Utafutaji wa nyambizi ya Titan: “Unatia saini orodha ya namna utakavyo kufa”

.

Chanzo cha picha, Mean PA

Maelezo ya picha, Picha ya faili ya mambo ya ndani ya submersible.

Mamlaka zinakimbizana na muda kutafuta nyambizi ya kibiashara iliyopotea siku ya Jumapili ikiwa na watu watano – waliokuwa wanakwenda kutazama mabaki ya meli iliyozama ya Titanic. Watu wawili ambao walifanya safari kama hiyo mwaka uliopita, wanatueleza hofu na uzoefu wao.

Nyambizi hiyo iitwayo Titan inamilikiwa na kampuni ya OceanGate, ilipoteza mawasiliano na inaaminika iko kwenye kina kikubwa cha maji mbali na fukwe ya Newfoundland, nchini Canada katika bahari ya Atlantiki.

Kwa mujibu wa ripota wa runinga ya CBS, David Pogue ambaye ameeleza safari yake ya mwaka 2022 – “haiwezekani kujiokoa bila ya msaada. Pia, itakuwa changamoto kwa timu za waokoaji kuipata nyambizi hiyo ndani ya muda, ameiambia BBC.”

Kwa mujibu wa Pogue, abiria wanafungiwa eneo la ndani la chumba kikuu na nati kadhaa hufungwa kwa nje, na zinapaswa kufunguliwa na timu kutoka nje.

Anaelezea nyambizi ina namna saba ya kuwawezesha abiria kurudi katika sehemu ya juu ya bahari, na inaogopesha kwamba hakuna hata namna moja kati ya hizo iliyofanya kazi hadi sasa. Vilevile, Pogue anaeleza uwezo wa chombo hicho kurudi juu hautakuwa na maana ikiwa kimekwama au kutoboka. “Hakuna cha kukusaidia, hakuna kifaa cha kutorokea,” ameongeza.

Wakati huo huo, mwandishi wa vichekesho vya runinga Mike Reiss, aliyefanya safari mwaka uliopita, anaweka wazi kwamba hana matumaini na hatima yao.

“Najua mipangilio na najua ukubwa wa bahari, na naelewa udogo wa nyambizi hii,” ameiambia BBC. “Ikiwa iko chini kabisa ya bahari, sijui nani ataifikia seuze kuileta juu,” ameongeza. Reiss anaweka wazi, kila mmoja anajua hatari kabla ya kwenda huko.

“Unatia saini andiko lenye orodha moja baada ya nyingine ya ambavyo unaweza kufa katika safari. Wanataja kifo mara tatu katika ukurasa wa mbele, ili uendelee kukumbuka.”

“Nilipokuwa naingia katika nyambizi, mawazo yangu yalikuwa huu unaweza kuwa mwisho wangu,” anasema. “Hakuna mtu ambaye anaingia akiwa hajajitayarisha. Kila mmoja anajua amejiingiza kwenye hali gani.”

“Ni uvumbuzi sio matembezi. Sio ya kutafuta furaha, sio ya kupaa angani. Ni wasafiri na wavumbuzi wanaotaka kuona kitu,” anaongeza.

Kuzamia hadi kuyafikia mabaki ya Titanic inachukua masaa nane. Lakini timu ya nyambizi ya Titan ilipoteza mawasiliano na meli kubwa ndani ya saa moja na dakikia 45 baada ya kuzamia baharini, kwa mujibu wa kikosi cha walinzi wa pwani ya Marekani.

.

Chanzo cha picha, Mean PA

Maelezo ya picha, Nyambizi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nyambizi hiyo mara nyingi hubeba oksijeni inayodumu siku nne kwa ajili ya timu. OceanGate hutoza dola za kimarekani 250,000 kwa mtu mmoja kwa siku nane za safari kutoka pwani ya Canada kuelekea yalipo mabaki ya Titanic.

Vikosi vya wana maji wa Marekani na Canada, na kampuni nyingine za kibiashara zinasaidia katika operesheni ya utafutaji.

Jingine linalozidisha ugumu wa operesheni hiyo ni ukweli kuwa GPS haifanyi kazi chini ya bahari na mawasiliano ya redio pia. Maanake hakuna njia ya kuwasiliana na chombo hicho.

“Meli ya msaada inapokuwa karibu na nyambizi inaweza kutuma ujumbe mfupi wa maandishi. Ni wazi kwamba kwa sasa hawapokei tena jawabu,” Pogue anaeleza na kukumbuka Titan ilipopotea kwa masaa matatu katika safari ambayo yeye alishiriki mwaka jana.

Mabaki ya Titanic yanapatikana kilomita 700 Kusini mwa kisiwa cha Newfoundland, ingawa operesheni ya utafutaji inafanyika ikitokea Boston, Massachusetts, Marekani.

Miongoni mwa wasafiri katika nyambizi hiyo ni bilionea wa Uingereza, mfanyabiashara na mvumbuzi Hamish Harding kwa mujibu wa familia yake.

Mfanyabiashara wa Kipakistan, Shahzada Dawood na mtoto wake Suleiman pia walikuwemo. Familia imeeleza. Pia, yumo mvumbuzi wa Ufaransa, Paul Henry Nergeolet, BBC imeweza kuthibitisha hilo. Pia, inaamini mkurugenzi wa OceanGate, Rush yumo katika nyambizi.

Taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, OceanGate inaeleza, “kipaumbele ni kwa timu iliopo katika nyambizi hiyo na familia zao.” Kampuni hiyo imeongeza kwa kusema, inashukuru kwa msaada mkubwa unaotolewa na mashirika ya kiserikali na kampuni zinazojihusisha na operesheni za chini ya maji.