Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi na Ukraine: Ondoeni vikwazo na tutaruhusu chakula kutoka, yasema Urusi

Urusi imetoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa kutokana na uvamizi wake Ukraine kama sehemu ya "mbinu kamili" inayolenga kuepusha mzozo wa chakula duniani.

Moja kwa moja

  1. Tumefikia mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Habari za hivi punde, Makabiliano ya kuiteka barabara muhimu yaendelea huku vita vikifika katika mji wa Ukraine

    Msimamizi wa ngazi za juu mashariki mwa Ukraine amekanusha ripoti kwamba barabara muhimu inayounganisha maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine upande wa mashariki imefungwa kutoka kwa maeneo mengine ya nchi na vikosi vya Urusi.

    "Luhansk haijakatwa," mkuu wa utawala wa kijeshi wa eneo hilo, Serhiy Haidai alisema.

    Mapigano yamefikia viunga vya jiji kubwa la Severodonetsk, unaolengwa na Urusi.

    Ikiwa watateka barabara ya Bakhmut basi mji huo unaweza kuzingirwa.

  3. Kwanini mji wa Zaporizhzhia unalengwa hivi sasa?

    Kumekuwa na mashambulizi ya makombora ya Urusi katika mji wa kusini wa Zaporizhzhia katika kile kinachoonekana kuwa shambulio kubwa zaidi katika mji huo hadi sasa.

    Mtu mmoja amefariki na wengine watatu kujeruhiwa. Maafisa wa Ukraine wanasema Urusi imekusanya vikundi vitatu vya mbinu za kivita huko Vasylivka karibu kilomita 50 kusini mwa mji huo, lakini bado haijabainika iwapo wanapanga kufanya mashambulizi huko Zaporizhzhia.

    Eneo hilo ni muhimu kwa sababu ni kituo kikuu cha usafiri, hasa kwa reli. Ni muhimu kwa utengenezaji wa chuma na kuna kampuni kadhaa za ulinzi, pamoja na kiwanda cha Motor Sich ambacho hutengeneza injini za ndege na helikopta ambazo Warusi wanadai kuwa walizishambulia na pia utengenezaji wa rada.

    Hapo awali katika mzozo huo watu wengi kutoka Mariupol walikwenda katika mji huo ambao hadi sasa ulikuwa unafikiriwa kuwa salama.

    Zaporizhzhia pia iko karibu na eneo la kituo cha nguvu za nyuklia, ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya, kwenye ukingo wa kusini wa mto Dnieper.

    Wanajeshi wa Urusi wanakalia eneo hilo , na wakati wafanyakazi wa Ukraine wakikiendesha, Warusi wametuma wataalam wao wa nyuklia kufuatilia kazi yao.

    Kwa kawaida mtambo huo huzalisha zaidi ya nusu ya nishati ya nyuklia ya Ukraine na 20% ya jumla ya usambazaji wa umeme nchini humo.

    • Miili ya wanajeshi wa Urusi yatelekezwa na kuzagaa karibu na mji wa Kyiv
    • Vita vya Ukraine: Nini kinaweza kuleta usawa katika vita hivi?
  4. Ondoeni vikwazo na tutaruhusu chakula kutoka, yasema Urusi

    Urusi imetoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa kutokana na uvamizi wake Ukraine kama sehemu ya "mbinu kamili" inayolenga kuepusha mzozo wa chakula duniani.

    Ukraine ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa kuuza nafaka nje ya nchi lakini imejilimbikizia akiba kubwa ambayo haiwezi kupeleka nje ya nchi kutokana na vikwazo vya Urusi kwenye bandari zake.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kremlin Andrey Rudenko alisema Urusi iko tayari kutoa njia ya kibinadamu ambayo itaruhusu njia salama kwa meli kutoka Ukraine - ikiwa vikwazo vitaondolewa.

    Jana, Umoja wa Ulaya uliishutumu Urusi kwa kutumia chakula kama silaha yenye athari za kimataifa.

    Hapo awali, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema bei za vyakula duniani kote zitaendelea kupanda huku mzozo ukiendelea.

