Lionel Messi: Nguli wa soka nchini Argentina atacheza wapi msimu ujao?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kila kitu kinawezekana" kuhusiana na wapi Lionel Messi atacheza msimu ujao, anasema mtaalam wa soka wa Uhispania Guillem Balague.
Balague anasema nahodha huyo wa Argentina amepokea ofa kutoka kwa Saudi Arabia na Ligi Kuu ya Soka ya Marekani, huku kukiwa na nia ya kumrejesha Barcelona, ingawa bado hakuna ofa rasmi iliyotolewa.
Messi alikuwa amefikia "makubaliano ya kimsingi" ya kuongeza mkataba wake huko Paris St-Germain kwa mwaka mwingine, na kipaumbele chake kuendelea katika soka ya kiwango cha juu Ulaya hadi kombe la 2024 la Copa America.
Baada ya misimu miwili huko Paris, klabu hiyo inayomilikiwa na Qatar Sports Investment, ingependa kumshawishi akubali mwaka huo wa nyongeza chini ya masharti aliyonayo sasa.
Kulingana na Balague, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 bado anahitaji kushawishika kuwa klabu hiyo ya Ligue 1 inaweza kubaki na ushindani katika kilele cha soka la Ulaya, huku mkurugenzi wa soka Luis Campos akitakiwa kupunguza orodha ya mishahara ili kukidhi mahitaji ya kanuni za Financial Fair Play.
"Messi alisema angekaa kwa mwaka huo wa ziada mradi tu – bora tu ikubalike na pande zote mbili – kwamba kutakuwa na timu ya ushindani wa juu iliyojumuishwa," alisema Balague.
“Ujumbe alioupata Messi ni kwamba PSG itaweka sawa hali ya kifedha, jambo ambalo si tatizo, lakini walipaswa kupunguza orodha ya mishahara jambo ambalo linaifanya timu kukosa ushindani.
"Pia haijabainika kama meneja (Christophe Galtier) atabadilishwa na nani ataingia. Nchini Qatar, mazungumzo ni kwamba safu ya timu itatofautiana kati ya wachezaji wanne hadi watano, jambo ambalo linafanya msimu ujao kutokuwa na uhakika."
Vilabu vingi kutoka kote ulimwenguni vinaongeza juhudi zao kumshawishi mshindi huyo wa Kombe la Dunia la 2022 kusaini kwa ajili yao.
"Shinikizo kutoka kwa wamiliki wa klabu ya Qatar ni kubwa. Hawaelewi kwa nini kuna ucheleweshaji na watakuwa tayari kuweka pesa zaidi mezani. Lakini nasisitiza, hilo sio suala," alisema Balague.
PSG wanaongoza Ligue 1 kwa pointi sita lakini jaribio lao la 11 mfululizo la kushinda Ligi ya Mabingwa lilimalizika kwa kushindwa kwa jumla ya mabao 3-0 na Bayern Munich katika hatua ya 16 bora mwezi uliopita.
Je, kweli Messi anaweza kurudi Barca?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Messi, ambaye aliondoka Barcelona kwa sababu za kifedha mnamo 2021, alizomwa na sehemu ndogo ya mashabiki wa PSG kabla ya kupoteza mechi yao ya saba katika msimu huu wa 2023 nyumbani dhidi ya Lyon Jumapili.
Hilo lilifuatia habari za wiki iliyopita kwamba Barcelona walikuwa wakiwasiliana na Messi kuhusu kurejea klabuni hapo, na baada ya habari kuanza kuonekana kwenye vyombo vya habari vya Ufaransa kuhusu mustakabali wake ambao ulimweka Muargentina huyo katika hali mbaya.
Jorge Messi, baba na wakala wa Lionel, alikuwa na mkutano wa dakika 25 na rais wa Barca Joan Laporta katika hoteli ya Barcelona. Ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana tangu siku ambayo Laporta alithibitisha katika ofisi ya Messi kwamba mchezaji huyo hataendelea kuwepo klabuni hapo.
"Mada kuu ya mazungumzo ya hoteli haikuwa mustakabali wa Leo lakini vipi Barcelona wanaweza kumpa heshima," alisema Balague.
