Kombe la Dunia Vilabu: Al-Hilal waongeza wasiwasi Man City?

x

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kulikuwa na huzuni na furaha baada ya dakika 120 za kusisimua
    • Author, Shamoon Hafez
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Saudi Arabia imetumia mabilioni ya kupesa kujaribu kujenga nguvu yake katika soka la dunia. Siku ya Jumatatu usiku huko Florida, Marekani, mashabiki waliona nguvu hizo zikilipa.

Timu ya Ligi ya Saudi, Pro League, Al-Hilal ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya timu ya Ligi Kuu ya Uingereza, Manchester City katika pambano la Kombe la Dunia la Vilabu.

Winga wa zamani wa Uingereza, Andros Townsend anasema: "Al-Hilal imeushangaza ulimwengu."

Mwezi mmoja uliopita, Kocha mkuu wa Al-Hilal, Simone Inzaghi aliondoka Inter Milan, siku tatu baada ya timu yake kuchapwa mabao 5-0 na Paris St-Germain kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Akiwa bado hajatulia katika timu yake mpya, na bila huduma za wachezaji wawili majeruhi Salem Al Dasani na Aleksandar Mitrovic, amejikuta na ushindi mkubwa wa kusherehekea.

"Usiku wa leo tulilazimika kufanya kitu kisicho cha kawaida kwa sababu tunajua jinsi Manchester City walivyo wazuri. Tulijua tunapaswa kupanda Mlima Everest bila oksijeni na tumefanya vizuri.”

Pia unaweza kusoma

Ushindi wa Al-Hilal

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Al-Hilal ilifuzu baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa ya AFC 2021

Kombe la Dunia la Vilabu lililoboreshwa bado halijavutia wengi, lakini mechi isiyosahaulika ya hatua ya 16 bora itazungumzwa katika pembe zote za dunia.

Al-Hilal walikwenda kipindi cha mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0. Ni kutokana na ushujaa wa kipa Bono, ndio mabao hayakuwa mengi kipindi cha kwanza.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini kipindi cha pili walirudisha huku Mbrazil, Marcos Leonardo akitoa kipigo kwa kufungua magoli mawili. Na magoli mengine yakifungwa na Malcom na Kalidou Koulibaly. Filimbi ya mwisho ilipopulizwa, wafanyakazi na wachezaji wa akiba walimiminika uwanjani kufurahia.

Mashabiki wenye furaha wa Al-Hilal, walipeperusha bendera za buluu za klabu hiyo na rangi ya kijani na nyeupe ya nchi.

Wakitoka kwenye Uwanja wa Camping World, mashabiki waliotoka Saudia Arabia, walicheza na kuimba "ole, ole ole ole," huku waandishi wa habari wa Saudi wakikumbatiana na kubusiana kila mmoja katika chumba cha mkutano wa wanahabari baada ya mechi.

Mmoja aliingia huku akiwa anatokwa na machozi na mikono yake ikiwa juu, akipiga kelele "Mabrook" kwa Kiarabu, ikiwa na maana "hongera," alikuwa huamini kile alichokishuhudia.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa klabu ya Asia kuishinda timu kutoka Ulaya katika mashindano rasmi ya Fifa. Timu za Ulaya zimeshinda mechi 18 kati ya 20 za huko nyuma, huku mechi mbili zikiwa sare.

Mwandishi wa habari kutoka chombo cha habari Arryadia aliyataja matokeo hayo "moja ya matokeo makubwa zaidi katika historia ya soka la Saudia" - lakini akaongeza ushindi wa kushtua wa nchi hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya Argentina kwenye Kombe la Dunia 2022 "ni mkubwa zaidi."

Soka la Saudi Arabia

Pesa nyingi zimetumika kujaribu kukuza mchezo wa soka huko Saudia - zaidi ya pauni milioni 700 zimetumika, kuleta wachezaji kwenye Ligi hiyo. Ujio wa nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo huko Al-Nassr miaka miwili na nusu iliyopita ulikuwa usajili muhimu.