    • Vita vya Ukraine:Ufahamu mji wa Melitopol, unaokaidi kukaliwa na Urusi
    • Vladimir Putin: Rais wa Urusi 'chupuchupu' kuuawa
  5. Rais Samia: 'Nimewashinda marais wanaume'

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu anasema katika baadhi ya maeneo kwenye majukumu yake ya urais amesimamia vyema zaidi kuliko marais wengine wanaume waliomtangulia.Rais wa Tanzania alisema alikabiliwa na changamoto za kutoaminiwa katika siku zake za kwanza ofisini kwa sababu yeye ni mwanamke - jambo ambalo alilazimika kulishinda.

    Bi Samia alikuwa akizungumza kwenye kongamano katika mji mkuu wa Ghana Accra – ikiwa ni ziara yake ya kwanza Afrika Magharibi tangu aapishwe kuwa rais kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli Machi 2021.“Ilikuwa vigumu sana kuwafanya watu wa Tanzania kuniamini.

    Kwamba naweza kuendesha nchi sawa na wanaume – hiyo ndiyo ilikuwa changamoto kubwa,” alisema wakati wa kikao kilichoandaliwa kama sehemu ya mkutano wa kila mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)."Katika kipindi cha mwaka mmoja nimeonyesha nguvu za wanawake, niliongoza nchi kama wanaume walivyofanya na katika mazingira mengine kwa ubora kuliko wao," aliongeza.

    Kiongozi huyo wa Tanzania aliliambia jukwaa la AfDB kwamba ukuaji wa uchumi wa nchi umeshuka kutoka 6.4% hadi 4% wakati wa janga la Covid - lakini chini ya uongozi wake ulipanda hadi 5.2% na ilitabiriwa kufikia 6.7% ifikapo 2025.Kongamano hilo lililofanyika mjini Accra pia lilihudhuriwa na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na Rais wa Comoro Azali Assoumani.

  6. Majina ya wahanga wa kwanza wa shambulio la shule Marekani yatolewa

    Vyombo vya habari vya Marekani sasa vimemtaja mwalimu wa pili aliyeuawa katika shambulizi hilo kuwa ni Irma Garcia, ambaye alifundisha katika Shule ya Msingi ya Robb kwa miaka 23, kulingana na maelezo ya shule yake.

    Alikuwa na watoto wanne na alipenda kuchoma nyama na mume wake na kusikiliza muziki.

    Mwanawe alisema rafiki wa sheria ambaye alikuwa katika eneo la tukio alimwona Garcia akiwakinga wanafunzi wake, NBC inaripoti.

    Majina mengine ya waliothibitishwa kufariki ni:

    Mwalimu mwenza: Eva Mireles, ambaye alifundisha wanafunzi wa darasa la nne shuleni.

    Alipigwa risasi na kuuawa na Salvador Ramos alipokuwa akijaribu kuwalinda wanafunzi wake, shangazi yake, Lydia Martinez Delgado, aliambia New York Times.

    Watoto: Xavier Lopez na Amerie Garza, wote wenye umri wa miaka 10, na Uziyah Garcia mwenye umri wa miaka minane.

  7. FBI yazuia njama ya kuuawa kwa George W Bush

    Shirika la FBI limefanikiwa kugundua na kuzia njama za kumuua rais wa zamani wa Marekani George W Bush iliyopangwa kufanywa na mfuasi mmoja wa kundi la Islamic State, mamlaka za Marekani zimesema.

    Sasa yuko kizuizini na alifikishwa katika mahakama ya Ohio siku ya Jumanne.

    FBI ilitumia taarifa za kichunguzi na ufuatiliaji wa kielektroniki ili kutatiza mpango wake.

    Kulingana na hati za mahakama, mshukiwa huyo aliyetambuliwa kama Shihab Ahmed Shihab, 52 - ni raia wa Iraq ambaye amekuwa Marekani tangu 2020 na alikuwa na ombi lake la kuomba hifadhi ambalo liliwekwa pembeni kusubiri.

    Katika mazungumzo na chanzo cha FBI, Shihab alisema alitaka kumuua Bush kwa "kuua Wairaq wengi" na "kuigawanya" Iraq.

