'Nilitoroka shule nikiwa na miaka 14 kumuona Bob Marley - na nikawa mpiga picha wake'

Chanzo cha picha, Dennis Morris
- Author, Tim Stokes
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mapema alfajiri mwaka 1973, kijana mwenye umri wa miaka 14 aitwaye Dennis Morris alifanya uamuzi ambao ungebadili maisha yake milele.
"Bob Marley alikuwa anakuja kufanya ziara yake ya kwanza nchini Uingereza, nami nikaamua kwamba nataka kumpiga picha. Nikatoroka shule na kuelekea kwenye klabu aliyokuwa anatumbuiza kwa mara ya kwanza jijini London."
"Alipokuwa akitembea kuelekea nilipokuwa, nikamwambia: 'naweza kukupiga picha?' Akanijibu: 'Ndiyo ndugu, ingia ndani.'"
Wakati wa mapumziko ya ukaguzi wa sauti, Marley alianza kuzungumza na Dennis kuhusu maisha ya kukua Uingereza, huku kijana huyo naye akimhoji kuhusu maisha yake nchini Jamaica.
"Kisha akanieleza kuhusu ziara hiyo, na kuniuliza kama ningependa kujiunga nao. Asubuhi iliyofuata, nikapakia begi langu kana kwamba naenda kucheza michezo shuleni, nikaelekea hotelini na safari ikaanza."

Chanzo cha picha, Dennis Morris
Ziara hiyo hata hivyo haikudumu sana ilisitishwa mapema baada ya baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo kudai warejee nyumbani mara walipoona theluji kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, wiki chache hizo ndizo zilizowasha moto wa taaluma ambayo ingemfikisha Morris kwenye kilele cha sanaa ya upigaji picha, na kumpa nafasi ya kuwapiga picha wasanii wakubwa wa muziki duniani.
Miongoni mwa picha zake maarufu zaidi ni ile ya Bob Marley aliyopiga ndani ya gari la bendi wakati wa ziara hiyo ya kwanza.
Picha hiyo, pamoja na kazi nyingine nyingi, zinaonyeshwa katika maonyesho maalum ya kazi zake yanayofanyika katika The Photographers' Gallery huko Soho, London.
Morris alizaliwa Jamaika mwaka 1960 na alihamia katika eneo la East End, London, akiwa na umri wa miaka mitano.
Shauku yake kwa upigaji picha ilianza akiwa na miaka tisa, alipokuwa mwana-kwaya katika kanisa lenye kasisi wa kipekee, kanisa ambalo pia lilikuwa na klabu ya upigaji picha.
"Kulikuwa na chumba cha giza (darkroom) kwenye nyumba ya kasisi. Nilipomuona mmoja wa wavulana wakubwa akichapisha picha, nilijua mara moja hii ndiyo itakuwa njia yangu maishani."

Chanzo cha picha, Dennis Morris
Baada ya kupiga picha za Marley kwa mara ya kwanza mwaka 1973, Morris alipewa tena nafasi ya kumfuatilia mwaka 1975, alipokuwa akitumbuiza katika ukumbi maarufu wa Lyceum Theatre jijini London.
"Nilipata picha kali sana kwa sababu nilikuwa nimeshaona namna anavyotumbuiza tangu ziara ya kwanza. Nilielewa harakati zake jukwaani, na nikajikuta nikichapisha picha za jalada kwenye majarida kama NME, Melody Maker na Time Out."
Aliendelea kushirikiana na Marley hadi kifo chake mwaka 1981.
"Lengo langu halikuwa kuwa mpiga picha wa muziki, bali mpiga picha wa vita, lakini maisha yalinigeuza kwa njia nzuri sana."

Chanzo cha picha, Dennis Morris

Chanzo cha picha, Pearl de Luna
Ingawa hakufikia vita ya kivita, aliipata vita yake ya picha alipoalikwa kuandamana na kundi la Sex Pistols katika kilele cha harakati za punk mwaka 1977.
"Ilikuwa ni hali ya vurugu za kila mara kutishiwa, kushambuliwa mitaani, na maonyesho yenyewe yalikuwa ya fujo. Lakini kwangu, hiyo ndiyo vita vyangu. Ilikuwa kamilifu." Anasema Morris.
Morris aliwahi pia kufanya kazi na wasanii wengine wakubwa kama vile Patti Smith, Oasis, Goldie na Radiohead - akisafiri nao duniani kote.

Chanzo cha picha, Dennis Morris

Chanzo cha picha, Dennis Morris
Lakini yeye binafsi huona kazi hii ya muziki kama njia ya kufadhili ari yake halisi- upigaji picha wa kihabari na wa kijamii ambayo pia inachukua nafasi kubwa kwenye maonyesho hayo.
Kazi zake za awali zilisababisha miradi kama Growing Up Black, iliyochunguza maisha ya watu weusi London miaka ya 1970; Southall – A Home from Home, iliyojikita kwenye jamii ya Kisikh; na This Happy Breed, ambayo ilielezea maisha ya kawaida jijini London.
"Nilikuwa naandika historia ya jamii yangu, jirani zangu, halafu nikazidi kupanua mipaka."Anaeleza.
"Nilikuwa na uwezo wa kuwafanya watu wafungue milango yao… nina kipawa cha asili — siwezi kueleza, wananiona, wananiamini."

Chanzo cha picha, Dennis Morris

Chanzo cha picha, Dennis Morris
Ni kipawa hiki ambacho Morris anaamini kimechangia mafanikio yake makubwa, iwe katika picha za maisha halisi au muziki.
"Ninapopiga picha za wanamuziki, ninajaribu kuondoa wanachokiigiza na kufichua nafsi yao halisi, kwa sababu mara nyingi wanakuwa na sura wanayojitengenezea mbele ya watu."
"Watu wengi huniambia iwe ni kuhusu Bob Marley au Sex Pistols, kwamba wanahisi wapo kwenye mazingira yale na mimi. Si tu picha ya haraka, bali inakupa hisia kuwa upo hapo, ni sehemu ya tukio."Anaendelea na simulizi yake.

Chanzo cha picha, Dennis Morris
Morris anasema amefurahishwa mno na jinsi maonyesho hayo yamepokelewa.
Maonyesho hayo yalifunguliwa kwa mara ya kwanza huko Paris katika Maison Européenne de la Photographie, kabla ya kuletwa London kwenye The Photographers' Gallery, ambapo yatafungwa tarehe 28 mwezi huu wa Septemba.
"Watu wanasema wanahisi kama wanaona maisha yao ya zamani, au maisha ya wazazi wao. Kwa mfano, kwenye picha za Growing Up Black, vijana wengi walikuwa wamesimuliwa na wazazi wao kuhusu walivyowasili England… na sasa wanasema, 'ah, kumbe kweli ndivyo ilivyokuwa'."
"Upande wa muziki… wanashuhudia nyakati za ndani kabisa za bendi au harakati fulani, ni mwangaza wa kipekee juu ya jitihada zilizohitajika kufikia walipofika."
"Ninajivunia sana yote haya", anasema Morris.
Maonyesho na Kitabu
- Dennis Morris: Music + Life linaendelea kuonyeshwa katika The Photographers' Gallery hadi 28 Septemba 2025.
- Kitabu kipya, Dennis Morris: Music + Life, kilichochapishwa na Thames & Hudson, kinapatikana sasa madukani.