"Leo na Laporta hawajazungumza lakini ni wazi Barcelona wanaendelea kusukuma wazo kwamba wanamhitaji . Injini kuu ni meneja Xavi ambaye huzungumza mara kwa mara na Messi na humuonesha picha ya timu inayohitaji huduma yake bora.
“Xavi anamwambia Messi atatumika kama kiungo kati ya wawili waliopo mbele , karibu sana na anachofanya akiwa na Argentina. Xavi amefikiria njia tofauti za kufanya hivyo na kila Leo anaposikia hili, macho yake huchomoza.
Messi alikubali mkataba mpya na Barcelona kwa kupunguzwa mshahara miaka miwili iliyopita, lakini klabu hiyo ilibadilisha mawazo yao bila kutarajia dakika za mwisho. Sasa, kwa hali kama hiyo ya kifedha, mawazo ni kwamba kuwa na Messi kwenye timu kutaleta pesa ili kuendelea kuleta wachezaji wakubwa.
Uamuzi huo wa Laporta mnamo 2021 ulihitimisha maisha marefu ya Messi katika klabu hiyo ambayo ilishinda Ligi ya Mabingwa mara nne na mataji 10 ya La Liga - pamoja na Ballons d'Or mara sita.
Klabu hiyo imeendelea kuhangaika na fedha tangu wakati huo.
"Inawezekanaje Barcelona, ambao wako katika hali sawa na walivyokuwa wakati Messi alipoondoka, wanadhani wanaweza kumnunua Messi?" Alisema Balague. "Na kwanini wasianzishe mazungumzo?
"Hakuna aliyemtafuta Jorge au Leo kuwaambia jinsi ya kuweka yote hayo pamoja na kifurushi cha fedha. Barcelona bado wanahitaji kupunguza orodha yao ya mishahara kwa euro 200m.
"Mtazamo wangu ni kwamba ikiwa wangefanya hivyo, wangekuwa katika hali mbaya kumshawishi Messi na uwezekano wa kurejea. Kila wiki inayopita bila ofa ni milioni moja inayopotea ambayo labda watatoa.
"Ikiwa ofa pekee ambayo Messi amepata kusalia kwenye timu ya PSG, na hajashawishika kabisa kwa sababu ya hali yao ya kimchezo, Barcelona wanaweza kuja baada ya mwezi mmoja na kusema 'hatuna uwezo wa kulipa unachostahili lakini tunaweza kukupa hiki, ambacho hakitakuwa kingi'."
Uhamisho wa euro 400m kwenda Saudia?
Messi amekuwa na ofa wiki hii kusaini na klabu ya Al-Hilal katika Ligi ya Saudi Arabia, ambapo mpinzani wake Cristiano Ronaldo tayari anacheza, kwa zaidi ya euro 400m kwa msimu mmoja, kulingana na Balague.
Pia amekuwa akinyatiwa na na Inter Miami katika Ligi Kuu ya Soka ya Marekani, klabu ambayo mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona na rafiki yake Sergio Busquets anatarajiwa kujiunga nayo msimu ujao. Busquets bado hajajitolea kuhama kwa sababu ana matumaini ya kuungana tena na Messi.
"Kwenye MLS, hawawezi kamwe kulipa kile Al-Hilal na PSG wanaweza kutoa. Matumaini kwa Inter ni kwamba Messi anahisi ni wakati wa kuwacha soka ya kiwango cha juu na kuwa mahali patulivu tayari kwa Copa America," Balague alisema.
"Yeyote anayesema Messi ameamua kwa njia moja au nyingine atakuwa anadanganya. Atachukua uamuzi wakati fulani lakini kipaumbele ni kusalia kwenye mchezo wa kiwango cha juu hadi 2024 na Copa America, ambayo inaiweka PSG bado mstari wa mbele. .
"Barcelona haijatoa ofa yoyote, ofa kutoka kwa Inter iko wazi kabisa na imekuwa kwa muda, halafu ofa nyingine ya 400m-plus haiwezi kumweka Messi kwenye orodha ya klabu za kiwango cha juu na uwezekano wa kucheza tena dhidi ya Ronaldo hapo ndipo tulipo."












