Tunachokifahamu kuhusu kinachoendelea mashariki mwa DRC

Mapigano baina ya jeshi la Congo FARDC na waasi wa M23 yalikuwa yametulia kwa wiki kadhaa, lakini tarehe 20 Oktoba yaliibuka tena na wanamgambo wa M23 wamekuwa wakiendelea kuyateka maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini.
Chini ya wiki moja, maeneo yanayodhibitiwa na M23 yameongezeka karibu mara dufu, kulingana redio ya Umoja wa mataifa nchini humo Okapi.
Waasi wa M23 na jeshi la serikali walikabiliana katika maeneo ya Kahunga na Mabenga, ambapo M23 walisonga mbele kilomita tano kaskazini mwa eneo la Kiwanja in Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, shutuma ambazo Rwanda imekuwa ikizikanusha.
Maelfu ya watu wamekuwa wakifanya maandamano tangu Jumapili katika mji wa mashariki mwa DRC wa Goma kuipinga Rwanda.
Waandamanaji walisikika wakipaza sauti kupinga uvamizi wa Rwanda , na kuipinga Uganda ambayo baadhi wanaishutumu pia kuwaunga mkono M23.
Waandamanaji pia wanailaumu serikali yao kwa kushindwa kuurejesha mikononi mwake mji wa mpakani wa Bunagana uliotekwa na waasi wa M23 tangu mwezi Juni.
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita picha za video zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wakazi wa DRC wanaonekana wakiyatoroka maeneo yao huku wakilalamikia milio ya risasi na makombora kusikika katika maeneo yao.
Waandishi wa habari katika eneo hilo wanasema wapiganaji wa M23 wameimarisha ulinzi wao katika maeneo wanayoyadhibiti.
Takriban wakimbizi wa ndani 20,000 kutoka kutoka kambi mbali mbali eneo la Rutshuru wametoroka mapigano, na kujiunga na maelfu wengine walioomba hifadhi katika makanisa na shule.

Chanzo cha picha, FACEBOOK/VINCENT KAREGA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufuatia mapigano baina ya serikali ya DRC na wapiganaji wa M23, Jumamosi, serikali ya Kinshasa ilimtimua balozi wa Rwanda DRC Vincent Karega Jumatatu, kwa tuhuma kuwa nchi yake inawaunga wapiganaji hao wenye asili ya Kitutsi wanaozungumza Kinyarwanda.
Jumanne DRC imemtaka balozi wake mpya mjini Kigali kuahirisha uwasilishaji wa nyaraka zinazomruhusu kuiwakilisha DRC nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Jumanne na Wizara ya mambo ya nje, Waziri husika na wizara hiyo Christophe Lutundula amemtaka aliwasilishe nyaraka hizo’’hadi pale atakapopewa taarifa zaidi’’ kuhusiana na mpango huo.
Kauli za chuki dhidi ya Rwanda zinazotolewa na dhidi ya wanyarwanda zimeipelekea Rwanda kuwaonya wakazi wake kuepuka safari zisizo muhimu nchini Congo, kulingana na ripoti ya wavuti wa gazeti la Rwanda New Times.
Maafisa wa Rwanda wanasema mpaka utaendelea kusalia kuwa wazi na usalama utaimarishwa kwa ajili ya usalama wa raia wake.
Jumatatu Marekani ilielezea kwa mara nyingine tena hofu kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo na ikaunga mkono miito ya Umoja wa Mataifa ya kurejeshwa kwa hali ya amani.
Umoja wa Mataifa ulisema kuwa una wasi wasi kutokana na mapigano yanayoendelea ambayo yamewalazimisha watu wapatao 50,000 kuzikimbia nyumba zao katika kipindi cha siku 11, wakiwemo 10,000 waliokimbilia nchini Uganda.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema kuwa mapigano yalisababisha vifo, watu wengi kuyakimbia makazi yao na kujeruhiwa kwa walinda amani wanne wa Umoja wa Mataifa.
Bw Guterres amewataka wapiganaji wa M23 na makundi mengine kusitisha mapigano mara moja na kuweka chini silaha.
Uhusiano baina ya Rwanda na Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo ulivurugika tangu idadi kubwa ya Wahutu wanaoshukiwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994 walipowasili mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.















