Vita vya Ukraine: Mwanaharakati wa Urusi aandika barua akiwa jela

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Vladimir Kara-Murza alitangaza kwamba anarudi Moscow mapema mwaka huu, mkewe Evgenia alijua hatari iliyopo mbele yake lakini hakujaribu kumzuia.
Urusi ilikuwa imeivamia Ukraine na kuifanya kuwa hatia kuiita tukio hilo ‘vita’.
Maelfu ya waandamanaji walikuwa wamekamatwa.
Vladimir mwenyewe alikuwa mpinzani wa Rais Vladimir Putin na mkosoaji mkubwa wa ukatili uliofanywa na jeshi lake.
Hata hivyo, mwanaharakati huyo wa upinzani alisisitiza kuwa ataenda Urusi.
Sasa amefungwa na kushtakiwa kwa uhaini na Evgenia hajaruhusiwa kuzungumza naye tangu Aprili.
Lakini katika mfululizo wa barua kutoka Kituo cha 5 cha kizuizini, Vladimir - ambaye mara mbili amekuwa mwathirika wa sumu ya ajabu - anasema hana majuto, kwa sababu "gharama ya ukimya haikubaliki".
Kumpinga Rais Putin ilikuwa hatari hata kabla ya uvamizi huo, lakini tangu wakati huo ukandamizaji wa wapinzani umeongezeka.
Takriban wakosoaji wote mashuhuri wamekamatwa au wameondoka nchini.
Hata hivyo, matibabu ya Vladimir ni makali sana.
Mashtaka yote dhidi yake ni ya kuzungumza dhidi ya vita na Rais Putin na bado wakili wake anasema kuwa anaweza kukaa miaka 24 jela.
"Sote tunaelewa hatari ya shughuli za upinzani nchini Urusi. Lakini sikuweza kukaa kimya nikiangalia kile kinachotokea, kwa sababu ukimya ni aina ya ushirikiano," Vladimir anaelezea katika barua kutoka gereza alipofungwa.
Alihisi hawezi kukaa nje ya nchi pia.
"Sikufikiria nilikuwa na haki ya kuendelea na shughuli zangu kisiasa, kutoa wito kwa wengine kuchukua hatua, wakati mimi niko salama mahali pengine."
'Ningeweza kumuua'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara ya kwanza Evgenia kusikia mume wake amekamatwa ilikuwa kwa njia ya simu kutoka kwa wakili wake, ambaye alikuwa akifuatilia simu ya mwanaharakati huyo kama alivyokuwa akifanya kwa mteja na rafiki yake walipokuwa mjini.
Mnamo Aprili 11, simu ilikuwa imesimama kwenye kituo cha polisi cha Moscow.
Hatimaye Vladimir aliruhusiwa kumpigia simu mke wake, ambaye anaishi Marekani na watoto wao kwa usalama.
Kulikuwa tu na wakati wa kusema: "Usijali!"
Evgenia alitabasamu kwa maagizo hayo ya kipuuzi.
Wanandoa hao walikuwa watoto wa perestroika, walikua wakati wa mwamko wa kidemokrasia wa Urusi baada ya kuanguka kwa Usovieti.
Vladimir kisha alisoma historia huko Cambridge, na wakati huo huo alianza kazi ya siasa za Urusi kama mshauri wa mwanamabadiliko anayeibukia Boris Nemtsov.
Huu ndio muda mrefu zaidi ambao wawili hao wametengana tangu ndoa yao siku ya wapendanao mwaka 2004 na mwanaharakati huyo anasema kutoiona familia yake ndilo jambo gumu zaidi.
"Ninawafikiria kila dakika ya kila siku na siwezi kufikiria kile wanachopitia," anasema.
"Ninampenda na kumchukia mtu huyu kwa uadilifu wake wa ajabu," Evgenia alisema kwenye safari ya hivi karibuni ya London.
"Ilibidi awepo pamoja na wale watu ambao walitoka mitaani na kukamatwa," alisema, akimaanisha Warusi wengi waliowekwa kizuizini kwa kupinga vita.
"Alitaka kuonyesha kwamba hupaswi kuogopa mbele ya uovu huo na ninamheshimu sana na kuvutiwa kwa hilo. Na ningeweza kumuua!"

Hapo awali Vladimir aliwekwa kizuizini kwa kutomtii afisa wa polisi, lakini mara tu akiwa kizuizini mashtaka makubwa yalianza kumiminika.
