Rais alitangaza ubakaji kuwa janga la kitaifa. Nini kilitokea baadaye?

tt

Tyson Conteh & Tamasin Ford,

BBC Africa Eye, Makeni & London

Mwaka wa 2019 Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio alichukua hatua ya kijasiri kutangaza ubakaji na unyanyasaji wa kingono kuwa janga la kitaifa. Miaka mitano baadaye, BBC Africa Eye inachunguza kama walionusurika katika mashambulizi wanapata haki.

Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo yanaweza kuwakasirisha baadhi ya wasomaji.

Katika jiji la Makeni, umbali wa saa tatu kwa gari mashariki mwa mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, mama mdogo ameketi nje ya nyumba yake na binti yake wa miaka mitatu.

Anita, ambalo si jina lake halisi, anaelezea siku ya mnamo Juni 2023 alipompata mtoto wake mchanga akivuja damu kutoka kwa nepi yake.

"Nilimfanyia kazi mwanamke huyu, na alinipa kazi Jumamosi asubuhi hiyo ili niende sokoni," anasema, akieleza kwamba alimwacha mtoto wake kwa mwajiri wake na mwanawe wa miaka 22.

"Alichukua mtoto wangu, akisema anaenda kumnunulia peremende na biskuti. kume ilikuwa uongo."

Aliporudi, aligundua kuwa binti yake hayupo. Baada ya kumtafuta kwa muda, waliungana tena lakini mama huyo mwenye umri wa miaka 22 aliona kwamba mtoto wake mdogo alikuwa akivuja damu. Alimpeleka hospitali na baada ya kushonwa nyuzi mbili, ikathibitishwa kuwa amebakwa.

"Wauguzi wakaanza kumchunguza mtoto, wakasema: 'Ee Mungu wangu, mtu huyu amemfanyia nini mtoto huyu?' Daktari aliyekuwa akimtibu mtoto wangu hata alilia."

Anita alienda polisi kushtaki tukio hilo lakini mwanamume huyo alikimbia na mwaka mmoja umepita polisi hawajafanikiwa kumpata.

“Rais alitunga sheria kwamba yeyote anayebaka watoto, akamatwe na apelekwe jela,” anasema huku akikasirishwa kwamba hakuna kilichofanyika.

Anaashiria sheria kali zaidi ya makosa ya kingono iliyobuniwa miaka mitano iliyopita baada ya Rais Maada Bio kutangaza ubakaji kuwa janga la kitaifa.

Sheria zipo lakini mamlaka hazina nyenzo za kushughulikia suala hilo
Maelezo ya picha, Sheria zipo lakini mamlaka hazina nyenzo za kushughulikia suala hilo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yalifuatia maandamano ya Desemba 2018 wakati mamia ya watu waliovalia fulana nyeupe zilizoandikwa maneno "Hands off our girls" walipoandamana Freetown.

Taarifa za ubakaji mwingine wa mtoto zilishangaza taifa - msichana wa miaka mitano ambaye aliachwa akiwa amepooza kuanzia kiunoni kwenda chini. Iliripotiwa wakati huo kwamba visa vya unyanyasaji wa kijinsia viliongezeka karibu mara mbili ndani ya mwaka mmoja, theluthi moja ikihusisha watoto. Wananchi wa Sierra Leone walikuwa wamechoshwa.

Hali ya hatari iliyodumu kwa muda wa miezi minne kuanzia Februari 2019 ilimruhusu rais kutumia raslimali za serikali kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia.

Kifungu cha sheria kilichoboreshwa kuhusu Makosa ya Kingono, iliyotoa adhabu kali zaidi kwa wanyanyasaji wa kijinsia kiliidhinishwa.

Hukumu za ubakaji ziliongezwa hadi angalau miaka 15, au kifungo cga maisha ikiwa ilihusisha mtoto. Mahakama maalum ya kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kingono iliundwa mjini Freetown mwaka uliofuata.

Inaonekana ilisaidia- visa vya unyanyasaji wa kingono na kijinsia viliripotiwa kupungua kwa karibu 17%, kutoka zaidi ya visa 12,000 mnamo 2018 hadi zaidi ya 10,000 mnamo 2023, kulingana na takwimu za polisi.

