Kwanini Papa huvaa viatu vyekundu? na maswali mengine ambayo unaona aibu kuuliza

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Andrew Webb
- Nafasi, BBC World Service
- Author, Additional reporting by David Willey
- Nafasi, BBC News, Rome
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Kanisa Katoliki limemchagua Robert Prevost kuwa kiongozi mpya kufuatia kifo cha Papa Francis.
Kumekuwa na mvuto wa kimataifa kuhusu asili anayotokea papa mpya.
Pia, hoja za ikiwa atafuata njia ya Papa Francis ya kuwa na mtazamo wa uvumilivu zaidi ikilinganishwa na watangulizi wake, na kukataa anasa ambazo mapapa wengi walizifurahia, akichagua maisha ya unyenyekevu zaidi.
Papa anafanya nini hasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Papa ndiye kiongozi wa kiroho wa zaidi ya Wakatoliki bilioni 1.4 duniani kote.
Wakatoliki wanamwona kama mrithi wa Mtakatifu Petro, mmoja wa viongozi wa awali wa Kanisa la Kikristo.
Katika imani ya Kikristo, Yesu Kristo ni mwana wa Mungu na Mtakatifu Petro ni mmoja wa mitume wake 12 - au wafuasi.
Wakatoliki wanaamini kuwa hii inamuunganisha Papa moja moja kwa moja na Yesu, na kumfanya kuwa chanzo kikuu cha mwongozo wa kiroho.
Papa kawaida huongoza sherehe za kidini za sherehe zote kuu za mwaka ndani ya Mtakatifu Petro, pamoja na Krismasi na Pasaka.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alitokea kwenye kibaraza baada ya kuchaguliwa ili kuwasilisha ujumbe wake wa "Urbi Et Orbi" (Kilatini kwa "mji na kwa ulimwengu"), baraka maalum za papa, ambazo hutolewa kwa kawaida katika hafla kuu za kidini na matukio mengine maalum.
Papa ana wafanyakazi wachache watawa wanaosimamia shughuli katika nyumba yake, kupika na kusafisha, na anaweza kuwa na mpishi binafsi.
Pia ana timu ya waandishi wanaomuandalia hotuba.
Moja ya majukumu ya papa ni kukutana angalau mara moja kila baada ya miaka mitano na maaskofu wake zaidi ya 5,000 kutoka duniani kote - takriban 1,000 kwa mwaka, au 20 kwa wiki.
Siku hizi, safari za nje pia zimekuwa sehemu ya majukumu ya papa.
Je, Papa huoa?
Kumekuwa na mapapa waliooa zamani - Ni wazi Mtakatifu Petro, anayechukuliwa kuwa Papa wa kwanza, alikuwa na mke - lakini chini ya utaratibu wa sasa, hakuna uwezekano mkubwa kwamba mwanamume aliyeoa kuchaguliwa.
Historia ya mapapa wa mwanzo ni chanzo cha mjadala mkubwa wa kitaaluma, na haijulikani ni wangapi walikuwa, kama Mtakatifu Petro, walioa kabla ya kuwa papa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Inadhaniwa kwamba Papa Hormisdas (514–523) alikuwa baba yake Papa Silverius, ambaye alimfuata, na Papa Adrian II (867–872) inasemekana aliwahamisha mke wake na binti yake kuishi katika Kasri la Lateran.
Wanahistoria wengi pia wanaamini kwamba Papa John XVII (1003) na Clement IV (1265–1268) walikuwa wanaume waliooa walipoteuliwa kuwa mapapa.
Kuna ushahidi mdogo unaoonyesha kuwa hakuna kati ya mapapa 266 waliotajwa na Vatican aliyeoa baada ya kuwa Papa, ingawa inadhaniwa kwamba baadhi ya mapapa walijihusisha na mahusiano ya kimapenzi yasiyo rasmi.
Je, mwanaume aliyeoa anaweza kuwa papa katika siku za usoni?
Hakuna uwezekano wa kutokea.
Kitaaluma, mwanaume yeyote Mkatoliki aliyebatizwa anaweza kuzingatiwa kwa nafasi hiyo, lakini tangu Papa Urban VI mwaka 1378 (mapapa 64 hadi sasa), wote wametoka miongoni mwa makardinali wanaomchagua papa.
Hakuna kati ya makardinali wanaoruhusiwa kupiga kura kwa sasa aliyeoa, na kawaida, mapadre wa Kanisa Katoliki wanatakiwa wawe waseja (wasiokuwa wameoa) wakati wanawekwa wakfu.
Ingawa Kanisa Katoliki linahitaji wanaume wasiooa, kuna baadhi ya tofauti – wanaume waliooa wanaruhusiwa katika Kanisa Katoliki la mashariki na pia kwa baadhi ya makuhani wa Anglikana waliobadili na kuwa Wakatoliki.
Hata hivyo, wanaume waliooa, pamoja na wale wanaotoka katika makundi haya ya kipekee, hawawezi kuwa makardinali.
Papa hulipwa mshahara?
Papa Francis anaripotiwa kutoa mshahara wake kwa mashirika ya misaada.
Mnamo 2021, msemaji wa Vatican alitaka kumaliza uvumi kwa kusema "Papa hapati na hajawahi kupokea mshahara.''
Francis pia alikataa baadhi ya malipo ya ofisi yake na akachagua kuishi katika nyumba ya wageni ya Vatican, Casa Santa Marta, badala ya vyumba vya kifahari zaidi vya papa.

