Nini kinafuata baada ya Rais Mteule William Ruto kuidhinishwa na mahakama?

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Mteule William Ruto anatarajiwa kuapishwa siku ya Jumanne, Septemba 13, 2022.
Hii ni baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9 na mpinzani wake mkuu ambaye pia ni kiongozi wa Muungano wa Azimio, Raila Odinga.
Kawaida, kutakuwa na shughuli nyingi zitakazo shuhudiwa wiki moja kabla ya sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Rais mteule William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua.
Kikatiba, sherehe hiyo inafanyika siku ya saba tangu tarehe ambayo Mahakama ya Juu Zaidi imetoa uamuzi wake kutokana na kesi yoyote ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyowasilishwa.
Rais Mteule hushika madaraka kwa kula kiapo au uthibitisho wa uaminifu, wa utekelezaji majukumu ya ofisi.
Sherehe za kukabidhi mamlaka huandaliwa na kamati maalum ya kula kiapo cha rais inayoongozwa na mkuu wa utumishi wa umma Joseph Joseph Kinyua.
Rais mteule atatwaa hatamu za uongozi kwa kula kiapo cha kukubali majukumu yaliyotwikwa katika ofisi ya urais kwa mujibu wa sheria.
Wakati wa sherehe hiyo, Rais mteule anapaswa kuapishwa hadharani na Jaji Mkuu au Naibu Jaji Mkuu iwapo Jaji Mkuu hatakuwepo.
Baada ya kula kiapo, Rais atatia saini cheti cha kuapishwa kwake huku rais anayeondoka akimkabidhi vifaa vya mamlaka na uongozi: upanga na katiba.
Rais atashika madaraka yake kwa muhula unaoanzia tarehe ambayo aliapishwa, na kuishia wakati mtu anayefuata aliyechaguliwa kuwa rais anapoapishwa.
Kilichoangaziwa na Mahakama ya Juu wakati wa uamuzi wake

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati Mahakama ya Juu Zaidi inatoa uamuzi wake wa pamoja, majaji hao wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome walisema kwamba ushahidi uliotolewa na mlalamishi Raila Odinga ulikuwa umejaa uvumi na porojo.
Akiangazia maswala tisa ya kesi hiyo, Jaji Martha Koome alisema kuwa mshindi wa uchaguzi huo William Ruto alifanikiwa kupata kiwango cha asilimia 50 na kura moja zaidi kama inavyohitajika kikatiba.
Katika suala la teknolojia, Jaji mkuu Martha Koome alisema majaji hawakushawishiwa na madai kwamba teknolojiailiyotumika ilifeli katika majaribio ya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi.
Suala la pili lililoibuliwa na walalamishi ni iwapo kulikuwa na kuingiliwa kwa matokeo kama yalivyopakiwa kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi. Na Mahakama ya Juu Zaidi ilijibu kwamba hakukuwa na ushahidi kwamba mfumo wa matokeo uliingiliwa.
Jaji mkuu pia alisema hakukuwa na ushahidi kwamba fomu za uchaguzi katika tovuti ya matokeo ya mtandaoni zilibadilishwa kutoka fomu za awali zilizochapishwa.
Katika kesi moja, jaji alisema kwamba ushahidi umeonekana kuwa "hewa' /yaani uwongo.
Walalamishi katika kesi yao, walikuwa wameonyesha kutoridhika na hatua ya Tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi katika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali kuwa hatua hiyo ilikuwa jaribio la kuwazuia wapiga kura kujitokeza kwa wingi na kulenga kuwa na athari hasi kwa maeneo yaliyoonekana kuwa ngome za Raila Odinga.
Aidha, Mahakama hiyo ilitupilia mbali madai ya kujazwa kwa karatasi za kura katika masandukuna kuongeza kwamba hakukuwa na hati hata moja ambayo ilitolewa na timu ya Raila Odinga kuthibitisha kulikuwa na ujazo wa kura, kumpendelea rais mteule William Ruto.
Kuhusu suala la mzozo juu ya nani alikuwa na uwezo wa kusoma matokeo, majaji walisema kuwa mamlaka ya kuthibitisha na kujumlisha matokeo ya uchaguzi wa urais hayatokani na mwenyekiti bali tume.
Lakini majaji hao walizingatia ukweli kwamba makamishna wanne waliopinga matokeo ya mwisho walishiriki katika uhakiki wa awali na kujumlisha matokeo.
Na kwenye suala la madai ya kwamba hakukuwa na mgombea aliyefikisha kiwango cha asilimia 50 na kura moja zaidi kama inavyohitajika kisheria, Mahakama ya Juu iliona kwamba walalamishi hawakutoa ushahidi wa kutosha kubatilisha matokeo kwa msingi.
Baada ya muda wa kuhudumu kwa Rais kuanza rasmi, hataweza kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili kulingana na katika ya Kenya.