Kuongeza ufahamu na miundo mipya ni jambo moja, lakini kuhakikisha kuwa watu, kama binti ya Anita, wanapata haki ni jambo lingine.

Mpango wa Rainbo ni shirika la kitaifa la kutoa misaada linalofanya kazi na waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia.Linasema kuwa mwaka 2022 ni asilimia tano tu ya visa 2,705 ilizoshughulikia zilifika Mahakama Kuu.

Moja ya changamoto ni masuala ni rasilimali zinazopatikana kwa wale wanaopaswa kutekeleza sheria.

Katika kituo cha polisi cha Makeni ambapo Anita aliripoti tuo la kubakwa kwa binti yake, Assnt Supt Abu Bakarr Kanu ambaye anaongoza Kitengo cha Kusaidia Familia (FSU) anasema wanapata takriban visa vinne vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto kila wiki.

Assnt Supt Abu Bakarr Kanu
Maelezo ya picha, ''Kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi ni changamoto”-Assnt Supt Abu Bakarr Kanu- Polisi wa Sierra Leone

Changamoto kubwa inayokabili timu yake ni ukosefu wa usafiri wa kwenda kuwakamata watuhumiwa.

Anaratibu vitengo vyote saba vya polisi mkoani humo na baadhi ya vitengo hivyo havina gari hata moja.

“Kuna wakati mshukiwa anapatikana lakini kwa sababu ya ukosefu wa usafiri huwezi kumfikia mshukiwa huyo ili kumkamata,” anasema Assnt Supt Kanu.

"Kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi ni changamoto."

Kama ilivyo kwa wengi nchini Sierra Leone, alifurahishwa na hatua ya serikali ya kutangaza hali ya dharura.

"Tuna sheria za kutosha... sheria na sera nzuri, lakini muundo na wafanyakazi ni changamoto kwetu kushughulikia kwa ukamilifu masuala ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia nchini Sierra Leone."

Hata kama mtuhumiwa amekamatwa, kufikishwa mbele ya hakimu ni pambano kubwa zaidi.

Ili kesi dhidi ya mtuhumiwa wa ubakaji isikilizwe, kuna mtu mmoja tu nchini ambaye anaweza kusaini hati hizo - mwanasheria mkuu. Ilikusudiwa kuharakisha mchakato na kupeleka kesi moja kwa moja mahakamani, lakini imeleta changamoto nyingine.

"Kwa sasa haiwezekani kuwa na afisa mwingine yeyote wa sheria au wakili mwingine yeyote kutia saini hati ya mashtaka kwa makosa yanayohusiana na uhalifu wa kingono," anasema Wakili wa Serikali Joseph AK Sesay.

"Marekebisho ya 2019 yanaeleza kuwa ni mwanasheria mkuu pekee ndiye anayeweza kusaini hati ya mashtaka. Kwa hiyo hilo limekuwa likileta changamoto linapokuja suala la kuwasilisha kesi mahakamani."

Chernor Bah
Maelezo ya picha, Chernor Bah- Waziri wa Habari

Waziri wa Habari Chernor Bah anakiri huu si mchakato kamili lakini anasema ni "mchakato ambao tutaendelea kuuboresha".

Akiwa na changamoto juu ya swali ambalo wengi wanaamini kidogo limebadilika linapokuja suala la kupata haki kwa waathirika wa ubakaji, alikiri kwamba "katika baadhi ya jamii watu wanahisi hivyo".

Lakini anapinga wazo kwamba hakuna hatua iliyopigwa.

"Nadhani mageuzi ya kimfumo ambayo tumeweka yapo. Sheria mpya zipo. Na hatua hizo, nadhani, zimetusaidia kukabilia na jinamizi la 2019."

Kwa Anita, mkazi wa Makeni, ni karibu mwaka mmoja tangu mtoto wake mchanga abakwe.

Hajapokea taarifa mpya kutoka kwa polisi, hivyo ameamua kuweka picha ya mshukiwa huyo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

"Nataka watu wanisaidie kumtafuta huyo kijana, nateka na sina furaha. Kilichompata mtoto wangu sitaki kitokee kwa mtoto mwingine."

Soma pia:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi