Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kombe la Dunia Qatar 2022: Fainali za mwaka huu ndizo zenye siasa nyingi zaidi kuwahi kutokea?
Taarifa katika orodha ya vichwa vya habari ambavyo Fifa na waandaji wa Kombe la Dunia la Qatar wangetarajiwa kuvikwepa. Wiki mbili tu kabla ya mechi ya ufunguzi kuanza balozi rasmi wa mashindano hayo amezua utata baada ya kuelezea mapenzi ya jinsia moja ni "kuharibikiwa akili".
Kauli ya mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Qatar, Khalid Salman kwa shirika la utangazaji la Ujerumani ZDF imeongeza orodha inayoongezeka kila uchwao ya masuala yanayozunguka Kombe la Dunia ambayo ni pamoja na haki za wafanyakazi, uhuru wa kujieleza, na vita nchini Ukraine.
Mzozo huo unaokua umepelekea baadhi ya watu kuyataja mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu ni lenye siasa nyingi zaidi katika historia.
Haki za LGBT
"Matumaini yangu ya awali yalikuwa ni kwamba, kulingana na maboresho waliyofanya kwa wafanyakazi wahamiaji, wanakuja na hatua kadhaa za kuboresha maisha ya watu wa LGBT+ (wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na waliobadili jinsia)," anasema Paul Amann, mwanzilishi wa kundi la LGBT+ la Liverpool FC Kop Outs.
Alialikwa kuzuru Qatar mnamo 2019 na mumewe kama sehemu ya ziara iliyoandaliwa na kamati ya kuandaa Kombe la Dunia. Mahusiano ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Qatar, huku adhabu zikianzia faini hadi hukumu ya kifo.
Lakini mamlaka za Kombe la Dunia zimesema "kila mtu anakaribishwa" kuzuru nchi hiyo kutazama mechi hizo na kudai hakuna atakayebaguliwa.
Lakini matukio kama mahojiano ya Khalid Salman yamepunguza matumaini ya mapema ya Paul kuhusu mashindano ya mwaka huu. "Cha kusikitisha, tangu kushinikizwa kufanya mabadiliko ili kuboresha mambo, Qatar kwa kweli imeongeza maradufu juu ya ubaguzi wa LGBT+."
Ripoti za wapenzi wa jinsia moja kufungwa jela na vitendo vingine ina maana kwamba Paul hangefikiria tena kwenda Kombe la Dunia. "Si jambo la busara kufikiria kuhudhuria kwa kuwa ni wazi kwamba mamlaka ya Qatari inaendelea kuwatendea vibaya watu wa LGBT+."
Wachezaji kuandamana na kupinga
Pamoja na ukosoaji kutoka kwa wanasiasa wa kimataifa na makundi ya kutetea haki, pia upingaji umekuwa ukitoa mpaka viwanjani. Denmaki itavaa jezi "iliyofifishwa" huku nembo za nchi na chapa zingine hazionekani vizuri.
Nahodha wa timu hiyo - na wale wa mataifa mengine tisa yakiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Ubelgiji - pia watavaa vitambaa vya unahodha vya OneLove zenye nembo ya upinde wa mvua.
Licha ya ombi kutoka kwa timu hizo, Fifa haijafafanua iwapo matumizi yao yatakiuka sheria za Kombe la Dunia zinazokataza wachezaji kutoa kauli za kisiasa wakati wa mechi.
Dk Gregory Ioannidis, mwanasheria na mtaalam wa sheria za michezo wa kimataifa, anaamini bodi inayosimamia soka inakabiliwa na kibarua kigumu kujaribu kutafuta wapi pa kuweka mipaka.
"Wachezaji wa Norway hivi karibuni waliweka ujumbe kwenye jezi zao, swali ni: 'Je, hii ni sawa na kauli ya kisiasa?' "Sijui, unaweza kunifafanulia kauli ya kisiasa ni nini? Sidhani kama kuna mtu anaweza, na hilo ndilo tatizo ambalo Fifa inakabiliana nayo kwa sasa."
Paul Amann anaamini kuwa haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni "maswala ya kimsingi ya kijamii, sio kuhusu siasa" na wachezaji hawapaswi kuadhibiwa kwa kuzungumza kuhusu wao. Lakini inaweza tu kuwa wakati mashindano yanapoanza ndipo mashabiki (na wachezaji) watagundua jinsi sheria zitatekelezwa.
