Burkina Faso inawazuilia maafisa huku uchunguzi wa jaribio la mapinduzi ukiendelea

Chanzo cha picha, Reuters
Burkina Faso inawazuilia maafisa huku uchunguzi wa jaribio la mapinduzi ukiendelea
Mamlaka ya nchi hiyo inasema maafisa wanne wa jeshi wamezuiliwa kwa mahojiano siku moja baada ya serikali ya kijeshi kutangaza kuzuia jaribio la mapinduzi.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi pia ilisema maafisa wawili wametoroka.
Idara ya usalama na ujasusi ya Burkina Faso ilizuia jaribio la mapinduzi Jumanne, kulingana na serikali ya kijeshi ya nchi hiyo.
Serikali hiyo ilidai kuwa maafisa wa kijeshi na wengine walikuwa wamepanga kuyumbisha nchi na kuiingiza katika machafuko.
Ni chini ya mwaka mmoja tu tangu Rais wa mpito Kapteni Ibrahim Traoré achukue mamlaka.
Hayo yalikuwa mapinduzi ya pili ya nchi hiyo mwaka 2022 huku ikikabiliana na waasi wa Kiislamu.
Katika taarifa iliyosomwa kwenye runinga, mamlaka ilisema baadhi ya watu walikamatwa, bila kutoa maelezo maalum.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kumekuwa na dalili za mvutano ndani ya jeshi.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi anasema uchunguzi umeanza na ametoa wito kwa walioshuhudia kile alichokiita majaribio ya kuyumbisha nchi, kujitokeza na kusema kilichotokea.
Hata kabla ya tangazo kwamba njama ya mapinduzi ilikuwa imezimwa, kulikuwa na dalili kuwa mambo hayakuwa sawa ndani ya jeshi.
Wiki tatu zilizopita kulikuwa na tukio jingine dhidi ya utawala wa kijeshi.
Siku ya Jumanne, uvumi wa kutokea uasi ulisababisha mamia ya watu kumiminika katika mitaa ya mji mkuu, Ouagadougou, kuunga mkono serikali ya kijeshi.
Siku hiyohiyo, mamlaka ilisimamisha jarida la habari la lugha ya Kifaransa Jeune Afrique, ikilishutumu kwa kuchapisha makala yanayokashifu vikosi vya jeshi.
Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni Jumatano jioni, mamlaka ilisema baadhi ya watu wamekamatwa na walikuwa wakiwasaka washukiwa wengine, bila kutoa maelezo maalum.
Ilisema wahalifu hao "walikuwa na nia mbaya ya kushambulia taasisi za jamhuri na kuiingiza nchi katika machafuko".
Saa chache mapema, Kapteni Traoré alikuwa ametoa taarifa akisema "amedhamiria kuongoza kwa usalama kipindi cha mpito [kwenda kwa demokrasia] licha ya shida na hila mbalimbali za kukomesha maandamano yetu yasiyoweza kuepukika kuelekea kujitawala".
Junta imesema uchaguzi utafanyika Julai mwaka ujao.
Siku ya Jumanne, uvumi wa kutokea uasi ulisababisha mamia ya watu kumiminika katika mitaa ya mji mkuu, Ouagadougou, kuunga mkono serikali ya kijeshi.
Nchini Burkina Faso, wanajeshi wa Mali na Niger walitumia hali mbaya ya usalama kama sababu ya kunyakua mamlaka.
Maelfu ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa Ufaransa wanaondoka katika eneo hilo baada ya kuamriwa kutoka nje.
Kuna hatari kwamba wanamgambo wa Kiislamu watachukua fursa ya mabadiliko haya yote na ukosefu wa usalama katika katika eneo la Sahel utakuwa mbaya zaidi.













