UN, Jumuiya ya Madola: Shinikizo jipya la Raila dhidi ya Ruto

Na Dinah Gahamanyi

BBC Nairobi

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anautaka Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola kuingilia kati , ili kufanya ukaguzi wa kina wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka uliopita nchini humo, kufuatia madai ya mfichua siri, kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulitawaliwa na wizi wa kura.

 Bw Raila Odinga ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Muungano wa Azimio la Umoja, sasa anamtaka Rais William Ruto, Naibu wake Rigathi Gachagua na serikali nzima ya Kenya Kwanza kuondoka madarakani.

"Vijana tumesema kwanza tunataka Common Wealth and the United Nations itume inspectors hapa Kenya sio Ruto la sivyo wakenya watachukua hatua yao wenyewe," alisema Raila katika mkutano wa kisiasa uliofanyaka katika Jacaranda Grounds mjini Nairobi Jumapili.

Rais Ruto kwa upande mwingine amekuwa akipuuzilia mbali madai yaliyotolewa na mfichuzi wa siri, akisisitiza kuwa ni jitihada za Bw Odinga za kuvuruga utendaji kazi wa serikali yake ambazo anasema hazitafua dafu, na hazitamzuia kutekeleza kazi zake.

"Wajinga waliisha Kenya. Hakuna uwezekano kwamba Raila alimshinda Ruto katika Uasin Gishu, Nyeri, Tharaka nithi na Meru. Hayo bado ni madai ya kile kinachoitwa mfichua siri ," alisema Rais Ruto kuhusiana na madai ya ufichuzi ujumbe ambao pia aliusisitiza kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter:

Hali ya mtikisiko wa kisiasa za Kenya iliibuka kufuatia madai yaliyotolewa na mfichuzi wa siri kwenye mitandao ya kijamii aliyedai kuwa Raila alipata jumla ya kura 8,170,353 (sawa na 57.3%) dhidi ya Ruto ambaye anadaiwa kuwa alipata kura 5,915,973 ( sawa na 41.66 %) ya kura zilizopigwa.

Kauli hii ya Bw Odinga kuhusu mwaliko wa taasisi za kimataifa kufanya ukaguzi wa uchaguzi wa Kenya imekuwa ikiibua maswali mengi, huku wengi wakijiuliza iwapo Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola, wanaweza kujiingilia siasa za Kenya hususan baada ya Mahakama ya juu zaidi kuidhinisha ushindi wa Bw Ruto kama Rais wa tano wa Kenya.

Ikumbukwe kuwa Muungano wa Azimio na Bw Odinga waliwasilisha madai ya kupinga matokeo mahakamani na hoja zao kutupiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi nchini Kenya.

Hoja nyingine ni kwamba Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola, zilituma wajumbe wake kama waangalizi wa kimataifa waliosimamia uchaguzi mkuu wa Kenya, na kutoa ripoti ya kuridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi.

Odinga anasema anataka kujua kilichofanyika katika uchaguzi mkuu uliopita, na anadai ukweli hauwezi kupatikana hadi Tume huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) ifungue seva zilizotumiwa katika uchaguzi huo, kwa ajili ya kuchunguzwa, baada ya mfichuzi wa siri kuonyesha kuwa alishinda kwa zaidi ya kura milioni mbili.

Ili kushinikiza azma yake ya kutaka ‘’kuuondosha madarakani’’ uongozi wa Rais Ruto tayari Bw Odinga ameanzisha mikutano ya hadhara ya wafuasi wake.

“Tunataka Wakenya kusimama imara. Tutakwenda kila kona ya nchi hii; Machakos, Nakuru, Kakamega, Kisii, Kisumu, Kiambu na baadaye tutarudi tena Nairobi,” Odinga aliwaambia wafuasi wake mwishoni mwa Juma, katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi.

“Sio kwa faida za kibinafsi bali ni kwa ajili ya watu Wakenya. Wakenya lazima waweze kufanya uchaguzi, kupiga kura na idadi ya kura na masanduku zihesabiwe kama kama zilivyopigwa,” alisema.

‘’Sisi hatutaki nusu mkate, hatutaki mambo ya ‘handshake’

Kiongozi wa wa DAPK, mojawapo ya vyama vya Muungano wa Azimio la Umoja Eugene Wamalwa, ameiambia BBC kuwa hawana imani kuwa Bw Ruto anaweza kuunda tume ya uchunguzi wa mchakato wa uchaguzi:

‘’Hatuna imani na aliyewekwa kuwa rais kwasababu yale tumeonyeshwa ni kwamba Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa ameongoza katika uchaguzi huu na alipata ushindi, na yale tumepata yanatilia hofu ushindi wa yule aliyeko kwa madarakani kwa hivyo hatuwezi kumuamini yeye ndio achague jopo ambalo litamchunguza mwenyewe.’’

Bw Wamalwa ambaye ni mmoja wa vigogo wa upinzani kwa sasa nchini Kenya anasema mojawapo ya sababu zinazoufanya Muungano wa Azimio kutafuta usaidizi wa mashirika ya kigeni kuchunguza kura za Wakenya ni shida kuhusu tathmini ya mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya baada ya uamuzi wake.

‘’Wakati huu sheria zetu zinatoa muda mfupi sana kwa mahakama kuamua mambo ya uchaguzi, lakini sheria zetu hazijatoa nafasi. Muda mfupi baada ya Mahakama ya upeo kutoa uamuzi, ushahidi zaidi ukipatikana…mahakama inaweza kufanya tatmini. Mahakama inaweza sikiliza ushahidi mpya baada ya uamuzi lakini tuna shida kuhusu tathmini ya uamuzi wa mahakama ya upeo, na ndio maana tumeanza kuangalia iwapo tunaweza kupata Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola…tunataka suluhu kutoka nje, ili tuweze kuridhika wakati seva zitakapofunguliwa ukweli ujulikane ’’, aliongeza Bw Wamalwa.

‘’Sisi hatutaki nusu mkate, hatutaki mambo ya ‘Handshake’, Mheshimiwa Raila ametangaza wazi sisi tunataka haki na ukweli, kwa vile ukweli utatuweka huru kama nchi’’, Bw Wamalwa anasema.

Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola katika siasa za Kenya?

Si mara ya kwanza kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi mara baada ya kutangazwa na Tume ya IEBC, lakini kinachowashangza wengi mara hii ni uamuzi wake wa kuibua shutuma za wizi wa kura miezi zaidi ya minne baada ya Mahakama ya juu zaidi kuidhinisha rasmi matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi Rais William Ruto.

Kulingana na Katiba ya Kenya uamuzi wa Mahakama ya juu zaidi, ndio wa mwisho na Rais Ruto na Bw Raila wanalifahamu hilo.

Je Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola, ambao walikuwa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Kenya na kupongeza hatua iliyopigwa kidemokrasia nchini humo watakubali tena kuchunguza seva za IEBC?... ni jambo la kusubiri.