DRC yamfurusha balozi wa Rwanda nchini humo baada ya M23 kutwaa maeneo zaidi

th

Chanzo cha picha, FACEBOOK/VINCENT KAREGA

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imempa balozi wa Rwanda Vincent Karenga saa 48 kuondoka nchini humo kulipiza kisasi kwa madai ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 katika majimbo ya mashariki mwa Kongo.

"Hii ni kwa kiasi fulani, kutokana na kuendelea kwa nchi ya (Karenga) kushambulia DRC na kuunga mkono harakati za kigaidi za M23," msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni Jumamosi jioni.

M23 ni kundi la waasi ambalo mamlaka ya Kongo inashutumu Rwanda kwa kuunga mkono lakini Rwanda inakanusha, liliteka mji wa Kiwanja mashariki mwa Kongo siku ya Jumamosi, na kuukata mji mkuu wa Kivu Kaskazini Goma kutoka nusu ya juu ya jimbo hilo.

Wakazi watatu wa Kiwanja waliambia shirika la habari la Reuters kwamba makundi ya wapiganaji waliingia mjini bila upinzani mkubwa baada ya milio ya risasi Jumamosi asubuhi.

Kikosi cha kuzuia mapigano cha Umoja wa Mataifa, ambacho kimekuwa kikisaidia vikosi vya serikali, kilisema katika taarifa kwamba walinda amani wanne walijeruhiwa katika mapigano hayo. Taarifa hiyo haikuzungumzia hatima ya mji huo.

"Mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita," ilisema. "(Ujumbe) unatoa wito kwa kundi hili la waasi kusitisha mara moja uhasama wote na kuonya kuwa liko tayari kujibu kwa nguvu iwapo kutatokea uchokozi zaidi."

Kikosi cha jeshi la Kongo kinacholinda mji huo kiliondoka siku iliyotangulia, wakaazi walisema. Jeshi limechukua hatua kutoka maeneo yenye watu wengi ili kusogeza mapigano mbali na miji na kuwalinda raia.