    Aliongeza kuwa anatumai kushiriki katika oparesheni hiyo binafsi "na hakujali kama angefariki, kwani angejivunia kuhusika".

    Shihab alidaiwa kuviambia vyanzo alivyotarajia kuwatumia kusafirisha watu kwa njia ya magendo kuwa atawaleta wanachama wa Islamic State nchini Marekani, ingawa hashutumiwa kuwa mwanachama wa kundi hilo la kigaidi.

    Katika tukio moja, Shihab na mmoja wa watoa habari walienda Dallas, Texas kuchukua video ya makazi ya Bush na Taasisi ya George W. Bush.

    Machi 2022, alidaiwa kufanya mkutano katika chumba cha hoteli cha Columbus, Ohio kuangalia silaha na sare ghushi za polisi.

    Sasa anakabiliwa na miaka 10 jela kwa kujaribu kuleta mtu kinyume cha sheria nchini Marekani, na mingine 20 kwa kusaidia jaribio la mauaji ya afisa wa zamani wa Marekani.

    Msemaji wa Bush alisema rais huyo wa zamani "ana imani Huduma ya Siri ya Marekani na jumuiya zetu za kutekeleza sheria na kijasusi".

    • Mwanamume aliyekuwa akisakwa sana na FBI akamatwa
    • Vita vya Iraq:Bush na Clinton walaumiana
  8. Ethiopia haijafurahishwa na namna Abiy aliyoelezewa kwenye orodha ya Time 100

    Ethiopia inasema imekasirishwa na jinsi jarida la Marekani, Time, lilivyomuelezea kiongozi wa nchi hiyo wakati lilipotangaza orodha ya watu wenye ushawishi mkubwa wa mwaka huu.

    Jarida la Time limemjumuisha Waziri Mkuu Abiy Ahmed na raia wa Marekani na mwanasayansi wa kompyuta mzaliwa wa Ethiopia Timnit Gebru katika orodha ya hivi karibuni ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi 2022.

    Time ilisema mkataba wa amani wa Bw Abiy na Eritrea ''ulipanda mbegu za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia'.

    Pia ilisema kuwa Bw Abiy, pamoja na kiongozi wa Eritrea, ''walianzisha kampeni ya kijeshi dhidi ya'' viongozi wa kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF).

    Katika barua kwa jarida hilo afisi ya Bw Abiy ilisema ''wamefadhaishwa'' na jinsi ambavyo amewakilishwa pamoja na kuonyesha kuhusu nani aliyeanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

    Taswira yake imeelezewa kama ''muhusika wa mauaji' na inaishutumu kwa kurudia masimulizi ya TPLF - kikosi ambacho kimekuwa kikipigana na wanajeshi kaskazini.

    Imeliomba gazeti hilo kutoa maelezo. Hakuna majibu yoyote kutoka kwa jarida hilo.

    Pande zote zinazopigana zimeshutumiwa kukiuka haki za binadamu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia.

    Mzozo nchini Ethiopia ulianza tarehe 4 Novemba 2020 wakati Bw Abiy alipoamuru mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vikosi vya eneo la Tigray baada ya vikosi vya TPLF kuteka kambi ya kijeshi ya nchi hiyo.

    • Mgogoro wa Ethiopia wa Tigray: Jinsi TPLF ilivyolizidi maarifa jeshi la Ethiopia
    • Mzozo wa Ethiopia: Mgogoro ulioikumba Ethiopia una maana gani?
  9. Uingereza yaidhinisha ombi la kampuni ya Todd Boehly kununua Chelsea

    Serikali ya Uingereza imeidhinisha ombi la muungano wa makampuni ya kibiashara unaoongozwa na mmiliki mwenza wa LA Dodgers Todd Boehly. la kutaka kununua klabu ya soka ya Chelsea kwa kima cha pauni bilioni 4.25.

    Klabu hiyo ya London iliuzwa mwezi Machi kabla ya mmiliki Roman Abramovich kuwekewa vikwazo kutokana na uhusiano wake na rais wa Urusi Vladimir Putin.

    Siku ya Jumanne, Ligi Kuu ilisema muungano huo ulipitisha mtihani wa wamiliki na wakurugenzi. Chelsea imekuwa ikifanya kazi chini ya leseni maalum ya serikali ambayo muda wake unaisha tarehe 31 Mei.

