Kombe la Dunia 2022: Mashabiki wa Japan wasafisha uwanja baada ya kuishinda Ujerumani

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukubwa wa ushindi wao dhidi ya Ujerumani ungewafanya waondoke haraka kwa usiku mzima kusherehekea lakini mashabiki wa Japan walionyesha kuwa tabia nzuri zimekita mizizi, haijalishi hali ilivyo.
Baada ya mechi kukamilika, stendi za viwanja vya michezo kwa kawaida zimejaa mabaki ya chakula taka na vikombe vya plastiki vya vinywaji, vinavyoachwa kwa mtu mwingine kusafisha.
Lakini si wakati Samurai Blue iko mjini.
Wachezaji wao, wakiwa wamepata ushindi wa 2-1 dhidi ya mabingwa hao mara nne katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia, Wajapani waliokuwa kwenye umati wa watu walisitisha sherehe kwa muda katika Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa nchini Qatar ili kuusafisha kwanza .
Walifanya vivyo hivyo kwenye Kombe la Dunia nchini Urusi miaka minne iliyopita, haswa baada ya kufungwa 3-2 na Ubelgiji katika hatua ya 16 bora, na tena katika mechi ya ufunguzi wa mashindano ya 2022 kati ya wenyeji Qatar na Ecuador siku ya Jumapili - mechi ambayo timu yao haikushiriki
Huko Japani, usafi ni sehemu ya tamaduni na hujikita kwa watu wake tangu utotoni
Mnamo mwaka wa 2018, Scott North, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Osaka, aliiambia BBC kwamba kudumisha usafi ni njia ambayo Wajapani "huonyesha fahari katika njia yao ya maisha".
“Kusafisha baada ya mechi za mpira wa miguu ni upanuzi wa tabia za kimsingi zinazofundishwa shuleni, ambapo watoto husafisha madarasa na barabara za shule,” alisema.
Japan itacheza na Costa Rica katika mechi inayofuata ya Kundi E Jumapili, ikifuatiwa na Uhispania siku ya Alhamisi.
Lakini hata kama hawatashinda Kombe la Dunia, mashabiki wao tayari ni washindi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Getty Images












