Dhahabu, gharama ya bidhaa, na nafasi za kazi: Ni masuala yapi muhimu katika uchaguzi wa Ghana?

g

Chanzo cha picha, AFP

Muda wa kusoma: Dakika 5

Ghana inatazamiwa kupata rais mpya baada ya uchaguzi wa Disemba.

Makamu wa rais wa sasa, Mahamudu Bawumia, na mkuu wa zamani wa nchi, John Mahama, ndio wagombea wawili wanaoongoza katika kinyang'anyiro cha kushinda uchaguzi huo.

Nana Akufo-Addo, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016, anakaribia mwisho wa muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka minne.

Waghana wanapigia kura nini?

Siku ya kupiga kura, chaguzi mbili zitafanyika kwa wakati mmoja:

Urais - kuna wagombea 12

Wabunge - wapiga kura katika maeneo bunge 275 kote nchini watakuwa wakichagua mbunge wao

Unaweza pia kusoma:

Nani atakuwa rais ajaye wa Ghana?

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mahamudu Bawumia (kushoto) na John Mahama (kulia) ndio wagombea wawili wanaoongoza kuchukua nafasi ya Nana Akufo-Addo kama rais.

Ijapokuwa wagombea 12 wanawania kiti cha urais, ni wawili pekee walio na nafasi halisi ya kushinda. Tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992 ni wagombea pekee kutoka National Demokratki Congress (NDC) au New Patriotic Party (NPP) ndio wameshinda.

Wagombea walio mstari wa mbele ni :

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mahamudu Bawumia (NPP) - Baada ya kuhudumu kama makamu wa rais wa Akufo-Addo kwa miaka minane, mwanauchumi huyo mwenye umri wa miaka 61 aliyesoma Oxford anaweza kuweka historia kama rais wa kwanza Muislamu wa nchi hiyo.

Naibu gavana huyo wa zamani wa benki kuu alipata sifa kwa ujuzi wake wa kifedha. Lakini hilo pia linaweza kuwa mvuto wake kwani amekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya Ghana kutumbukia katika mzozo mkubwa wa kiuchumi katika miaka chini ya uangalizi wake.

John Mahama (NDC) - Kushinda kura hii kutamaanisha kurejea kwa mzee huyo mwenye umri wa miaka 65 kwani tayari alihudumu kama rais kwa miaka minne na nusu kuanzia 2012 lakini akashindwa katika uchaguzi wa 2016. Akiwa ofisini, alipewa jina la utani “Bw Dumsor”, ambalo ni rejeleo la kukatika kwa umeme kulikokumba muda wake wa uongozi. Katikati ya uchumi mgumu wa sasa, Mahama ameahidi "kuweka upya kwa dharura" kwa nchi ambayo inahitaji kiongozi mwenye uzoefu katika usukani.

Miongoni mwa wagombea wengine wanaovutia ni:

Nana Kwame Bediako - Mfanyabiashara huyo, anayejulikana pia kama "Cheddar", hana historia ya kisiasa lakini amefanya athari nyingi kwenye mitandao ya kijamii na kuvutia wafuasi wachanga.

Alan Kyerematen - Waziri wa zamani, aliyepewa jina la utani "Alan Cash", aliondoka NPP mwaka jana baada ya kulalamika kwamba kura za mchujo za urais zilikuwa na upendeleo dhidi yake. Anaweza kupata uungwaji mkono wa NPP katika kitovu cha chama katika eneo la Ashanti.

Masuala muhimu ni yapi?

Masuala ya kiuchumi yamezidisha wasiwasi wa watu katika maandalizi ya uchaguzi, hasa kupanda kwa gharama ya maisha. Mwishoni mwa 2022, mfumuko wa bei wa kila mwaka ulifikia 54%. Imeshuka tangu wakati huo lakini bei bado inapanda kwa kasi.