    "Jana usiku serikali ya Uingereza ilifikia hatua ambapo tunaweza kutoa leseni inayoruhusu uuzaji wa Chelsea," msemaji wa serikali alisema katika taarifa yake Jumatano.

    Chelsea imekuwa ikihudumu kwa leseni maalum ya serikali ambayo muda wake unamalizika Mei have 31.

    Serikali haitaki Abramovich kupokea mapato yoyote kutokana na mauzo hayo, ambayo badala yake yataingia kwenye akaunti ya benki iliyofungiwa ili kuchangwa kwa mashirika ya misaada.

    Taarifa hiyo iliongeza: "Kufuatia adhabu ya Roman Abramovich, serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha Chelsea imeweza kuendelea kucheza soka.

    Lakini siku zote tumekuwa tukiweka wazi kwamba mustakabali wa muda mrefu wa klabu unaweza kupatikana tu chini ya mmiliki mpya.

    "Kufuatia kazi kubwa, sasa tumeridhika kwamba mapato kamili ya mauzo hayatamnufaisha Roman Abramovich au mtu mwingine yeyote aliyeidhinishwa. Sasa tutaanza mchakato wa kuhakikisha mapato ya mauzo yanatumika kwa sababu za kibinadamu nchini Ukraine, kusaidia wahasiriwa wa vita.

    Soma zaidi:

    • Roman Abramovich: Rabi achunguzwa juu ya uraia wa Ureno
    • Roman Abramovich awekewa vikwazo na Uingereza
    • Roman Abramovich: Kutoka yatima mpaka bilionea wa kuwekewa vikwazo
  10. BBC yaomba radhi baada ya ujumbe wa 'Manchester United ni takataka' kutokea hewani

    BBC imeomba msamaha baada ya ujumbe kuonekana kwenye chaneli ya habari unaosomeka "Manchester United ni takataka".

    Maandishi hayo yalijitokeza kimakosa kwenye vidokezo vya habari vinavyopita chini ya televisheni wakati wa kutoa muendelezo wa habari za tenisi siku ya Jumanne.

    Baadaye asubuhi, mtangazaji Annita Mcveigh aliomba msamaha kwa mashabiki wote wa Manchester United ambao huenda waliudhika.

    Alisema kosa hilo lilitokea kwani mtu alikuwa akijifunza jinsi ya kuweka vidokezo hivyo katika televisheni na alikuwa "akiandika mambo bila mpangilio".

    Ujumbe mwingine ambao ulionekana ulisomeka kwa urahisi: "Hali ya hewa mvua kila mahali."

    Mcveigh aliwaambia watazamaji: "Hapo awali, baadhi yenu wanaweza kuwa wamegundua kitu kisicho cha kawaida kwenye mukhtasari huo ambao unapita chini kabisa ya kioo cha televisheni zikitoa maoni kuhusu Manchester United, na ninatumai kuwa mashabiki wa Manchester United hawakuchukizwa na kitendo hicho.

    "Ngoja nieleze kilichokuwa kikiendelea: nyuma ya pazia, mtu alikuwa akifanya mazoezi ya kujifunza jinsi ya kutumia kipengele hiko na kuweka maandishi, kwa hiyo walikuwa wanaandika mambo ya kubahatisha tu bila ya kumaanisha na maoni hayo yakatokea.

  11. Korea Kaskazini yafyatua makombora saa kadhaa baada Biden kuondoka Asia

    Korea Kaskazini imerusha makombora matatu ya balistiki mapema Jumatano asubuhi ,jeshi la Korea Kusini limesema.

    Mamlaka mjini Seoul imesema makombora hayo yalirushwa angani chini ya saa moja kutoka eneo la Sunan huko Pyongyang.

    Haya yanajiri siku moja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuondoka eneo hilo, kufuatia ziara iliyomwezesha kuahidi kuimarisha hatua ya kudhibiti Korea Kaskazini.

    Korea Kaskazini imekuwa ikifanyia majaribio makombora yake ya balistiki tangu mwanzo wa mwaka huu.