Chanzo cha picha, Reuters
Mtangulizi wake, Benedicto XVI, alichukua hatua isiyo ya kawaida ya kustaafu mwaka 2013, akitaja sababu za kiafya.
Vyombo vya habari, ikiwemo gazeti la Italia La Stampa, viliripoti kwamba alikuwa akipokea pensheni.
Papa anahudumu kwa muda gani?
Idadi kubwa ya mapapa huhudumu hadi kifo chao, kama ilivyokuwa kwa Francis, ambaye alihudumu kutoka mwaka 2013 hadi 2025.
Hakuna papa mwingine aliyejiuzulu tangu Gregory XII mwaka 1415, na Benedicto XVI alikuwa wa kwanza kufanya hivyo kwa hiari tangu Celestine V mwaka 1294.
Wanahistoria wanabishana kuhusu ni mapapa wangapi wamewahi kujiuzulu.
Hawa ni baadhi ya mapapa wanaosemekana kujiuzulu:
- Pontian mwaka 235
- Silverius mwaka 537
- John XVIII mwaka 1009
- Benedict IX mwaka 1045
- Celestine V mwaka 1294
- Gregory XII mwaka 1415
Unakuwaje Papa?
Kwa mujibu wa sheria za Kanisa (canon law), ambazo ni mfumo wa sheria za kidini unaolitawala Kanisa la Kikristo, watu wafuatao wanaweza kuchaguliwa kuwa papa, kwa mujibu wa ripoti ya Catholic Online:
"Mwanaume yeyote Mkatoliki aliyebatizwa na mwenye akili timamu."
Ingawa ni zaidi ya miaka 500 tangu mtu asiye kardinali achaguliwe kuwa papa, historia inaonyesha kuwa inawezekana kwa viongozi wengine wa dini au hata waumini wa kawaida kuchaguliwa.
Iwapo mgombea aliyechaguliwa si askofu tayari, ni lazima awekewe daraja la uaskofu mara moja kabla ya kuchukua wadhifa wa upapa.
Wataalamu kadhaa pia wameripoti kuwa na tabia njema ni hitaji lisilo rasmi lakini muhimu sana.

Chanzo cha picha, Mimmo Chianura-Pool
Ni viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki wanaojulikana kama makardinali pekee – ambao lazima wawe na umri wa chini ya miaka 80 – wanaoruhusiwa kupiga kura kumchagua papa, na uchaguzi wa papa mpya huonekana kama jukumu pamoja na wajibu wa kiroho.
Mikutano ya siri ya uchaguzi wa papa (Conclave) imekuwa ikifanyika kwa karne nyingi, ikifuata sheria kali zilizowekwa ili kulinda usiri na kuzuia ushawishi wa nje.
Kwa nini papa huvaa viatu vyekundu?
Katika imani ya Kikatoliki, rangi nyekundu inawakilisha wafiadini (wale waliokufa kwa ajili ya imani) na mateso ya Kristo – yaani, mateso, kukamatwa, kushtakiwa, na kusulubiwa kwa Yesu kama inavyosimuliwa katika Agano Jipya.
Papa Benedikto XVI na mapapa wengi waliomtangulia waliendeleza desturi ya kuvaa viatu vyekundu.

Hata hivyo, kwa Papa, Francis alichagua kuvaa viatu vyeusi - ishara ambayo watazamaji waliona kama ishara ya tamaa yake ya kuepuka fahari na hali.
Jozi ya viatu vyeusi viliwekwa kwenye miguu yake wakati mwili wake ukiwa umelazwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia kumekuwa na tofauti juu ya hili.
Papa John Paul II anaripotiwa kuvaa viatu vya zambarau nyakati fulani.
Jarida la mtindo wa maisha la Marekani la Esquire linasema pia alivaa "viatu vya kahawia".
Kwa nini Kanisa Katoliki lina papa?
Ili kujibu swali hili, hebu tuchukue nukuu kutoka kwa kitabu kitakatifu cha Kikristo, Biblia.
Yesu anamwita mwanafunzi wake Simoni Petro, neno linalomaanisha pia mwamba: "Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu. ( Mathayo 16:18 )
Kama ilivyoelezwa hapo awali, Wakatoliki wanamwona Papa kama mrithi wa Mtakatifu Petro, mmoja wa wanafunzi wa Yesu.
Kwa hiyo Papa anaweza kuonekana kuwa kiongozi, na sehemu muhimu ya misingi hai ya Kanisa Katoliki.
Anaashiria msingi wa Wakatoliki na kushauri jinsi ya kukabiliana na changamoto na matatizo ya maisha - makubwa na madogo. Pia huwasaidia viongozi wengi wa chini wa kanisa kupata mwelekeo wa kuongoza jumuiya zao.
Waumini husafiri kutoka sehemu mbalimbali za dunia hadi Vatican kumsikiliza Papa akitoa misa katika uwanja wa St Peter's Square.
Ziara zake katika nchi nyingine huvutia umati mkubwa wa watu - ishara ya jinsi Papa alivyo muhimu kwa Wakatoliki duniani kote.















