Kenya yatangaza siku 3 za maombolezo kufuatia mkasa wa moto uliowauwa watoto 18

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili News
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais wa Kenya William Ruto ametangaza muda wa siku tatu wa maombolezo ya kitaifa kufuatia mkasa wa moto uliowaka katika bweni la Hillside Endarasha katika kaunti ya Nyeri na kusababisha vifo vya watoto 18.
Katika tangazo lililotolewa na ofisi ya Ijumaa jioni, rais huyo wa Kenya kuwa siku hizo tatu zitaanza alfajiri Jumatatu, Septemba 9, hadi machweo siku ya Jumatano, Septemba 11, 2024.
Bw Ruto ameagiza kuwa katika kipindi hiki, bendera za Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki zipeperushwe nusu mlingoti kote nchini.
“Kwa masikitiko makubwa na heshima ya kumbukumbu ya maisha ya watu wasio na hatia waliopoteza maisha na wale waliojeruhiwa katika mkasa huu, mimi, William Samoei Ruto, chini ya mamlaka niliyopewa kama Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu. Vikosi vya Ulinzi vya Kenya, vinatoa agizo hili na kuelekeza kwamba, kama ushuhuda mzito wa alama isiyofutika iliyoachwa katika ufahamu wa taifa na roho za watoto kumi na saba walioaga, Kenya itaadhimisha muda wa siku tatu wa maombolezo ya kitaifa,” likasoma tangazo hilo.
“Katika kipindi hiki cha maombolezo ya kitaifa, Bendera ya Jamhuri ya Kenya na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itapeperushwa nusu mlingoti Ikulu, Balozi zote za Kenya, Majengo ya Umma, Viwanja vya Umma , Vituo vyote vya Kijeshi, Vituo, Vituo, Meli zote za Wanamaji za Jamhuri ya Kenya, na katika eneo lote la Jamhuri ya Kenya, kuanzia alfajiri ya Jumatatu, tarehe 9 Septemba 2024 hadi machweo ya Jumatano, tarehe 11 Septemba 2024.”
Rais alielezea huzuni ya pamoja ya taifa, akitoa salamu zake za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto wao kwa moto.
“Tukio hili linatulazimisha kuhakikisha uwajibikaji katika shule zote nchini na kuchukua kila hatua tuwezayo kulinda maisha ya watoto wetu wanaokwenda shule. Hakuna mtoto anayepaswa kupoteza maisha katika sehemu ambayo imekusudiwa kuwa kimbilio salama kwa elimu, ukuaji na maendeleo ya kijamii,” alisema.

Tangu Ijumaa polisi wamekuwa wakichunguza chanzo cha mkasa huo uliowauwa wanafunzi 18 katika bweni la shule ya msingi na secondari ya Junior ya Hillside Academy Endarasha iliyopo katika kaunti ya Nyeri eneo la kati mwa Kenya.
Hatika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa X , Rais wa Kenya William Ruto amesema kwamba anaomboleza vifo vya watoto hao na kuitaka polisi pamoja na idara ya zima moto kufanya uchunguzi kamili wa chanzo cha moto huo na watakaopatikana na hatia kufunguliwa mashtaka.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi Dkt. Resila Onyango, maafisa wa kitengo cha uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) wako katika shule hiyo na wameanza kukusanya vifaa na taarifa muhimu zitakazosaidia kupata ukweli kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na BBC Ijumaa asubuhi, Dkt. Resila amesema kwamba,’ Miili 16 iliungua kiasi cha kutoweza kutambuliwa, na kwamba mwanafunzi mmoja alifariki mapema asubuhi alipokuwa akipata matibabu hospitalini.
Wengine 14 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali kadhaa katika kaunti ya Nyeri.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwakilishi wa kata katika ofisi ya Kieni liason iliyoko shule sekondari ya Junior ya Hillside Academy Endarasha Samson, Mwangi Mwema ameieleza BBC kuwa moto huo ulitokea majira ya saa kumi na moja jioni, lakini shughuli ya uokozi ilikuwa ngumu : "Moto huo ulitokea majira ya saa 11 jioni na tuliitwa tuliamka, tulikuwa watu zaidi ya 2000 wakijaribu kuwaokoa, hakuna aliyejua moto ulitoka wapi lakini tulikuta bweni limeshika moto, tulijaribu kuwaokoa, tulikuta baadhi ya watoto wakiwa chini ya kitanda na tuliweza kuwaokoa, wengine walikuwa hawajachomwa moto lakini hii moja ya shule bora katika eneo hili, ni hasara kubwa, lakini tutaendelea na Mungu atatusaidia"
Vyanzo kutoka ndani ya shule vimeieleza BBC kwamba wanafunzi waliokuwa wakilala ndani ya bweni lililoungua wana umri wa kati ya miaka 8 na 13 wakisoma katika gredi ya 4 (sawa darasa la 4) na hadi 6 (sawa na darasa la 6), katika shule hiyo.
Rais William Ruto amesema: ’’Serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani inaweka mikakati ya kutosha kufanya uchunguzi na kusaidia familia za waliofariki na walio hospitalini’’.
Kwa sasa, BBC imefahamishwa kwamba taasisi za huduma za dharura kama vile Shirika la Msalaba mwekundu na taasisi nyingine za serikali kuu pamoja na ile ya kaunti ya Nyeri, vimebuni kitengo maalumu cha kuwasaidia wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi hao kuwatambua watoto wao, na kutoa taarifa muhimu kuhusu mkasa huo.
Imeandikwa na Laillah Mohammed na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