    Japan imethibitisha uzinduzi huo Jumatano lakini ikaafiki kuwa huenda makombora zaidi yalirushwa.

    Waziri wa Ulinzi wa Japan Nobuo Kishi alisema kombora la kwanza lilirushwa takriban kilomita 300 (maili 186) na urefu wa juu wa kilomita 550, wakati la pili, lililofikia urefu wa kilomita 50, lilisafiri karibu kilomita 750.

    Bw Kishi alikosoa uzinduzi huo akisema "haukubaliki" na kuongeza kuwa "utatishia amani, utulivu na usalama wa Japani na jumuiya ya kimataifa".

    Katika mkutano ulioitishwa baada ya kurushwa kwa kombora, Baraza la Usalama la Kitaifa la Korea Kusini liliita jaribio hilo "chokozi kubwa", ofisi ya rais ilisema.

    Maafisa wa Marekani na Korea Kusini walikuwa wameonya hapo awali kwamba Korea Kaskazini ilionekana tayari kwa majaribio mengine ya silaha, pengine wakati wa ziara ya Biden. Wakati wa ziara yake mjini Seoul mwishoni mwa juma,

    Bw Biden na mwenzake wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol walikubali kufanya mazoezi makubwa ya kijeshi na kupeleka mali zaidi za kimkakati za Marekani ikiwa ni lazima kuzuia majaribio ya silaha ya Korea Kaskazini.

    Bw Biden alikuwa amesema Marekani "imejiandaa kwa lolote Korea Kaskazini itafanya."

  12. Afisa wa Afrika Kusini afutwa kazi kwa ajili ya mchungaji mtoro wa Malawi

    Afisa wa Afrika Kusini aliyeidhinisha ukazi wa kudumu kwa mchungaji wa Malawi mwenye utata Shepherd Bushiri amefukuzwa kazi.

    Kufutwa kwake kulifuatia mchakato wa kinidhamu uliochukua takriban mwaka mmoja.

    Ronney Marhule alipatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na kutofuata sheria za uhamiaji kwa kutoa vibali kwa familia ya Bw Bushiri ambavyo "havikustahili", idara ya masuala ya ndani ilisema.

    "Matokeo ya kikao hiki cha kinidhamu yanatupeleka karibu na kuhakikisha kwamba tunakomesha vitendo na maamuzi yasiyo ya kawaida ya maafisa wa masuala ya ndani ndani ya mfumo," Waziri wa Mambo ya Ndani Aaron Motsoaledi amenukuliwa akisema na vyombo vya habari vya ndani.

    Bushiri, anayejiita "nabii", na mkewe Mary wanakabiliwa na mashtaka ya ulaghai nchini Afrika Kusini, lakini walikimbilia Malawi baada ya kupewa dhamana.

    Hati ya kukamatwa ilitolewa na taratibu za kuwarejesha nchini Malawi zinaendelea.

  13. Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye akamatwa

    Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Dkt Kizza Besigye alikamatwa siku ya Jumanne alipokuwa akijaribu kuongoza maandamano katika mji mkuu, Kampala, kupinga gharama kubwa ya maisha.

    Besigye mwenye umri wa miaka 66 aligombea urais dhidi ya Yoweri Museveni mara nne. Aliwahi kuwa daktari wa kibinafsi wa Rais Yoweri Museveni na amekamatwa mara nyingi.

    Dkt Besigye alifika kwenye maandamano ya Jumanne akiwa na megaphone kwenye gari lake na kusimamisha shughuli za biashara katika eneo hilo, kulingana na tovuti ya habari ya Daily Monitor.

    Polisi wa Uganda waliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanamshikilia Dkt Besigye kwa tuhuma za kuchochea ghasia.

    Besigye mwenyewe bado hajatoa kauli yake kuhusiana na suala hilo.

  14. Watoto 19 ni kati ya waliouawa katika shambulio la silaha nchini Marekani

    Watoto wadogo kumi na tisa na watu wazima wawili wamekufa kwa kupigwa risasi katika shule ya msingi kusini mwa Texas.

    Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 18 alifyatua risasi katika Shule ya Msingi ya Robb katika jiji la Uvalde kabla ya kuuawa na vyombo vya sheria, maafisa walisema.

