki (Justice Department) ilikataa madai haya. Mashahidi wengine walioitwa na Republican ni pamoja na Joe Biden, ambaye alitoa ushahidi kwamba Mwanasheria Mkuu, Merrick Garland hakuwahi kuingilia uchunguzi.

Uchunguzi wa Burisma

Vilevile Spika McCarthy alitaja mawasiliano kati ya wafanyikazi wa Joe Biden na timu ya Hunter Biden.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais na Hunter Biden walishirikiana katika kujibu maswali ya vyombo vya habari kuhusu ufisadi wa Burisma. Kamati ya Uangalizi ya Bunge pia ilitoa madai kama hayo.

Kamati hiyo ilinukuu barua pepe ya 2015 kutoka kwa mshirika wa biashara ya familia ya Biden, Eric Schwerin kwenda kwa Kate Bedingfield, mfanyikazi katika ofisi ya makamu wa rais.

Kamati hiyo ilisema barua pepe ilikuwa na nukuu kuhusu jukumu la Hunter Biden katika suala la Burisma kwa vyombo vya habari.

Akijibu kesi ya Burisma, msemaji wa Ikulu ya White House, Ion Sams alisema, "Hizi ni juhudi ya miezi kadhaa za Warepublican kupoteza pesa za walipa kodi kwa ushahidi usio na uthibitisho."