Haki za wafanyakazi
Msaada kwa wafanyakazi wa ujenzi nchini Qatar ni suala lingine ambalo baadhi ya wanakampeni wangefurahi sana kwa wachezaji kulizungumzia. "Nadhani ni makosa sana kwa Fifa kusema: 'Oh ni ya kisiasa, kutakuwa na aina fulani ya vikwazo kwao'," anasema Mustafa Qadri, mwanzilishi wa Equidem, mshauri wa uchunguzi wa haki za binadamu na haki za wafanyakazi.
Wamezungumza na wafanyakazi nchini Qatar, ikiwa ni pamoja na wale ambao wamesaidia kujenga viwanja kwa ajili ya Kombe la Dunia, na wamegundua kwamba wafanyakazi wametozwa ada ili kupata kazi, walikuwa na matatizo ya kupata mishahara yao na kulazimishwa kufanya kazi katika joto la juu la kiwango cha hatari.
Baadhi ya ripoti zinasema zaidi ya wafanyakazi wahamiaji 6,000 wamefariki tangu Qatari ishinde zabuni ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2010. Hata hivyo, serikali ya Qatar ilisema jumla hiyo ilikuwa ya kupotosha, na kulikuwa na vifo 37 kati ya vibarua katika maeneo ya ujenzi wa viwanja vya Kombe la Dunia, vitatu tu kati yao "vinahusiana na kazi".
Ushindi wa utata wa Qatar
Tangu itangazwe kama mshindi wa taifa litakaloandaa mashindano ya mwaka huu, wengi wamekosoa ushindi wake na hata rais wa zamani wa fifa, Sepp Blater, emenukuliwa akisema ilikuwa makosa kuipa uwenyeji Qatar.
Dkt Gregory Ionnidis anasema moja ya sababu ambazo Fifa huenda imeipa Qatar mashindano hayo ni kujaribu kuleta mabadiliko.
"Wanataka kutengeneza mazingira ya ushirikishwaji. Na ukifungua nchi hiyo kwa ulimwengu basi unaweza kuishawishi nchi hiyo kuwa na mtazamo tofauti katika suala la uhuru wa mtu binafsi na kadhalika."
Lakini kuendelea kukosolewa juu ya haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wafanyakazi kumesababisha wengi kufikiria Fifa ilifanya uamuzi mbaya.
Kutimuliwa Urusi
Eneo moja ambalo Fifa imepata sifa zaidi kimataifa ni kwa uamuzi wake wa kuiondoa Urusi katika michuano hiyo wakati wa hatua za kufuzu.
Ingawa sio kawaida kwa nchi kusimamishwa kwa ukiukaji wa sheria za uwanjani au ukiukaji wa usimamizi ni kawaida zaidi kwa timu kuzuiwa kwa kosa lisilohusiana na soka.
Ni Ujerumani na Japan pekee baada ya Vita vya Pili vya Dunia, na Afrika Kusini wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi nchini humo, ndizo zimekabiliwa na vikwazo sawa na hivyo. "Fifa inajaribu kuzuia kauli za kisiasa kwenye mchezo, lakini Fifa lenyewe ni shirikisho la kisiasa," anasema Dk Ionnidis kuhusu uamuzi huo.
"Bila shaka Fifa inapaswa kufanya maamuzi ya kisiasa." Hatua ya kuiondoa Urusi ilikuja tu baada ya nchi nyingine kwenye kundi lake la mchujo - Poland, Jamhuri ya Czech na Uswidi - kukataa kucheza dhidi ya timu hiyo kupinga uvamizi wa Ukraine.
Fifa huenda "ilihatarisha mapinduzi kutoka nchi nyingine zinazoshiriki" ikiwa ingeshindwa kufanya hivyo, anaongeza Dk Ionnidis.
Mageuzi
Licha ya misukosuko hiyo, Amiri wa Qatar, Tamim Bin Hamad Al Thani, amejibu ukosoaji wa nchi yake kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia akisema: "Kwa miongo kadhaa sasa, Mashariki ya Kati imekuwa ikikabiliwa na ubaguzi, na nimegundua kuwa ubaguzi, kwa kiasi kikubwa unatokana na watu kutotujua vyema, na wakati mwingine, kukataa kutufahamu."
Pia amedai kwamba watu binafsi "wameanzisha mashambulizi, kwa kasi ambayo haijawahi kuonekana hapo awali, wakati tukio kubwa la michezo lilipoandaliwa na nchi nyingine katika mabara tofauti" na kwamba "anajivunia mageuzi na maendeleo" ambayo Qatar inayafanya.
Wakati kelele za kupinga na mabishano yakiendelea ndani na nje ya uwanja huku michuano hiyo ikikaribia, Kombe hili la Dunia linaelekea litaendelea kupamba vichwa vya habari kwa sababu nyingine mbali na soka.