Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu namna ya kujihadhari na athari za El Nino
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Nafasi, BBC Swahili
Ulimwengu umeingia rasmi katika kipindi cha El Niño, kulingana na shirika la sayansi la Marekani NOAA, Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) na Umoja wa Mataifa.
Kila nchi kupitia Mamlaka zake za Hali ya Hewa zimeanza kutoa taarifa ya tukio hili la asili linalotokea kila baada ya miaka kadhaa baada ya kuonekana kwenye mifumo yao ya hali ya hewa.
Nchini Tanzania Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania (TMA) nayo imethibitisha kwamba nchi hiyo inatarajiwa kukumbwa na El Nino
Ni tukio lisilotabirika sana kwenye kiwango cha athari zake, lakini kawaida El Nino huathari hali ya hewa duniani, kuanzia joto kali, mvua nyingi na katika baadhi ya maeneo husababisha Ukame. Kwa ukanda wa Afrika katika kipindi cha miezi michache ijayo inatarajiwa kukumbwa na mvua kubwa.
Mbali na mvua kubwa, wataalamu wa Hali ya hewa wameonya kuwa huenda El Nono ya Mwaka huu ikasababisha mwaka 2024 kuwa mwaka wa joto kali zaidi duniani.
Je mataifa na wananchi wanapaswa kujiaandaaje na tukio hili linalodumu kwa miezi mpaka 12?
El Nino ni nini?
El Nino ni sehemu ya tukio la asili la hali ya hewa linaloitwa El Niño Southern Oscillation (ENSO). ENSO ina asili mbili zinazokinzana: El Niño na La Niña - ambazo zote zinabadilisha hali ya hewa duniani kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) El Nino ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki katika Bahari ya Pasifiki. Hali hii kwa kawaida huambatana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko.
Tukio la El Niño kwa kawaida huthibitishwa wakati ambapo halijoto ya uso wa bahari katika eneo la tropiki ya Pasifiki ya mashariki inapopanda hadi angalau 0.5C juu ya wastani wa kawaida na kwa muda mrefu.
La Niña ambayo si maarufu sana ni kinyume chake, Wakati halijoto ya uso wa bahari inaposhuka kwa karibu nyuzi joto 3-5, La Niña hutangazwa. Hii inasababisha hali ya hewa ya baridi na kavu kwa wastani katika sehemu za Bahari ya Pasifiki, kati ya Amerika Kusini na Australia.
Tukio la El Niño inahusiana na joto la maji ya bahari ya Pasifiki ambalo hutokea kila baada ya miaka mitatu au minane na hudumu kwa miezi 9-12, kwa mujibu wa wataalamu.
Inaelezwa tangu mwaka 1900 kumekuwa na angalau matukio 30 ya El Niño duniani huku El nino ya mwaka 1982-83, 1997-98 na 2014-16 ni miongoni mwa matukio yaliyoweka rekodi na kuleta madhara makubwa.
Katika miaka ya 2000, matukio ya El Niño yamejitokeza mwaka wa 2002–03, 2004–05, 2006–07, 2009–10, 2014–16, 2018–19, na sasa mwaka 2023 limeanza ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa kati ya mwezi Septemba 2023 na Februari 2024.
Athari za El Lino
Ingawa athari zake hutofautiana kila linapotokea, Lakini ni tukio linalosababisha matukio makubwa mbalimbali ya hali mbaya ya hewa, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko, vimbunga, na mawimbi ya joto, ambayo yote ni hatari kwa afya ya binadamu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, El Niño ya sasa inatarajiwa kuathiri maeneo mengi ulimwenguni lakini athari kubwa zaidi zitaonekana kwenye maeneo yenye hali ya ya joto, ikiwa ni pamoja na nchi na maeneo ya Afrika, Amerika ya Kusini, pamoja na Kusini na Kusini-Mashariki mwa Asia ambako huathirika zaidi na majanga ya asili.
Shirika la afya duniani limezitaka nchi zijiandae na athari zifuatazo za kiafya:
Uhaba wa chakula na kuongezeka kwa utapiamlo wa wastani na wa hali ya juu hasa miongoni mwa walio hatarini zaidi na Kuongezeka kwa magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu kutokana na uhaba wa maji au mafuriko na miundombinu ya vyoo.
Athari zingine ni Ongezeko la milipuko ya magonjwa yanayoenezwa na mbu kama vile malaria katika maeneo ya nyanda za juu ambayo kwa kawaida ni baridi sana, ongezeko la hatari ya Homa ya Bonde la Ufa na Kuongezeka kwa idadi ya watu walioathiriwa na magonjwa ya kuambukiza kama vile surua na uti wa mgongo
Kukatizwa kwa huduma za afya kutokana na ukosefu wa maji katika hali ya ukame au uharibifu wa miundombinu ya afya kutokana na mafuriko na vimbunga, Joto kali na ongezeko la hatari ya kutokea kwa moto wa mwituni katika baadhi ya maeneo yatakayokumbwa na ukame ni miongoni mwa athari zinazotarajiwa.
Ulimwengu unajiandaaje na El Nino?
Ingawa athari halisi za matukio ya El Nino haziwezi kutabiriwa kwa usahihi, lakini Ulimwengu umekuwa ukijiandaa kwa athari za tukio hilo kupitia ufuatiliaji endelevu wa utabiri, tathmini za hatari, uimarishaji wa juhudi zinazowezekana za kukabiliana, kujiandaa, kuwa na mipango ya dharura na kuimarisha mifumo ya kukabiliana na magonjwa na athari zingine ziletazwo na El Niño
Ukiacha joto, mvua na Ukame, El Nino pia husababisha athari kiuchumi, kimazingira na kiafya. Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa hivi karibuni na jarida la Sayansi, ulimwengu huenda ukapata hasara ya hadi dola trilioni 3 za Marekani.
Kupungua kwa uzalishaji wa kilimo, usalishaji wa viwanda, kuenea kwa magonjwa ni athari zinginge zinazotarajiwa.
Peru ambako iko chimbuko la El Nino imetenga dola bilioni 1.06 kujiandaa, Ufilipino imeunda timu maalum ya kushughulikia athari zozote ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa El Nino huku Marekani, India, Australia na China zimeanza kuchukua hatua madhubuti za kutenga fedha, vyombo na timu za wataalamu kukabiliana na tukio hilo.
Wewe unapaswa kujiandaaje?
Mamlaka zote za hali ya hewa duniani hujaribu kutahadharisha kuhusu athari za El Nino na kutoa wito wa wananchi kuchukua tahadhari.
Kwa kifupi mbali na hatua zinazofanywa na nchi kupitia Mamlaka zake kwenye kufuatilia tukio hili na kulitolea taarifa mara kwa mara na hatua za kuchukua, mwananchi wa kawaida na yeye ana jukumu la kufanya, ili kujiandaa na kuchukua tahadhari asiathirike na athari zinazoletwa na El Nino.
Baadhi ya hatua za kuchukua, zinazopendekezwa na wataalamu ni;
- Kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini kwako.
- Kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa watalaamu katika sekta husika ili kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.
- Epuka kukaa, kutembea sehemu hatarishi kama kwenye mikondo ya maji na umeme hasa kipindi cha mvua na upepo mkali.
- Kuhama kwenye maeneo ya mabonde hasa nyakati za mvua zinapoanza
- Wakati wote kuwa na akiba ya chakula, fedha, maji, dawa (kwa maelekezo) na vifaa vya huduma ya kwanza (First Aid Kit).
- Msaidie jirani yako kwenye dharura.
- Kuwa na mawasiliano ya watoa huduma za dharura, ya majirani zako na ya kiongozi wako wa eneo unaloishi.
- Shirikisha majirani, ndugu na jamaa taarifa muhimu kuhusu El Nino.
- Toa taarifa kwa Mamlaka inapotokea dharura yoyote katika eneo lako unaloishi.