Je, kuna hatari gani ya mwanaume kuzaa uzeeni?

Chanzo cha picha, Getty Images
Muigizaji Al Pacino alimkaribisha mtoto wake wa nne akiwa na umri wa miaka 83 mwaka jana na mpenzi wake, Noor Alfallah mwenye umri wa miaka 29. Amejiunga na klabu ya baba wenye umri mkubwa na nyota mwenzake Robert De Niro, ambaye mwezi uliopita alithibitisha amezaa mtoto wake wa saba akiwa na umri wa miaka 79.
Wawili hao kwa hakika si wanaume wa kwanza kuzaa uzeeni; waigizaji wengine kadhaa wa kiume, wanamuziki, na hata marais wa Marekani wamepata watoto uzeeni katika maisha yao.
Umri wa wastani wa wanaume kuanza kuwa baba umekuwa ukipanda. Umri huo umepanda kwa miaka 3.5 kati ya 1972 hadi 2015 nchini Marekani, ambapo baba kwa wastani ana umri wa miaka 30.9, na 9% ya baba hao walikuwa na umri wa miaka 40 wakati mtoto wao wa kwanza anazaliwa, kulingana na utafiti wa 2015 uliochapishwa katika jarida la uzazi wa binaadamu.
Baba mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutokea, kulingana na Guinness World Records, alikuwa na umri wa miaka 92 - ingawa kuwa madai yasiyo rasmi kuhusu wanaume wazee wanaozaa ambayo huibuka mara kwa mara.
Hatari za kuzaa uzeeni

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi Desemba 2022, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Utah, Marekani na taasisi nyingine walichapisha mapitio ya kina ya "umri wa kina baba" na athari zake kwa uzazi, matatizo katika ujauzito na afya ya mtoto.
Ingawa tafiti nyingi haziangalii umri wa wanaume kama akina Pacino, ushahidi unaonyesha mbegu za mwanaume wa umri wa miaka arobaini na hamsini hupungua ubora katika muktadha wa ujazo, idadi, uwezo wa kusafiri na kubadilika.
Mabadiliko haya yanamaanisha umri mkubwa wa uzazi "unahusishwa na hatari sio tu kuwa na utasa lakini pia kuharibika kwa mimba baada ya kutia mimba kwa njia ya asili," wanasema watafiti. Tafiti nyingi, zinasema, mwanaume mwenye umri mkubwa huongeza hatari ya mimba kuharibika.
Kisha kuna hatari ya ugonjwa baada ya kuzaliwa. Inaeleweka kuwa tangu miaka ya 1950, wanaume wanaozaa wakiwa na umri mkubwa – kuna uwezekano mkubwa wa kupata watoto wenye tatizo la kutokukuwa vizuri (umbilikimo). Lakini tangu wakati huo, hali zingine tofauti zimeibuka.
"Imezidi kudhihirika kuwa umri mkubwa katika uzazi, unahusishwa na matatizo ya kiafya kwa mtoto," wanasema watafiti wa Utah.
Matatizo kwa mtoto

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Stanford, waligundua kuwa wanaume wenye umri mkubwa wanaweza kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo na kifafa. Kuzaa ukiwa na umri mkubwa pia kunahusishwa na uwezekano wa mtoto kuzaliwa na kansa ya utotoni, pamoja na matatizo ya moyo ya kuzaliwa.
Inafaa kuelewa, tafiti nyingi huchunguza uhusiano kati ya afya na tatizo. Lakini pia kunaweza kuwa na mambo mengine yanayochangia, kama vile mtindo wa maisha wa wazazi na uchafuzi wa mazingira.
Watafiti wamegundua kadiri wanaume wanavyozeeka, wanaweza kupata mabadiliko na uharibifu wa DNA katika chembe zinazounda mbegu na zinaweza kupitishwa kwenda kwa mtoto.
Kihistoria, kumekuwa na tabia ya kumtazama mwanamke na umri wake wakati wanandoa wanapokuwa na matatizo ya kushika mimba. Na tafiti nyingi zinatazama zaidi uzazi wa mwanamke. Sasa inadhihirika kuwa, ingawa uzazi wa mwanaume hupungua polepole zaidi kuliko ule wa mwanamke, ila bado umri wa baba nao ni muhimu.
Kesi za Pacino na De Niro - na wanaume wengine katika miaka ya sabini, themanini na tisini - zimesalia kuwa chache. Lakini ubaba si kazi ya vijana peke yao kwa sasa.
Tangu miaka ya 1970, idadi ya wanaume wa Marekani wanaozaa wakiwa na umri wa chini ya miaka 30 imepungua kwa 27%, huku idadi ya wanaume wanaozaa wakiwa na umri wa miaka 45-49 imeongezeka hadi 52%.
Ikiwa hali ya sasa itaendelea hivi – basi dawa na mitazamo ya kijamii - bila shaka italazimika kuunga mkono.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












