Makanisa yanahoji uamuzi wa Mahakama Kenya kuhusu haki ya ushirika ya LGBTQ

LGBTQ

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku kadhaa baada ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kuamua kuhusu uhuru wa kujumuika kwa jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja (LGBTQ) , gumzo kali limeibuka miongoni mwa Wakenya kuhoji uamuzi huo.

Mjadala huo aidha umezua hofu miongoni mwa waamini wa Kikristo huku uongozi wa kanisa sasa ukionya kwamba suala hilo linaenda kinyume na mafundisho ya Biblia.

Katika uamuzi wake wa Ijumaa iliyopita, Mahakama ya Juu ilisema kuwa uamuzi wa kuwanyima wanachama wa LGBTQ haki yao ya kujiandikisha kama Shirika lisilokiwa la kiserikali, licha ya uhusiano wa wapenzi wa jinsia moja kuwa haramu katika taifa, ulikuwa wa kibaguzi.

Hatua hiyo ilifuatia uamuzi uliotolewa mwaka wa 2013 na mahakama za chini kuwanyima wanachama wa LGBTQ nchini Kenya kusajili Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) kwa ajili ya kuendeleza haki zao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili, Kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) lilikosoa vikali uamuzi huo likitoa wito wa kudumishwa kwa maadili ya kidini.

Askofu msimamizi Calisto Odede alitilia shaka uamuzi wa mahakama ya juu akitafakari iwapo wahusika wengine haramu pia wapewe uhuru wao wa kujumuika.

"Uamuzi huu unaokinzana umewaacha wengi wetu kujiuliza kama wanyanyasaji wengine haramu kama watoto wanaofanya ngono na wanaojihusisha na kujamiiana na jamaa pia wana haki ya kujumuika na kama sivyo, wana tofauti gani na wapenzi wa jinsia moja. Na pengine mashirika ya uhalifu pia," ilisema sehemu ya taarifa hiyo

mSALABA

Chanzo cha picha, EPA

Askofu Odede alithibitisha kuwa kanisa halitasita kukemea maamuzi kama hayo, akisema kuwa kuhimiza uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja kunaenda kinyume na mila za kitamaduni za Afrika na kupinga mafundisho ya Kikristo.

Kulingana na Askofu Odede, kanisa linachukulia uhusiano wa aina hiyo kuwa dhambi kwa sababu ni kinyume cha "utaratibu wa Mungu kwa ajili ya familia na mahusiano ya kibinadamu."

Kanisa hilo sasa limetoa wito kwa Wakenya ''waadilifu'' kujitokeza na kupinga uamuzi huo wa mahakama ya juu akidai utafutilia mbali kanuni za kijamii katika taifa.

"Tunatoa wito kwa Wakristo na Wakenya wenye nia njema kujitokeza kupinga uamuzi huu na kuonyesha kutoridhika kwao waziwazi."

Bibilia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maoni sawiya na hayo yameungwa mkono na Kanisa la Redeemed Gospel nchini Kenya.

Askofu Mkuu Arthur Kitonga amenukuliwa na Shirka la Habari la Kenya KBC alkisema makundi hayo hayafai hata kuruhusiwa nchini Kenya, taifa ambalo linashikilia sana mafundisho ya Kikristo.

Akizungumza katika Kijiji cha Kaloleni, Kaunti ya Machakos, Kitonga alisema kuwa kuruhusu mambo hayo kunaweza kuleta laana nchini, kwani ni sawa na kuvunja sheria za Mungu.

Alisema hivi karibuni viongozi wa dini watakutana ili kutoa tamko la pamoja kuhusu hilo.

Kitonga aliongeza kuwa ataandaa kikao na viongozi wote wa Kanisa, ili kuja na sauti moja, akiwataka viongozi kutolifumbia macho suala hilo.

Uamuzi wa utata

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya uamuzi huo kulaaniwa vikali na baadhi ya viongozi wa kanisa mbunge mmoja amedokeza nia yake ya kuwasilisha mswada wa kuimarisha haki ya wapenzi wa jinsia moja.

Katika taarifa yake iliyoandikwa Ijumaa, Februari 24, mbunge huyo Peter Kaluma alifichua kuwa alimwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula, akimfahamisha kuhusu mipango ya kuwasilisha mswada huo bungeni wakati ufaao.

Alibainisha kuwa alikuwa katika mchakato wa kutunga sheria hiyo na alihitaji Bunge kumsaidia kupata rasilimali mbalimbali ili kuwezesha hilo.

Hata hivyo Spika wa Bunge la Kenya Moses Wetangula, amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Kenya kwamba ameungana na viongozi na taasisi zingine kukemea uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu uhuru wa kujumuika kwa wapenzi wa jinsia moja.

Mwanasheria Mkuu wa kenya Justin Muturi kwa upande wake amesema ataelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa kuruhusu usajili wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali ya LGBTQ.

Katiba ya Kenya inasema nini?

Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume na sheria Kenya na mtu anaweza kuadhibiwa kwa hadi miaka 14 gerezani.

Mnamo 2016, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu liligundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na 'wasiwasi wa usalama kila siku'.

Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na Wanyama.

Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu yamwelekeo wao wa kijinsia.

Wanaharakati wamewasilisha kesi mahakamani kutaka kubainishwa uamuzi kuhusu uhalali wa sheria inayoharamisha mapenzi kwa watu wa jinsia moja.

Katiba ya Kenya inaonya dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia.

Kumekuwepo na shinikizo kutoka mataifa mengi duniani kwa taifa la Kenya kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.

Lakini wakenya wengi, akiwemo Rais Wilian Ruto, wanahoji kuwa taifa hili lina shida kubwa zaidi za kushughulikiwa, na zinazopaswa kupewa kipa umbele.