Kasongo, Zakayo, El Chapo na Naibu Yesu - kwa nini rais wa Kenya ana majina mengi ya utani?

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Kenya William Ruto ni mtu mwenye majina mengi ya utani.
Naibu Yesu, El Chapo, Hustler na Muuza Kuku ni baadhi tu ambayo amepata katika miaka ya hivi majuzi.
Kama ilivyo ada wakati watu wanapewa majina mbadala, mengine ni kuonyesha mapenzi lakini mengine yanakusudia kumdhihaki na kuonyesha hasira kali dhidi yake.
Historia ya majina hayo ya rais yanaonyesha jinsi mtazamo wake ulivyobadilika.
Ruto amekiri kwamba mtindo wa kumbatiza upya, akitania hivi majuzi kwamba Wakenya "wanammaliza" na majina mengi ya utani.
"Mumenipa majina mengi sana. Nilikuwa na jina William Kipchirchir Samoei Ruto. Mumeongeza Survivor… Zakayo... sasa muko na Kasongo (jina la wimbo wa Kikongo kuhusu kuachwa na kuhuzunisha). Je, mutamaliza yakifika kumi, au nijiandae kwa zaidi?" aliuliza hivi karibuni.
Umati wa watu, katika mkutano katika mji mkuu, Nairobi, ulijibu kwamba walikuwa na zaidi.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais mwaka wa 2022, Ruto alivutia majina yaliyoimarisha sifa yake kama mtu wa watu.
Hustler - usemi wa Kikenya wa mtu anayetafuta riziki dhidi ya hali ngumu - ulisaidia kumuonyesha kama mtu ambaye angetanguliza mahitaji ya watu wanaotatizika.
Muuza Kuku, akirejelea maisha yake ya utotoni alipokuwa akifuga kuku kando ya barabara, uliwagusa watu wengi walioona maisha yake kuwa mfano wao wenyewe.
"Haya yalikuwa majina mazuri sana. Walimuuza kwa umma kulingana na kura," mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Herman Manyora aliambia BBC akiteta kuwa walimsaidia kuingia kwenye wadhifa huo wa juu.
" Ruto ana majina mengi ya utani," aliongeza.

Chanzo cha picha, AFP / Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini rais amekuwa mtu mashuhuri katika siasa za Kenya kwa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kuhudumu kama naibu wa rais kwa miaka tisa hadi 2022, na hajawahi kukosa kuhusika na mabishano.
Prof Manyora anakumbuka jina la Arap Mashamba - linalotafsiriwa "mwana wa mashamba" – alilopewa chini ya miaka kumi iliyopita na linahusiana na umiliki wa Ruto wa ardhi kubwa kote nchini. Kumekuwa na wasiwasi kuhusu jinsi baadhi ya ardhi hizi zilivyopatikana.
Mwaka 2013, mahakama ilimuamuru Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 (hekta 40) na kufidia mkulima ambaye alikuwa amemshtaki kwa kulinyakua wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Alikana kosa lolote.
Tabia ya Ruto ya kunukuu mistari ya Biblia pia ilimfanya atambulishwe kama naibu Yesu.
Lakini ni tangu kupanda kwake katika wadhfa wa urais ndipo watengenezaji majina ya utani wamekuwa wakifanya kazi kwa muda wa ziada - huku majina mapya yakiundwa - na kuzidi kumkosoa kiongozi huyo.
Jina moja lililojitokeza ni lile la Zakayo - Kiswahili likimaanisha, mtu wa Biblia ambaye anajulikana kama mtoza ushuru mwenye pupa aliyepanda juu ya mti ili kumwona Yesu.
Serikali ya Ruto ilianzisha ushuru mwingi ambao haukupendwa na Wakenya na Wakenya wengi wakaanza kusema kwamba alikuwa amewasaliti "mahustler".
"Alishindwa kutimiza majukumu yake baada ya kuwa rais," Prof Manyora alisema.
Maumivu ya kulipa kodi zaidi, na mtazamo kwamba pesa za ziada zitapotea, mara nyingi yalitawala mazungumzo mengi.
Mwaka jana, vijana walijitokeza katika mitaa ya Nairobi kwa wiki za maandamano, ambayo yaligeuka kuwa mauti, kupinga pendekezo jipya la serikali la kuongeza ushuru ambalo lilitupiliwa mbali baadaye.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wimbo wa "Ruto lazima aondoke madarakani " uligeuka kuwa wito kwa waandamanaji na sasa Must Go limekuwa jina jipya la kiongozi huyo.
Wabunifu hao pia wamezingatia madai kwamba rais anafurahia kusafiri nje ya nchi.
Kwa hivyo jina la Vasco da Ganya - mchezo wa kuigiza unaohusu jina la mvumbuzi wa Kireno wa Karne ya 15, Vasco da Gama, na neno la Kiswahili danganya, ambalo linamaanisha "kudanganya".
Uaminifu wa Ruto pia umetiliwa shaka na Kaunda Uongoman, anayemwiga marehemu mwanamuziki wa Kongo Kanda Bongoman.
Sehemu ya kwanza inahusu mapenzi ya rais kwa suti ya Kaunda - koti la safari pamoja na suruali inayolingana - na Uongoman, ambayo inajumuisha neno la Kiswahili la uongo, linalomaanisha "uongo".
Lakini rais anaonekana kutoweza kukabiliana na hali hii ya mashambulizi ya maneno.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema majina mengi "hayaongezi wasiwasi" katika ofisi ya rais lakini "hunasa jinsi watu wanavyomtazama mtu".
Ruto "amejitolea sana na anafanya kila awezalo kubadilisha uchumi... Ni kawaida kwa kiongozi yeyote kuwa na lakabu nyingi kwani hii inaashiria sifa na mipango yake kama kiongozi", aliambia BBC.
Mwaura pia alisema licha ya jina la utani la Zakayo, serikali imelazimika kuongeza ushuru ili kulipia miradi mipya, kupunguza nakisi ya bajeti na kurekebisha uchumi.
Hata hivyo, wakati watu wamevuka mipaka zaidi ya kubuni majina mapya na kutumia kejeli na aina za sanaa kumkejeli rais, kumekuwa na hisia hasi kutoka kwa viongozi.
Baadhi ya katuni na picha zinazozalishwa na AI, ikiwa ni pamoja na kumuonyesha rais kwenye jeneza, zimetajwa kuwa za "uzembe" na "zinazochukiza".
Baadhi ya wanaodaiwa kuwa watayarishaji wa maudhui haya mtandaoni wamekuwa waathiriwa wa utekaji nyara. Hii, Prof Manyora alisema, inafaa kuonekana kama ishara ya serikali kushindwa kuvumilia raia wake.
Lachon Kiplimo, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 23, anasema kwamba ingawa anamuunga mkono rais, baadhi ya ahadi alizotoa wakati mwingine "hazina uhalisia", jambo ambalo linachochea majina ya utani.
Alitoa mfano wa matumizi ya El Chapo, akimaanisha mfanyabiashara huyo wa zamani wa dawa za kulevya wa Mexico, baada ya Ruto kuahidi mashine itakayozalisha chapati milioni moja (pia inajulikana kama chapo nchini Kenya) kila siku kwa ajili ya kulisha watoto wa shule katika mji mkuu.

Chanzo cha picha, AFP / Getty Images
Bw Kiplimo hata hivyo anafikiri kwamba jinsi rais anavyowapuuza wabunifu hao, huku akionekana kuwakumbatia, inaonyesha jinsi alivyo na nguvu.
Prof Manyora anaamini kwamba vijana wanaokuja na majina mbadala ya rais hufanya hivyo kama aina ya ukakasi, njia ya kutoa kero lao.
Mtazamo huu unaungwa mkono na mwanafunzi Margaret Wairimu Kahura mwenye umri wa miaka 24, ambaye alisema kuwa Wakenya wengi "wana uchungu mwingi".
Anahisi kuwa mzaha huo ni njia ya kumfahamisha Ruto jinsi vijana wanavyohisi.
Anasema kwamba hakuna rais mwingine wa Kenya ambaye amekabiliwa na kiwango hiki cha ukosoaji, na "kwa hivyo hii ni ya kipekee [lakini] kwa njia mbaya".
Ni kweli kwamba wakuu wa nchi waliopita walikabiliwa na majina ya utani lakini hawajawa wengi sana.
Rais wa mwisho, Uhuru Kenyatta, aliitwa Kamwana ("kijana mdogo"), Jayden (Mtoto wa Kenya aliyebembelezwa au mvivu) na Wamashati (kwa kupenda mashati).
Mtangulizi wake, Mwai Kibaki, alijulikana kama Jenerali Kiguoya (jenerali ambaye anaogopa) na asiye na msimamo.
Pengine umri wa mitandao ya kijamii, pamoja na hamu yake isiyoisha ya maudhui mapya ya kuwafanya watu waburudike imeongeza mwelekeo wa kuitana majina.
Lakini kwa wengi, kama vile Bi Kahura, ongezeko la majina ya utani ya Ruto ni dhihirisho la kweli la "matatizo tofauti ambayo linawakabili Wakenya".
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












