Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfahamu bilionea wa Urusi anayethubutu kuzungumza dhidi ya Putin
Boris Mints ni mmoja wa wafanyabiashara wachache matajiri wa Urusi waliozungumzia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na sambamba na kumkosoa Rais Vladimir Putin.
Wengi wa watu mashuhuri nchini Urusi wamekaa kimya juu ya vita vinavyoendelea, wakiepuka ukosoaji wa Kremlin.
Kwa mujibu wa Bw Mints: ni kwamba "Wote wanaogopa."
Ikulu ya Kremlin inafahamika sana kwa kuwakandamiza wakosoaji wakubwa wa Rais Putin huku maudhui ya vituo vya habari vya Urusi yakidhibitiwa. Maandamano yasiyoidhinishwa pia yamepigwa marufuku nchini humo tangu 2014.
Bw Mints alisema "mtu yeyote" ambaye anamkosoa Putin waziwazi "ana sababu za kuwa na wasiwasi kuhusu usalama binafsi".
Hata hivyo, katika mahojiano yaliyofanywa kwa njia ya barua pepe, aliiambia BBC: "Sina nia ya kuishi katika makazi ya mabomu, kama Bw Putin anavyofanya."
Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 64, ambaye alijipatia utajiri wake kupitia kampuni ya uwekezaji ya O1 Group, ambayo aliianzisha mwaka wa 2003 na kisha kuuzwa mwaka wa 2018, alisema kuwa nchini Urusi "njia ya kawaida" ya kuadhibu mmiliki wa biashara kwa "kutovumilia" kwao kwa serikali ilikuwa "kufungua kesi ya uongo na ya jinai dhidi ya biashara zao".
"Kesi hizo za jinai zitawaathiri sio tu wamiliki wa biashara peke yake, lakini pia familia zao na wafanyakazi," alisema.
"Kiongozi yeyote wa biashara anayejitegemea mbele ya macho ya Putin anaonekana kama tishio kwani anaweza kuwa na uwezo wa kufadhili upinzani au kukuza maandamano kwa hivyo, watu hao wanaonekana kama maadui wa Putin na, kwa hivyo, kama maadui wa serikali," aliongeza.
'Kifungo kisichoepukika'
Ni hali ambayo Bw Mints anakutana nayo kwa mara ya kwanza, baada ya kuzungumza hadharani dhidi ya sera za Rais Putin mwaka 2014 baada ya Crimea kutwaliwa kutoka Ukraine.
Mints alihisi alihitaji kuondoka Urusi mwaka wa 2015 na kuelekea Uingereza "katika muktadha wa kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya upinzani wa kisiasa", huku Boris Nemtsov akiuawa kwa kupigwa risasi mwaka huo huo.
Bw Nemtsov alikuwa hasimu mkali wa Rais Putin. Mauaji yake mwaka wa 2015 ni mauaji ya kisiasa yaliyotajwa zaidi tangu Bw Putin aingie madarakani. Hata hivyo mamlaka ilikanusha na inaendelea kukanusha kuhusika.
Miaka miwili baadaye, kampuni ya zamani ya uwekezaji ya Bw Mints ya O1 Group "ilijipata katika mzozo wa wazi dhidi ya Benki Kuu ya Urusi", alisema, huku kesi za kisheria zikianza katika maeneo kadhaa.
“Mambo kama haya yanapoanza kutokea, ni ishara tosha kwamba mtu anatakiwa kuondoka nchini mara moja,” alisema.
Anasalia kuwa chini ya hatua za sasa za kisheria na Kremlin.
Ni kwa sababu ya hatua hiyo kwamba Bw Mints anapendekeza "hatua ya kijasiri zaidi" kwa Warusi matajiri ambao hawampendi Rais Putin ni "kwenda kimyakimya uhamishoni", akitoa mfano wa kesi ya Mikhail Khodorkovsky, ambaye wakati mmoja alikuwa tajiri zaidi wa Urusi, lakini alifungwa jela kwa karibu muongo mmoja kwa madai ya ulaghai na ukwepaji kodi ambayo, anasema, yalichochewa kisiasa.
Wawili kati ya matajiri wakubwa nchini humo Mikhail Fridman na Oleg Deripaska waliacha kumkosoa moja kwa moja Rais Putin walipotoa wito tofauti wa amani nchini Ukraine.
Bw Fridman, bilionea wa benki, alisema matamshi yoyote ya kibinafsi yanaweza kuwa hatari sio kwake tu bali pia kwa wafanyakazi wake na familia nzima.
Hata hivyo, Bw Mints ameungana na tajiri wa Kirusi Oleg Tinkov, mwanzilishi wa Benki ya Tinkoff na mmiliki wa zamani wa timu ya waendesha baiskeli Tinkoff-Saxo, katika kulaani uvamizi huo.
Mints alitaja hatua za Rais Putin kuwa "mbaya", akisema uvamizi huo ulikuwa "tukio la kusikitisha zaidi katika historia ya hivi majuzi, sio tu ya Ukraine na Urusi, lakini ulimwenguni kwa ujumla".
Pia alilinganisha na uvamizi wa Adolf Hitler huko Poland mwaka 1939.
"Vita hivi ni matokeo ya kujilimbikizia madaraka kwa mtu mmoja, Vladimir Putin, akiungwa mkono na watu wake wa ndani," alisema Bw Mints, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mmoja wa wasimamizi wakuu wa mali ya pensheni nchini Urusi hadi 2018.
BBC imewasiliana na Kremlin ili kupata maoni yake.
'Alifutwa kazi siku moja baada ya kukutana'
Bw Mints alitambulishwa kwa Rais Putin kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1990 lakini alizungumza naye ana kwa ana tarehe 2 Januari 2000, siku mbili baada ya Bw Putin kuteuliwa kuwa kaimu rais wa Urusi.
Bw Mints, ambaye alifanya kazi chini ya Rais wa zamani wa Urusi Boris Yeltsin katika miaka ya 1990, alikuwa na hamu ya kujadili mipango yake ya kurekebisha serikali za mitaa ili kukuza demokrasia ya Urusi hadi Karne ya 21.
"Bw Putin alisikiliza mapendekezo yangu bila kutoa maoni wala kubishana. Siku iliyofuata, Putin alinifuta kazi," alisema.
Alijua wakati huo kwamba maono ya Bw Putin kwa nchi yake yalikuwa "umbali wa maili" kutoka kwa utawala uliopita.
Kuacha siasa, Bw Mints alianzisha udalali wa hisa kwa wateja binafsi miaka mitatu baadaye.
Bw Mints hajaidhinishwa na serikali ya Uingereza, tofauti na wafanyabiashara wengine wa Urusi ambao wametambuliwa kuwa na uhusiano wa karibu na Kremlin.
Hata hivyo, jina lake lilionekana kwenye orodha inayoitwa "Putin list" iliyotolewa na Marekani mwaka wa 2018. Kati ya majina 210, 114 kati yao yaliorodheshwa kuwa serikalini au kuhusishwa nayo, au wafanyabiashara wakuu.
Wengine 96, ambao ni pamoja na Bw Mints, waliorodheshwa kama oligarchs waliodhamiriwa zaidi na ukweli kwamba walikuwa na thamani ya zaidi ya $1bn (£710m) wakati huo, badala ya uhusiano wao wa karibu na Kremlin.
Baba huyo wa watoto wanne aliweka orodha ya mabilionea wa Forbes mnamo 2017 na utajiri wa jumla ya $ 1.3bn, kabla ya kujiuzulu mwaka 2018.
Lakini alipuuza mapendekezo kwamba yeye ni wa kundi la oligarch.
"Sio kila mfanyabiashara wa Kirusi anamuunga mkono Putin, na vile vile kila tajiri wa Kirusi si 'oligarch'," alisema. "Nchini Urusi, neno hili linamaanisha kiongozi wa biashara ambaye ameunganishwa sana na Putin na ambaye utajiri wake, au faida ya biashara zao, hutegemea ushirikiano na serikali ya Urusi.
"Urusi sio tu uwanja wa mafuta ulio na mgodi wa alumini katikati," aliongeza. "Ni nchi ya watu milioni 140. Watu huko kama kila mahali wana mahitaji yao na mahitaji haya hayatofautiani kabisa na yale ya hapa Magharibi."
Kwa sasa anaishi Uingereza, anajisikia vizuri bila kuhitaji usalama wa ziada ili kujiweka salama yeye na familia yake, na hana nia ya kurejea Urusi hivi karibuni.