Benki ya Dunia ilisema kiasi cha Waghana 850,000 wanaweza kuwa wameingizwa kwenye umaskini mwaka 2022 kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma. Hawa "maskini wapya" walijiunga na milioni sita ambao tayari walikuwa wanaishi katika umaskini.

Kufikia mwisho wa mwaka wa 2022, fedha za serikali zilikuwa zimepungua ikiwa imesalia kidogo kusaidia bajeti ya nchi, na kulazimisha Ghana kwenda kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwa ajili ya usaidizi.

Ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kuhama kwa Waghana wanaotafuta fursa bora kwingineko pia kumekuwa kipengele cha miaka ya hivi karibuni.

NDC imekashifu hili kama "utendaji mbaya" na imedai kurekebishwa.

NPP inayoongoza inasema imejenga uchumi thabiti ambao uko kwenye "kilele cha ... mabadiliko" kwa hivyo sio wakati wa kubadilika.

Wasiwasi juu ya athari za kimazingira za uchimbaji haramu wa dhahabu - unaojulikana nchini kama "galamsey" - umekuwa gumzo lingine kuu. Msururu wa maandamano juu ya tabia hiyo, ambayo imesababisha uchafuzi wa mito kadhaa mikubwa yenye kemikali hatari, yamefanyika katika maandalizi ya upigaji kura.

Pande zote mbili kuu zinakubali kwamba suala hilo linahitaji kushughulikiwa, lakini wakati NPP inasema ni muhimu kwa uchumi kuruhusu baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini kuendelea na kazi yao, NDC inataka kuwepo kwa udhibiti mkali zaidi na kuzuiwa kwa leseni mpya.

Je, uchaguzi unafanyika vipi?

f

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Uchaguzi uliopita wa 2020 ulifanyika chini ya vizuizi vya covid

Ili kushinda uchaguzi wa urais katika awamu ya kwanza, mgombea lazima apate zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa. Iwapo hakuna atakayepitisha kiwango hicho basi duru ya pili ya mchujo itakayoshirikisha wagombea wawili walio na idadi kubwa ya kura itafanyika mwishoni mwa Disemba.

Uchaguzi wa ubunge unaendeshwa kwa msingi wa nafasi ya kwanza na mshindi ni mgombea katika kila eneo lenye kura nyingi zaidi, hata ikiwa ni chini ya 50%.

Siku ya uchaguzi, kila mpiga kura anaweza kufika katika kituo alichopangiwa cha kupigia kura akiwa na kitambulisho cha mpiga kura, ambapo alama za vidole vyao vitakaguliwa kielektroniki na kisha kupewa karatasi mbili za kupigia kura. Kila mtu ambaye amepiga kura yake basi kidole chake kidogo kiwekewe wino usiofutika ili kuzuia kupiga kura mara ya pili.

Nini kimetokea katika chaguzi zilizopita?

Tangu mwaka wa 1992, Ghana imekuwa na chaguzi kadhaa zenye mchuano mkali za urais.

Mnamo 2008, chini ya nusu ya asilimia iliwatenganisha wagombea hao wawili katika duru ya pili.

Katika uchaguzi huo miaka minne baadaye, mshindi, Mahama, alinyakua 50% katika duru ya kwanza kwa chini ya kura 80,000.

Matokeo hayo yalizua malalamiko ya kisheria kutoka kwa chama cha NPP, ambacho kilisema kwamba karatasi za kujumlisha kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ziliingiliwa. Changamoto hiyo haikufaulu, lakini ilisababisha tume ya uchaguzi kuanzisha hatua mpya za kuhakikisha uwazi zaidi.

Waangalizi wa uchaguzi mara kwa mara wamepongeza jinsi upigaji kura ulivyoendeshwa.

Tutajua matokeo lini?

Kulingana na chaguzi zilizopita, tume ya uchaguzi huenda ikatangaza matokeo kufikia tarehe 10 Disemba.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah