Burkina Faso: Je, wakosoaji wa serikali huadhibiwa kwa kupelekwa mstari wa mbele wa vita?

'

Chanzo cha picha, AROUNA LOURÉ

Maelezo ya picha, DKT. AROUNA LOURÉ
    • Author, Khadidiatou Cissé
    • Nafasi, BBC

Katika kile kilichoonekana na wengi kama adhabu kwa ukosoaji wake kwa watawala wa kijeshi wa Burkina Faso, daktari Arouna Louré 38, alilazimika kwenda mstari wa mbele wa vita dhidi ya wanajihadi wanaofanya uharibifu katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Dkt Louré anasema alikuwa na wagonjwa katika chumba cha upasuaji katika hospitali moja ya mji mkuu, Ouagadougou, wakati askari waliokuwa na silaha walipoingia ghafla.

Aliwekwa ndani ya gari na askari na kusafirishwa hadi kwenye kambi ya mafunzo ya kijeshi iliyo umbali wa mamia ya maili. Ni miongoni mwa wanaume wengi ambao wamelazimishwa kujiunga na kile kinachoitwa Kujitolea kwa Ajili ya Ulinzi wa Nchi.

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi, Kapteni Ibrahim Traore ametetea mpango huo, akisema "uhuru wa mtu binafsi [si] bora kuliko uhuru wa kitaifa" na kuongeza "taifa halijengwi kwa utovu wa nidhamu na machafuko."

Kuandikishwa Dkt. Louré mwezi Septemba, kumekuja miezi mitano baada ya serikali ya kijeshi kupitisha amri ya kusajiliwa mtu yeyote aliye na umri wa zaidi ya miaka 18 kupigana dhidi ya wanajihadi.

Pia unaweza kusoma

Kuwadhibiti Wakosoaji

dsx

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanajeshi wametatizika kukabiliana na waasi wa jihadi waliosambaratika kutoka nchi jirani ya Mali

Daktari huyo anaamini alilengwa kwa sababu alikuwa mkosoaji mkubwa wa watawala wa kijeshi kwenye mitandao ya kijamii, akiwaelezea kama "waasi wa kikatiba" huku wakiondoka mstari wa mbele na badala yake wakiwapeleka raia kupigana.

"Katika nchi hii, hatuko huru tena kusema kile tunachofikiria," aliambia BBC.

Madai ya Dkt. Louré yameungwa mkono na kundi la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW), ambalo lilisema katika ripoti ya mwezi Novemba, serikali ya kijeshi inatumia "mpango huo kudhibiti wakosoaji."

Msemaji wa serikali ya kijeshi na waziri wa sheria hawakujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao.

HRW na mashirika mengine yanasema kesi ya Dkt. Louré sio pekee - kuna takribani wanaharakati kumi na wawili, waandishi wa habari na viongozi wa upinzani wameandikishwa jeshini.

Ni pamoja na mfamasia Daouda Diallo, ambaye aliunda kikundi cha haki za binadamu mnamo 2019 kurekodi unyanyasaji kutoka pande zote katika mzozo wa Burkina Faso .

Familia yake na mawakili wanaamini alitekwa nyara na maajenti wa usalama tarehe 1 Desemba alipokuwa akitoka katika ofisi ya uhamiaji huko Ouagadougou.

Siku chache baadaye, picha yake iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa nyuma ya lori la jeshi amevalia sare za kijeshi.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limefuatilia masaibu yake, likitoa wito wa "kukomeshwa mbinu ya uandikishwaji katika jeshi kama njia ya kuwanyamazisha wapinzani."

L

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Kiongozi wa mapinduzi Capt Traoré, anayeonekana akipunga mkono
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuandikishwa jeshini kumesababisha taharuki kubwa kwa familia. Mwanamke mmoja anasema mumewe - mwandishi wa habari za uchunguzi - alitoroka nchini, muda mfupi kabla ya barua ya kuitwa kuwasili.

'Bado anahofia usalama wa mumewe,' alisema. Ingawa familia nzima kwa sasa inaishi kwenye mkoani mwingine.

Dkt. Louré anasema alipewa mafunzo kidogo ya mapigano kabla ya kutumwa katika maeneo matatu - ikiwa ni pamoja na Koumbri, mojawapo ya maeneo hatari zaidi katika eneo la Kaskazini mwa nchi.

Takribani wanajeshi 17 na wanajeshi wa kujitolea 36 waliripotiwa kuuawa katika vita huko Koumbri tarehe 5 Septemba, siku mbili tu kabla ya kupokea barua rasmi ya kuitwa kutoka kwa jeshi.

Dkt. Louré aliambia BBC kwa bahati hakuhusika katika mapigano yoyote wakati wa kutumwa kwake kwa siku 94. Badala yake, aliwatibu askari walioonyesha dalili za magonjwa kama vile malaria.

"Uwepo wangu ungekuwa na manufaa zaidi hospitalini kuliko mstari wa mbele wa vita," anasema.

Jumuiya moja ya kiraia ilipinga mahakamani kuandikishwa katika jeshi baadhi ya wanachama wake - baada ya kupokea barua za wito muda mfupi baada ya kutangaza mipango ya kufanya maandamano dhidi ya kuminywa uhuru wa kujieleza.

Mmoja wa mawakili wao, Guy Hervé Kam, anasema mahakama iliamua, kuandikishwa kwao jeshini ni kinyume cha sheria.

"Tuliweza kuonyesha kuandikishwa huku hakukuwa lazima na kulitumika kama adhabu," Kam anasema.

Lengo ni kudhalilisha

GFVB

Dkt. Louré, amerejea nyumbani na familia yake, anasema haoni njia ya kutoka kwa mtu yeyote ambaye atapokea wito.

“Lengo ni kudhalilisha, ukitii wanakupiga picha na kuiweka kwenye mitandao ya kijamii ili kukudhalilisha, ukikimbia nchi wanakuita mwoga, na ukishtaki serikali watu pia husema wewe ni mwoga.”

Licha ya kupitia hayo, Dkt. Louré bado yuko kwenye mitandao ya kijamii na ana matumaini mema kuhusu mustakabali wa Burkina Faso.

"Mgogoro huu ni fursa kuelewa gharama ya kutoelewana kwetu na nina hakika tutarudi tena kwenye hali ya kawaida kama nchi," anasema.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah