'Wachezaji wa Man Utd ni mzigo na wanalipwa pesa nyingi'

Muda wa kusoma: Dakika 4

Baadhi ya wachezaji wa Manchester United "sio wazuri" na "wanalipwa pesa nyingi", mmiliki mwenza wa klabu hiyo Sir Jim Ratcliffe amesema.

Kiungo wa kati Casemiro, mshambuliaji Rasmus Hojlund, mlinda mlango Andre Onana, na mawinga wawili Antony na Jadon Sancho - ambao wako kwa mkopo katika vilabu vingine - walitajwa na bilionea huyo katika mahojiano na BBC Sport kama wachezaji mzigo ambao utawala wake "ilirithi".

Ratcliffe, shabiki wa muda mrefu wa Manchester United, ni mwenyekiti wa kampuni ya petrochemicals Ineos, ambayo ina uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo.

Ratcliffe mwenye umri wa miaka 72 mwaka jana alitumia £1.3bn kwa 28.94% ya hisa katika klabu hiyo kwenye mkataba ambao ulishuhudia Ineos kuchukua udhibiti wa uendeshaji shughuli za soka.

Katika mahojiano marefu, Ratcliffe alizungumzia matatizo ya hivi majuzi ya timu hiyo uwanjani - ambayo iko katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi kuu England- na akarudia ahadi yake ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ifikapo mwaka 2028.

Akizungumza siku moja tu baada ya mashabiki kupinga umiliki wake United, pia alizungumzia ugumu wa kifedha wa klabu hiyo, akisema inatazamiwa timu hyo kukosa pesa ifikapo mwisho wa mwaka.

Haya ni mambo kadhaa aliyoyazungumza Ratcliffe:

  • Kuondoka kwa Marcus Rashford kutoka kwa klabu hiyo kwa mkopo kwenda Aston Villa
  • Kumuunga mkono na kisha kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Erik ten Hag – na kuajiriwa kwa Dan Ashworth, ambaye aliondoka baada ya miezi mitano – akikiri yalikuwa "makosa"
  • Anakubali kuwa mchezo wa klabu hiyo "hauridhishi"
  • Anaamini kocha Ruben Amorim atakuwa kwenye klabu hiyo kwa "muda mrefu"
  • Jinsi anavyopanga kufanya Manchester United kuwa "klabu yenye faida zaidi ulimwenguni"
  • Inapanga kutengeneza uwanja mpya wa hadhi ya kimataifa
  • Mwaka wake wa kwanza wenye changamoto katika klabu hiyo
  • Huruma yake na mashabiki kwa baadhi ya mabadiliko ambayo alihisi yanahitajika kufanywa

Wachezaji wengine'sio wazuri na wanalipwa pesa nyingi zaidi'

Ratcliffe alilalamikia ukweli kwamba klabu hiyo bado ilikuwa inalipa madeni ya wachezaji waliosainiwa kabla ya kuinunua, akionyesha kile alichosema ni malipo ya pauni 17m ambayo bado yanapaswa kulipwa mchezaji Sancho katika msimu huu wa joto.

Mchezaji huyo wa England alisajiliwa kwa dau la pauni 73m kutoka Borussia Dortmund mnamo 2021 lakini alirudi kwenye klabu yake ya Ujerumani kwa mkopo baada ya kukosana na kocha wa wakati huo Ten Hag na alienda kwa mkopo Chelsea mwanzoni mwa msimu wa sasa.

"Ukiangalia wachezaji tunaowanunua msimu huu wa joto, tulimnunua Antony, Casemiro, Onana, tukamnunua Hojlund na Sancho. Hii yote ni mikataba ya zamani tupende tusipende ni mambo ambayo tumerithi na inabidi tuyatatue.

"Kwa Sancho, ambaye sasa anachezea Chelsea na tunalipa nusu ya mshahara wake, tunalipa £17m kumnunua katika majira ya joto."

Winga wa Brazil Antony ni mwingine ambaye yuko kwa mkopo katika klabu ya Real Betis ya Uhispania, baada ya kuwa na kipindi kigumu Old Trafford kufuatia uhamisho wake wa pauni milioni 81.5 kutoka Ajax.

Casemiro aliwasili 2022 kwa mkataba wa pauni milioni 70, wakati mshambuliaji wa Denmark Hojlund alisajiliwa mwaka uliofuata kwa pauni milioni 72.

Mchezaji wa kimataifa wa Cameroon Onana alijiunga na klabu hiyo majira ya joto kwa £47.2m.

Wachezaji hao wote wamekuwa wakikosolewa sana klabuni hapo.

"Inachukua muda kwa sisi kujitenga na yaliyopita na kujiweka mahali papya katika siku zijazo," Ratcliffe alisema.

