Vita vya Ukraine: Kiongozi wa Wagner aapa kukabidhi mji wa Bakhmut kwa jeshi la Urusi ifikapo Juni

Chanzo cha picha, AFP VIA GETTY IMAGES
Kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner la Urusi ameapa kuhamisha udhibiti wa mji wa Bakhmut wa Ukraine kwa jeshi la Urusi ifikapo tarehe 1 Juni.
Mwanzilishi wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin alidai kuwa aliiteka Bakhmut siku ya Jumamosi, lakini Kyiv inasema bado inadhibiti sehemu za jiji hilo.
Ukraine inasema wanajeshi wake bado wanasonga mbele kwenye viunga vya Bakhmut.
Lakini Bw Prigozhin alisema wanajeshi wake wataanza kuukabidhi mji huo kwa jeshi la Urusi siku ya Alhamisi.
"Kundi la Wagner litaondoka Artemovsk kuanzia Mei 25 hadi Juni 1," Bw Prigozhin alisema katika rekodi ya sauti kwenye mtandao wa Telegram.
Bakhmut hapo awali ilijulikana kama Artemovsk, kwa heshima ya wa Soviet, kabla ya Ukraine kuipa jina.
Alisema kuwa Wagner alikuwa ameanzisha "safu ya ulinzi" magharibi mwa jiji kabla ya uhamisho huo.
Lakini Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Hanna Maliar, alirejelea kwamba vikosi vyake bado vina sehemu ndogo ndani ya mji huo na vinasonga mbele kwenye viunga vyake, na kuongeza kuwa "nguvu" ya harakati zao imepungua.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadaye aliandika katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram kwamba wanajeshi wa Ukraine bado wanadhibiti "vifaa fulani vya kibinafsi na sekta ya kibinafsi katika eneo la 'Litak'" la jiji.
Wachambuzi wanasema Bakhmut haina thamani ya kimkakati kwa Moscow, lakini kutekwa kwake kutakuwa ishara ya ushindi kwa Urusi baada ya vita vya muda mrefu zaidi nchini Ukraine hadi sasa.
Mamluki wa Wagner wameelekeza juhudi zao katika jiji hilo kwa miezi kadhaa na mbinu yao isiyokoma, yenye kugharimu pakubwa kwa upande wa wanaume inayoonekana kudhoofisha upinzani, Kyiv hatua kwa hatua.
Kumekuwa na madai yanayokinzana kutoka kwa pande hizo mbili kuhusu hadhi ya Bakhmut katika siku za hivi karibuni.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisisitiza Bakhmut "haijakaliwa" na Urusi, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa kilele wa G7 nchini Japan siku ya Jumapili.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alipongeza kundi la Wagner baada ya kusema kuwa limeuteka mji huo.
Bw Prigozhin - akipiga picha na baadhi ya wapiganaji wake - alidai kutekeleza hayo katika video iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii Jumamosi.

Chanzo cha picha, TELEGRAM
Bw Prigozhin ameweka hatarini sifa yake, na ya jeshi lake la kibinafsi, kwa kuteka jiji.
Katika maoni yake ya hivi punde, Bw Prigozhin alisema: "Ikiwa wizara ya ulinzi haina wafanyakazi wa kutosha, tuna maelfu ya majenerali."
Mara kwa mara amekuwa akiwalenga maafisa wakuu wa jeshi la Urusi, akiwakosoa hadharani kwa kutowaunga mkono wanajeshi wake.
Mwezi uliopita, pia alitishia kuwaondoa wanajeshi wake nje ya jiji iwapo hawatapewa silaha zinazohitajika.
Kutekwa kwa mji wa Bakhmut kutaileta Urusi karibu kidogo na lengo lake la kudhibiti eneo lote la Donetsk, moja ya mikoa minne ya mashariki na kusini mwa Ukraine iliyotwaliwa na Urusi Septemba iliyopita kufuatia kura za maoni zilizolaaniwa vikali nje ya Urusi kama udanganyifu.
Hata hivyo, wakati Urusi ilipopigana vikali kudai miji ya Severodonetsk na Lysychansk majira ya joto yaliyopita, Ukraine hivi punde ilichukua maeneo mengi kwingineko.
Mapema mwezi huu, Marekani ilisema inaamini zaidi ya wanajeshi 20,000 wa Urusi wameuawa katika vita vya Bakhmut na wengine 80,000 kujeruhiwa.
Hata hivyo, BBC haiwezi kuthibitisha takwimu hizo kwa uhuru.
Kulikuwa na takriban watu 70,000 waliokuwa wakiishi Bakhmut kabla ya uvamizi huo, lakini ni elfu chache tu waliosalia katika jiji hilo lililoharibiwa, ambalo wakati mmoja lilijulikana sana kwa migodi yake ya chumvi na jasi na kiwanda kikubwa cha divai.