Saudi Arabia pia itakuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2034 - uamuzi ambao umetetewa na rais wa Fifa Gianni Infantino huku kukiwa na ukosoaji mkubwa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International likielezea hatua hiyo ni ya "kutojali."

Infantino - muasisi wa muundo mpya wa Kombe la Dunia la Vilabu la timu 32 - ametoa hoja kwamba kuandaa Kombe la Dunia katika ufalme wa Ghuba kunaweza kuwa kichocheo cha maboresho katika jamii yao.

Saudi Arabia inakabiliwa na ukosoaji wa miaka mingi juu ya rekodi yake ya haki za binadamu na mazingira. Ombi la kuandaa Kombe la Dunia liliungwa mkono na Chama cha Soka cha England, cha mwezi Desemba baada ya kupokea hakikisho kwamba mashabiki wote watakaribishwa.

Jitihada za Saudia kuwania kuandaa Kombe la Dunia hazikupingwa, kwani Australia - ambayo ni mgombeaji pia - iliamua kutoingia kwenye kinyang'anyiro hicho, ikidokeza kuwa haikuwa na muda wa kutosha kujiandaa, baada ya kupewa muda wa chini ya mwezi mmoja na Fifa kugombea nafasi hiyo.

Fifa iliendesha mchakato wa haraka ambao wakosoaji walibishana haukuwa na uwazi. Wakisema, mchakato huo ulifungua njia kwa Wasaudi kwa uamuzi wa kuruhusu nchi kutoka Asia na Oceania tu ndio zigombee nafasi ya kuandaa kombe hilo.

Kiungo wa kati wa Serbia, Sergej Milinkovic-Savic, ambaye alijiunga na Al-Hilal kutoka Lazio mwaka 2023, aliulizwa kuhusu ukosoaji wa wachezaji kuondoka Ulaya kwenda katika ligi tajiri ya Mashariki ya Kati.

“Tuone sasa kama watatukosoa,” alisema. "Tumewaonyesha. Natumai tutaendelea kuwaonyesha."

Beki wa zamani wa Chelsea, Kalidou Koulibaly, ambaye alifunga dakika za nyongeza, aliongeza: “Tulijua itakuwa mechi ngumu, dhidi ya moja ya timu bora zaidi duniani.

"Tulitaka kuonyesha vipaji vyetu. Tuna furaha sana kwa sababu tulitaka kuonyesha Al-Hilal ina talanta ya kuwa hapa."

Wasiwasi kwa Man City

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pep Guardiola alipokea kichapo chake cha kwanza katika Kombe la Dunia la Klabu akiwa meneja

Hatua ya makundi ilikuwa nyepesi kwa City, wakishinda michezo yote mitatu, lakini walijikuta kwenye kikwazo cha kwanza kufuatia safu ya ulinzi kucheza ovyo.

Kikosi cha Pep Guardiola kilikuwa dhaifu kwenye mashambulizi ya kushtukiza na kukawa na uzembe kwenye ncha zote mbili za uwanja - kwani mbele pia walishindwa kutumia nafasi nyingi za kipindi cha kwanza.

"Ni dalili ya kutisha kwa Guardiola," mlinda mlango wa zamani wa City, Shay Given anasema. "Wangeweza kufunga mabao zaidi. Inatia wasiwasi sana nafasi walizopoteza."

Matokeo hayo pia yanatia dosari rekodi isiyo na dosari ya Guardiola kwenye Kombe la Dunia la Klabu akiwa meneja wa Barcelona, Bayern Munich na City.

Mhispania huyo alishinda mechi zake zote 11 za awali kwenye michuano hiyo, akiruhusu mabao manne pekee. Kwa Guardiola, kazi sasa ni kutatua matatizo waliyokumbana nayo huko Florida kabla ya mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu England, huko Wolves mwezi Agosti 16.

Anasema: "Ulikuwa mchezo mgumu. Tuliwaruhusu kufanya mashambulizi lakini na sisi tulifanya mengi. Inasikitisha.

"Tunarudi nyumbani na sasa ni wakati wa kupumzika na kupumzisha akili zetu kwa msimu mpya."