AFCON 2025: Tanzania katika mtihani wa ndoto ya historia dhidi ya Morocco

S

Chanzo cha picha, CAF

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika dimba la Prince Moulay Abdellah, Rabat, macho ya mashabiki wa Afrika Mashariki na wengine yataelekezwa kwenye pambano la Raundi ya 16 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya wenyeji Morocco na Tanzania. Ni mechi inayokutanisha timu mbili zenye hadithi mbili tofauti kabisa: moja ikiwa na historia, ubora na matarajio ya ubingwa, nyingine ikiwa katika safari ya kihistoria na ndoto ya kuandika ukurasa mpya wa soka lake.

Morocco wanaingia wakiwa wababe wakubwa, wakibebwa na ubora wa kikosi, uzoefu wa mashindano makubwa na nguvu ya kucheza nyumbani. Lakini licha ya kupewa nafasi kubwa ya ushindi, kocha Walid Regragui amesisitiza jambo moja muhimu: unyenyekevu, na kuiheshimu Tanzania. AFCON mara nyingi imewafundisha vigogo kuwa jina peke yake halitoshi.

Kwa Tanzania, huu ni mtihani mkubwa zaidi kuwahi kuikabili Taifa Stars katika historia ya AFCON. Kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya 16 bora tayari ni mafanikio, lakini wachezaji na benchi la ufundi wanasisitiza hawapo Morocco kwa matembezi. Wanaingia bila presha, wakiwa na kiu ya kushangaza Afrika.

Katika mazingira hayo, huu si tu mchezo wa soka, bali ni pambano la kisaikolojia na kihistoria, uzoefu dhidi ya ndoto, na ubora dhidi ya ujasiri.

1. Historia inaihukumu Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mlinzi wa Morocco, Achraf Hakimi (kushto) akiwania mpira na kiungo wa Tanzania Himid Mao katika mchezo wa kundi F michuano ya AFCON 2024 uliopigwa January 17, 2024. Tanzania ilichapwa 3-0

Kwa takwimu na historia, Morocco inaingia uwanjani ikiwa juu kwa kila kipimo. Katika mechi 8 zilizopita walizokutana awali kati ya timu hizi katika mashindano yote, Morocco imeshinda 7, huku Tanzania ikishinda mara 1 tu ushindi wa kihistoria wa mabao 3-1 mwaka 2013 katika kufuzu kombe la dunia. Mbwana Samatta ambaye miaka 13 baadaye anakuja kukutana na tena alifunga mawili, Thomas Ulimwengu alifunga moja. timu hizi hazikuwahi kuwa na sare katika mechi hizo.

Katika mechi 5 za mwisho mfululizo, Morocco ameibuka mshindi bila hata kuruhusu bao. Tanzania imeshindwa kufunga katika mechi 4 za mwisho dhidi ya Atlas Lions. Kwenye AFCON 2023, Morocco waliwafunga Taifa Stars 3-0 hatua ya makundi, na kwenye CHAN 2024 waliwatoa wenyeji Tanzania kwa ushindi wa 1–0 wakaenda kutwaa ubingwa.

Morocco pia ina historia kubwa barani Afrika, imetwaa ubingwa wa AFCON mara 1 mwaka 1976, imefika fainali, nusu fainali mara kadhaa, na kwa sasa ni namba 1 Afrika na namba kwa ubora wa soka na namba 11 duniani kwa viwango vya FIFA.

Tanzania, kwa upande mwingine, ipo namba 112 duniani na 22 Afrika, na bado haijawahi kushinda mechi yoyote kwenye fainali za AFCON. Mbali na hivyo matokeo yao ujumla katika mechi walizocheza na mataifa mbalimbali katika miezi mitatu iliyopita, tofauti ni kubwa: Morocco katika mechi 7 zilizopita haijafungwa hata moja, imeshinda 6, na sare 1, wakiruhusu bao 1 pekee dhidi ya Mali walipokwenda sare ya 1-1 mwezi uliopita kwenye AFCON 2025.

Tanzania katika mechi 7 zilizopita haijashinda hata moja, imefungwa 5, sare 2 za juzi dhidi ya Uganda na Tunisia, ikiwa na mabao 6 ya kufunga na 11 ya kufungwa.

Kwa mantiki hiyo, historia na takwimu zinaihukumu Tanzania mapema kabla hata kipyenga hakijapulizwa. Lakini ndoto zao huenda zikawapendelea.

2. Haina cha kupoteza

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nidhamu sehemu ya ulinzi ni changamoto kwa Tanzania, imesababisha penati mbili katika mechi tatu zilizopita
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini soka si takwimu pekee. Tanzania inaingia kwenye mechi hii ikiwa na silaha moja kubwa: 'Hatuna cha kupoteza'. Hakuna aliyewapa nafasi Taifa Stars kufika Raundi ya 16. Sare dhidi ya Tunisia na Uganda tayari zimewapa heshima na historia mpya.