Alipoulizwa kama kwa upande wake anaona wachezaji hao hawakuwa wazuri vya kutosha kuichezea Manchester United, alisema: "Wengine sio wazuri na wengine wanalipwa pesa nyingi sana, lakini kwa sisi kuunda kikosi ambacho kitapambana kikamilifu, itachukua muda.

"Tuna kipindi hiki cha mpito ambapo tunahama kutoka nyakati za zamani hadi siku zijazo.

"Kuna wachezaji wazuri kwenye kikosi kama tunavyojua, nahodha ni mchezaji mzuri. Hakika tunamhitaji Bruno, ni mwanasoka wa kupigiwa mfano."

'Amorim atakuwepo kwa muda mrefu'

Kocha mkuu wa Ureno Ruben Amorim aliteuliwa mwezi Novemba kufuatia kufukuzwa kazi kwa Ten Hag.

Mabadiliko hayo hayajasaidia sana kikosi hicho katika msimamo wa ligi - United wamepoteza michezo tisa kati ya 26 chini yake na wako na alama 36 nyuma ya vinara wa ligi na wapinzani wao Liverpool.

Hata hivyo ushindi wa nyumbani dhidi ya Real Sociedad wiki hii utawafanya kutinga robo-fainali ya Ligi ya Europa - na kukaribia kufuzu kuingia kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

"Nikiaangalia kikosi kilichopo kwa Ruben, kusema kweli, nafkiri anafanya kazi nzuri sana," Ratcliffe alisema.

"Ruben ni kocha bora na kijana. Na nadhani atakuwepo kwa muda mrefu tu.

Pia alimsifu Amorim kwa kujaribu kufanya mabadiliko kwenye kikosi – mshambuliaji wa Uingereza Rashford alipelekwa kwa mkopo Aston Villa baada ya kubainika kuwa hakuwa sehemu ya mipango ya meneja mpya.

"Yeye, kama makocha wengi walivyo, ni mwenye hisia. Ruben si mkamilifu lakini mimi ni mfuasi mkubwa wa Ruben," alisema.

"Anataka chumba cha kubadilishia nguo ambacho kimejaa watu ambao wamejitolea kabisa kushinda mechi. Hatawavumilia watu ambao hawajitumi kwa 100% . Wachezaji wanapaswa kuwa kwenye mstari sawa."

Ratcliffe aliongeza kuwa "alifurahishwa" kuona Rashford akifanya vyema Villa.

"Amehama Manchester na labda hilo ni jambo zuri kwake," Ratcliffe alisema. "Nimefurahi sana na anafanya vyema. Ni vizuri kuona akiendelea vizuri kwa kuwa ana kipaji kikubwa, lakini kwa sababu fulani hali haikuwa nzuri Manchester kwa misimu michache iliyopita. Lakini ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, Rashford."

Ratcliffe pia alisema wachezaji kama vile Rashford kuondoka kabisa msimu wa joto wanaweza kumsaidia Amorim, ambaye atakuwa na pesa za kutumia msimu wa joto - licha ya matatizo ya kifedha katika kilabu.

"Tumefanya makosa - lakini tunaweza kushinda Ligi kuu ndani ya miaka mitatu"

Hata hivyo, Ratcliffe anakubali sio kila uamuzi uliochukuliwa umekuwa sahihi.

"Sisi sio wakamilifu, na tuko safarini, na kumekuwa na makosa yaliyofanyika katika safari hii, lakini nadhani kimsingi, yote tunayofanya ni mambo sahihi kwa klabu," alisema.

Moja ya makosa hayo ilikuwa kuajiri mkurugenzi wa michezo Dan Ashworth - ambaye aliacha jukumu hilo baada ya miezi mitano tu.

Ratcliffe alisema "hawakuendana" na hilo likasababisha kuondoka kwake.

Akimuunga mkono Ten Hag msimu wa joto, baada ya kocha huyo Mholanzi kuondoka miezi michache baadaye, alikiri kuwa lilikuwa kosa lingine - iligharimu klabu hiyo pauni milioni 20 kufidia Ten Hag na timu yake na kisha kumleta Amorim.

"Ninakubali maamuzi ya Erik ten Tag na Dan Ashworth yalikuwa makosa. Nadhani kulikuwa na hali fulani zenye mapungufu. Ninakubali hilo na ninaomba msamaha.

"Ukiangalia wakati tulipofanya uamuzi kuhusu Erik, timu ya usimamizi haikuwepo kwa zaidi ya dakika tano," alieleza, akiongeza kuwa ilikuwa vigumu kuhukumu utendakazi wa Mholanzi huyo chini ya utawala uliopita.

"Ilidhihirika zaidi miezi mitatu baadaye na tulikosea, lakini tulisonga mbele. Nadhani tulirekebisha hilo na sasa tuko mahali tofauti sana leo," aliongeza.