    Wachunguzi wanasema mshukiwa alikuwa amejihami kwa bunduki, bunduki aina ya AR-15 semi-automatic rifle na magazine zenye uwezo wa juu.

    Kijana huyo anashukiwa kumpiga risasi bibi yake mwanzoni mwa shambulio hilo.

    Vyombo vya habari vya nchini vinaripoti kuwa huenda alikuwa mwanafunzi wa shule ya upili katika eneo hilo.

    Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Shule ya Uvalde Consolidated Independent, Pete Arredondo alisema ufyatuaji risasi huo ulianza saa 11:32 saa za ndani siku ya Jumanne, na kwamba wachunguzi wanaamini kuwa mshambuliaji "alitenda peke yake wakati wa uhalifu huu mbaya".

    Gavana wa Texas Greg Abbott alisema mpiga risasi aliacha gari kabla ya kuingia shuleni na kufyatua risasi "kwa kutisha, isiyoeleweka".

    Mmoja wa watu wazima waliouawa alikuwa mwalimu, ambaye ametajwa kwenye vyombo vya habari vya Marekani kama Eva Mireles. Ukurasa wake kwenye tovuti ya wilaya ya shule ulisema ana binti chuoni na alipenda kukimbia na kupanda milima.

    Kulingana na CBS News, mshambuliaji huyo alikuwa amevalia silaha za mwili alipokuwa akitekeleza shambulio hilo.

    Mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 18 ambaye anashukiwa kushambulia duka la mboga huko Buffalo, New York, tarehe 14 Mei pia alikuwa amevalia silaha za mwili na kubeba bunduki ya nusu-otomatiki - zote zinapatikana kwa kununuliwa nchini Marekani.

    Mashambulizi ya silaha yameongoza kusababisha vifo nchini Marekani kuliko ajali za gari kwa mwaka 2020, kulingana na data iliyotolewa na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) mwezi uliopita.

  15. Marekani yafunga mwanya wa malipo ya deni la Urusi

    Marekani inakata njia nyingine ya kifedha kwa Urusi kulipa madeni yake ya kimataifa, hatua ambayo inaweza kuisogeza nchi hiyo karibu na kushindwa.

    Idara ya Hazina ya Marekani ilisema itakomesha msamaha ambao ulikuwa umewaruhusu wenye dhamana wa Marekani kukubali malipo, na hivyo kuimarisha vikwazo vilivyowekwa kutokana na vita vya Ukraine.

    Urusi, ambayo ni tajiri kutokana na usambazaji wake wa mafuta na gesi, ina pesa za kulipa.

    Tayari imeashiria mipango ya kupinga tamko lolote la chaguo-msingi.

    Nchi ina takriban dola bilioni 2 za malipo ambayo yatalipwa hadi mwisho wa mwaka kwenye bondi zake za kimataifa.

    Ingawa sheria mpya zinatumika kwa watu wa Marekani pekee, zitafanya iwe vigumu kwa Urusi kufanya malipo mahali pengine kutokana na jukumu la benki za Marekani katika mfumo wa kifedha wa kimataifa.

    Marekani ilikuwa tayari imeizuia Urusi kutumia benki za Marekani kuhamisha malipo.

    Katika maoni wiki iliyopita, Waziri wa Hazina wa Marekani Janet Yellen alionya msamaha kwa wawekezaji huenda ukaisha. Alisema msamaha huo ulikusudiwa kuruhusu "mabadiliko ya utaratibu".

    Wachambuzi wamesema hawatarajii matokeo makubwa kutokana na kuhamia nje ya Urusi, huku mkuu wa IMF Kristalina Georgieva akisema mnamo Machi kwamba kufichuliwa kwa wamiliki "sio muhimu kimfumo".

    Deni la Urusi lilikuwa tayari limeshushwa hadhi na kuwa "hadhi ya chini" na mashirika makubwa ya ukadiriaji mwezi Machi, hatua ambayo inainyima haki ya kununuliwa na wawekezaji wakuu, hivyo kuwa vigumu kwa Urusi kukusanya fedha katika masoko ya kimataifa.