Mwanaharakati huyo alishutumiwa kwanza kwa "kueneza habari za uwongo" kuhusu jeshi la Urusi na "uongozi wa juu".
Kundi la haki za OVD-Info limerekodi mashtaka zaidi ya 100 chini ya sheria hiyo inayoitwa "habari za uwongo" tangu vita kuanza: diwani wa eneo hilo, Alexei Gorinov, alihukumiwa kifungo cha miaka saba mnamo Julai na mwanaharakati Ilya Yashin atashtakiwa hivi karibuni baada ya kurejelea mauaji ya raia huko Bucha.
Kesi ya Vladimir inatokana na hotuba yake huko Arizona ambapo alisema Urusi ilikuwa ikifanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine kwa mabomu ya cluster katika maeneo ya makazi na "mashambulizi ya hospitali za kina mama kujifungua na shuleni pia".
Hayo yote yamerekodiwa kwa njia huru, lakini kulingana na hati ya mashtaka niliyoona, wachunguzi wa Urusi wanaona taarifa zake kuwa za uwongo kwa sababu wizara ya ulinzi "hairuhusu matumizi ya njia zilizopigwa marufuku ... za kuendesha vita" na inasisitiza kuwa raia wa Ukraine "sio walengwa".
Ukweli ulivyo hauzingatiwi.
Shtaka lingine linatokana na tukio la wafungwa wa kisiasa ambapo mwanaharakati alirejelea kile wachunguzi wanachoita "sera zinazodaiwa kuwa kandamizi" za Urusi.
Kisha mwezi uliopita alishtakiwa kwa uhaini wa serikali.
Mwanaharakati huyo alijibu hilo katika barua yake ya hivi karibuni: "Kremlin inataka kuwaonyesha wapinzani wa Putin kama wasaliti ... , wasaliti wa kweli ni wale wanaoharibu ustawi, sifa, na mustakabali wa nchi yetu kwa ajili ya uwezo wao binafsi, sio wale wanaoisema vibaya".
Mateso ya kisiasa
Shtaka la uhaini linatokana na hotuba tatu nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na moja ambayo Vladimir alisema kuwa nchini Urusi wapinzani wa kisiasa waliteswa.
Wadadisi wanashikilia kuwa alikuwa akizungumza kwa niaba ya Wakfu wa Free Russia wenye makao yake makuu nchini Marekani, ambao umepigwa marufuku nchini Urusi, ambapo "ushauri" au "msaada" wowote kwa shirika la kigeni unaozingatiwa kuwa tishio la usalama sasa unaweza kuchukuliwa kuwa uhaini.
Hakuna siri inayopaswa kufichuliwa.
"Uhaini wa serikali kwa hotuba za umma? Hiyo ni upuuzi tu. Ni mateso tu kwa uhuru wa kujieleza. Kwa maoni. Si kwa uhalifu wowote wa kweli," mwanasheria wa Vladimir, Vadim Prokhorov, anasema kwa simu kutoka Moscow.
Anasema mwanaharakati huyo hakuwa na jambo lolote lenye kumhusisha na wakafu huo.
"Hii ni kesi ya kisiasa. Wanajaribu kuunyanyapaa upinzani wa kawaida kabisa wa Urusi uliostaarabika".

Chanzo cha picha, EVGENIA
Vladimir mwenyewe anaonyesha kwamba mtu wa mwisho aliyeshutumiwa kwa uhaini kwa upinzani wa kisiasa alikuwa mwandishi mshindi wa Tuzo ya Nobel Alexander Solzhenitsyn mwaka wa 1974.
"Ninachoweza kusema ni kwamba nina heshima kuwa katika kampuni hiyo."
Evgenia huona ni ngumu zaidi kusikika mtulivu.
Hii si mara ya kwanza kwa mumewe kuwa na hofu.
Alikaribia kufa, mara mbili, huko Moscow, na sababu ya sumu aliyowekewa haijawahi kutambuliwa.
Alipoanguka kwa mara ya kwanza mnamo 2015 na kuzimia, Evgenia aliambiwa kuwa alikuwa na nafasi ya 5% ya kuishi, lakini alikaidi hilo.
Alimuuguza hadi akarejesha afya, akimsaidia kujifunza kufanya kazi tena, hata kushika kijiko.