Morocco, kama wenyeji na wababe wa mashindano, wako na presha kubwa ya matarajio. Kila mtu anawangalia kama wameshafuzu tayari robo fainali, kwa kukutana na vibonde. Tanzania wenyewe wako huru kiakili. Hakuna anayewatarajia washinde, kila mtu anaipa nafasi Morocco.

Kocha Miguel Ángel Gamondi, anayefahamu vyema soka la Morocco, amesisitiza hilo wazi: "Tunakwenda kucheza mchezo mgumu zaidi katika historia ya soka la Tanzania, lakini tuko tayari kupambana. Tutapigania matokeo mazuri na kuonyesha taswira nzuri ya soka letu."

Alphonce Mabula, kiungo wa Tanzania anasema : "Kila mtu anajua, ni mechi ngumu, ni mchezo mgumu, lakini sisi pia kama wachezjai tumejiandaa".

Hii ndiyo aina ya mechi ambazo AFCON imekuwa ikizaa miujiza, timu kubwa ikishangaa kidogo, timu ndogo ikitumia nafasi moja tu lolote lina: "Sisi tumejiandaa vizuri, na mpira ni mchezo wa dakika 90, chochote kinaweza kutokea, tunahaadi kuweka hisotria".

Ubora wa Morocco dhidi ya ujasiri wa Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Morocco ina mchezaji bora wa Afrika, Achraf Hakimi aliyetwaa kombe la ligi ya mabingwa Ulaya msimu uliopita akiwa na PSG

Historia ndicho kinachotafutwa na Tanzania, heshima ndiyo inayoangaliwa na Morocco. Kufungwa na Tanzania kwao ni kujishushia heshima, kushinda dhidi ya Morocco ni kutengeneza historia mpya Tanzania.

Tofauti kubwa zaidi ipo kwenye ubora wa mtu mmoja mmoja na uzoefu wa kiwango cha juu. Morocco wana nyota wanaocheza katika klabu kubwa Ulaya: Achraf Hakimi, Brahim Diaz, Romain Saïss, Nayef Aguerd, Sofyan Amrabat ni wachezaji waliocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na hata nusu fainali ya kombe la dunia 2022.

Mchambuzi Shaffih Dauda anaeleza wazi: "Morroco ni taifa bora sana, sisi hatujafika hata nusu ya ubora wao, ni mechi ngumu sana kwa Taifa stars, lakini matokeo ya mpira wakati mwingine huwa ni ya kustaajabisha".

Dauda anasema uzoefu anasisitiza uzoefu unaweza kuwa eneo muhimu la kuamua mechi alipoulizwa na BBC maeneo gani yanaweza kuwa changamoto kwa Tanzania: "Eneo la kwanza ni uzoefu, wachezaji wa Morocco ukiwaangalia kwa mchezaji mmoja mmoja ni wachezjai wanaocheza kwenye viwango va juu sana, wana Hakim mchezaji bora wa Afrika, Amrabat mchezaji mzoefu, kwa Tanzania tunamuangalia Mbwana Samatta, ambaye uzoefu wake ndiyo tunautegemea zaidi".

Kwa Morocco, changamoto si vipaji bali akili, umakini na wameamkaje siku hii. Kocha wa Morocco, Regragui anateka Tanzania iheshimiwe. Regragui anaamini kuwa historia ya mashindano haya imeonyesha mara nyingi kuwa kujiamini kupita kiasi kunaweza kukupa matokeo ya ajabu. Mtazamo ulioungwa mkono na Nahodha Romain Saïss akitaka Morocco kuheshimu kila mpinzani, na kusisitiza kuwa katika hatua hii hakuna timu ndogo.

Hakuna timu ndogo, ila kwa Tanzania, changamoto kubwa nyingine itakuwa ni kuhimili presha ya dakika 90, kukaa imara nyuma, na kutumia kwa ufanisi nafasi chache zitakazopatikana.

Mwisho wa siku, mzani umeegemea kwa Morocco. Lakini kuna wakati mpira hauchezwi kwenye makaratasi. Tanzania wakiweza kucheza kwa nidhamu, kuzuia bao la mapema, na kuifanya mechi ibaki hai hadi dakika za mwisho, historia inaweza kubadilika. Ndoto inaweza kutimia dhidi ya ubora na uzoefu wa timu bora zaidi Afrika kwa sasa.

Lakini kama ubora wa Morocco utaongea mapema, basi safari ya kihistoria ya Taifa Stars huenda ikaishia Rabat, ikaisha kwa heshima, lakini bila tiketi ya robo fainali.