Barua iliowasili baada ya miaka 100 kwa aliyeandikiwa

Mnamo Februari 1916 barua ya kibinafsi iliyoelekezwa kwa "Katie Mpenzi Wangu" ilitumwa ambapo kwa sababu fulani haikuishia kumfikia.
Na ilichukua zaidi ya miaka 100 kwa bahasha ambayo ilitumwa nayo kufika kwenye anwani ambapo Katie alikuwa wakati huo, katika jumba moja la ghorofa huko Crystal Palace, kaskazini mwa Norwood, eneo lililo kusini mwa London.
Ilikuwa ni mwaka wa 2021 wakati Finlay Glen alipopokea nyumbani kwake iliopo barabara ya hamlet, Crystal Palace, bahasha yenye alama ya posta ya Bath na muhuri wenye picha ya King George V kwa thamani ya 1d, kama senti ilivyoitwa karne iliyopita. .
"Ni wazi, tulishangaa sana na kushangazwa na jinsi gani ingeweza kuwepo kwa zaidi ya miaka 100," Glen alisema.
Huduma ya posta ya Uingereza, Royal Mail, ilikubali kwamba bado "haijui ni nini kilifanyika katika tukio hili."
Hakuna ajuaye jinsi barua - iliyotumwa miaka miwili kabla ya Vita vya Kwanza Dunia nchini Uingereza na wakati Mfalme George V alikuwa kwenye kiti cha enzi kwa miaka mitano tu - haikuwasilishwa kwa miaka mingi.
Udadisi
Ingawa Sheria ya Huduma za Posta ya 2000 inafanya kuwa kosa kufungua barua ambazo hazijatumwa kwako, Glen alisema ilionekana kuwa "sawa" kuifungua alipogundua kuwa ilikuwa ya 1916 na sio 2016.
"Ikiwa nimefanya uhalifu, naweza tu kuomba msamaha," aliongeza meneja wa ukumbi wa michezo mwenye umri wa miaka 27.

Chanzo cha picha, FINLAY GLEN
Barua hiyo iliandikwa kwa "Katie mpenzi wangu", mke wa mfanyabiashara wa stempu anayejulikana kama Oswald Marsh.
Kulingana na Stephen Oxford, mhariri wa Norwood Review, jarida la robo mwaka la historia ya eneo hilo, Marsh alitambuliwa sana kwa kazi yake na mara nyingi alihitajika kutoa ushahidi kama mtaalamu wa kesi za ulaghai wa stempu.
Barua hiyo iliandikwa na Christabel Mennell, rafiki wa familia na binti ya Henry Tuke Mennell, mfanyabiashara tajiri wa chai wa eneo hilo, alipokuwa likizoni huko Bath, jiji lililo kusini magharibi mwa Uingereza.
Katika maandishi hayo, Mennell alisema kwamba alihisi "aibu sana juu yangu baada ya kusema nilichosema" , na kwamba amekuwa akihisi vibaya kutokana na "baridi mbaya sana".
Tazama yaliyopita
Akizungumzia ugunduzi huo, Oxford alisema "haikuwa wa kawaida sana na wa kusisimua sana katika suala la kutoa fununu kuhusu historia ya eneo hilo na watu walioishi Norwood, ambayo ilikuwa mahali maarufu sana kwa watu wa tabaka la kati mwishoni mwa 1800".

Chanzo cha picha, ANNUAL MONITOR
"Crystal Palace ilizalisha wimbi kubwa la watu matajiri sana, kwa hivyo kufahamu kuhusu mtu aliyehamia eneo hilo labda kwa sababu hiyo hiyo ni ya kuvutia sana," mwanahistoria aliongeza.
Alipoulizwa angefanya nini iwao jamaa za mtumaji au mpokeaji iliwasiliana naye, Glen alijibu kwamba "ni sehemu ya ajabu ya historia ya familia yake ambayo imetokea. Ikiwa wanataka, wanaweza kuja."
Msemaji wa Royal Mail alisema: "Matukio kama haya hutokea mara chache sana, na hatuna uhakika ni nini kilifanyika katika kesi hii.
"Tunafahamu kwamba watu watavutiwa na hadithi ya barua hii ya 1916, lakini hatuna habari zaidi kuhusu kile ambacho kinaweza kutokea," alilalamika.