Kisha angesisitiza kufanyia kazi kompyuta yake ya mkononi kwenye kochi lao, licha ya kuwa mgonjwa kila baada ya nusu saa.
"Wakati alipoweza kutembea, alifunga virago vyake na kwenda Urusi. Pambano hilo ni kubwa kuliko hofu yake".
Kwa Evgenia, hiyo ina maana ya miaka saba ya kulala na simu yake, akiogopa kupata simu kutoka kwake, au kutoka kwa mtu mwingine kwa sababu hawezi kuzungumza tena."
Aliacha kumshawishi mumewe asiende Moscow zamani: pingamizi lake pekee lilikuwa kukataa kumsaidia kubeba virago vyake.
Lakini kabla ya ziara yake ya mwisho, baada ya vita kuanza, Evgenia aliandamana naye kwanza hadi Ufaransa.“Nilitaka kuifanya safari hiyo kuwa nzuri,” anakumbuka, huku akilia machozi, kutembea kwa muda mrefu katika mitaa ya Paris, wakizungumza bila kikomo.
Mahala pa Nemtsov
Tangu kukamatwa kwa Vladimir, Evgenia ameanza kazi yake ya utetezi: akizungumza kuhusu vita vya Ukraine na ukandamizaji wa kisiasa nchini Urusi, pamoja na kesi ya mumewe.
Siku ya Jumatatu atazindua Mahali pa Boris Nemtsov huko London, matokeo ya kampeni ndefu ya Vladimir kumheshimu mshauri na rafiki yake.
Mwanasiasa huyo mashuhuri wa upinzani alipigwa risasi kando ya Ikulu ya Kremlin mnamo 2015 katika mauaji ya kandarasi ambayo mkandarasi hajawahi kukamatwa.
Barabara ya London iliyopewa jina jipya, kwa kweli ni mzunguko, iko karibu na wajumbe wa wafanyabiashara wa Urusi huko Highgate.

Chanzo cha picha, EVGENIA KARA-MURZA
"Wazo lilikuwa kwamba kila gari linalokuja kwenye lango kubwa litaona bamba la Boris Nemtsov, " Evgenia anaelezea.
Mumewe anatumai Urusi tofauti siku moja itajivunia jina hilo.
Kwa miaka kadhaa, mwanasiasa huyo alifanya kazi kwa karibu na Vladimir kushawishi serikali za Magharibi kuwawekea vikwazo maafisa wakuu wa Urusi kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Mafanikio yao yalikasirisha viongozi wa kisiasa ambao walifurahia kusafiri nje ya nchi na kupeleka pesa huko.
Kuna wakati huko Moscow, Vladimir aliniambia alikuwa amehitimisha kwamba vikwazo hivyo vya "Magnitsky" ndio sababu yeye na Bw Nemtsov walilengwa.
Kusimama kwa mume wake kunamsumbua sana Evgenia, lakini pia kunamfanya aendelee.
"Ninafanya kile ninachohitaji kufanya ili aweze kurejeshwa kwa watoto na vita hivi vya kutisha vikome na utawala huu wa mauaji uweze kufikishwa mahakamani."
Vladimir pia hajakaa kimya.
Barua zake ndefu, zilizoandikwa kwa mkono gerezani zilionyesha imani yake kwamba Urusi haiko chini ya utawala wa kiimla na watu wake sio waaminifu wote wa Putin.
Anaashiria idadi kubwa ya barua anazopata kutoka kwa wafuasi wanaokosoa waziwazi uvamizi wa Ukraine na Kremlin, na kwa wale ambao bado wanapinga hadharani, licha ya hatari.
Anazihimiza nchi za Magharibi kutotenga sehemu hiyo ya jamii ya Kirusi ambayo "inataka mustakabali tofauti wa nchi yetu".
Pia anaonya kuwa vita vya Ukraine havitakoma wakati Vladimir Putin akisalia madarakani.
"Kwa Putin, maelewano ni ishara ya udhaifu na mwaliko wa uchokozi zaidi," anasema.
Vladimir ananiambia anakabiliana na kifungo kwa mchanganyiko wa mazoezi na maombi, vitabu na barua.
Kama mwanahistoria, anapendezwa sana na wapinzani wa enzi ya Usovieti na amekuwa akisoma zaidi kuwahusu anapongojea kesi.















