Marais wa Marekani waliopokea zawadi za kifahari

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ikulu ya White House inaweza kujipata kwenye mzozo juu ya mipango ya Rais Trump kupokea ndege ya kifahari kutoka kwa serikali ya Qatar, yenye thamani ya dola milioni 400 ambayo itakabidhiwa Idara ya Ulinzi ya Marekani ili itumike kama sehemu ya zinazoitwa Air Force One - ndege rasmi za usafiri wa rais.
Wapinzani na wafuasi wake wa Trump, wote wanaungana kupinga zawadi hiyo. Wafuasi wake wa Maga (Make America Great Again) wamesema jambo hilo ni kama "hongo" au ufisadi wa hali ya juu ambao Trump mwenyewe amekuwa akiahidi kuutokomeza.
Gazeti la New York Post, ambalo kwa kawaida hushinikiza ajenda za Maga, liliandika tahariri: "Ndege ya Qatar si zawadi ya bure' - na Trump hapaswi kuikubali kama ilivyo."
Naye Mark Levin, mfuasi wa rais kwenye Fox News, alichapisha maoni kwenye mtandao wa kijamii wa X akiituhumu Qatar kuwa "taifa la kigaidi" na kuandika: "Ndege yao na vitu vingine vyote wanavyonunua kutoka katika nchi yetu, havitokuwa kinga wanayoitafuta."
Lakini usichojua ni kwamba, utawala wa Trump sio wa kwanza Marekani kupokea zawadi za kifahari kutoka kwa viongozi wa nchi za nje.
Marais na zawadi za kifahari walizopokea

Chanzo cha picha, Universal History Archive
Ni mambo yaliyoanza tangu wakati wa mwanzilishi na rais wa kwanza wa Marekani George Washington aliyehudumu kuanzia mwaka1789 hadi 1797.
Mfalme Charles III wa Uhispania alimpa Washington zawadi ya punda wa Kihispania, iliyopewa jina "Royal Gift".
Washington alinuia kutumia punda huyo kuzaliana ili kuboresha ufanisi wa kilimo.
Marquis de Lafayette, afisa wa kijeshi wa Ufaransa ambaye alihudumu katika jeshi la Marekani wakati wa Vita ya Mapinduzi alimpa zawadi ya punda wawili wa kike Jack and Jennys ikiwa ni baadhi tu zile alizopokea.
Abraham Lincoln alikuwa Rais wa 16 wa Marekani, akihudumu kutoka mwaka 1861 hadi kuuawa kwake mnamo 1865.
Abraham Lincoln alikataa kwa uzuri zawadi ya kundi la tembo kutoka kwa Mfalme wa Siam, ambayo kwa sasa inajulikana kama Thailand, mwaka wa 1862. Lakini alichukua "upanga uliotengenezwa kwa nyenzo za thamani na ustadi wa hali ya juu," na picha ya familia ya mfalme huyo na meno mawili ya tembo, kulingana na barua ambayo Lincoln alituma kwa Mfalme Mongkut.

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Ronald Reagan alipokea Jayathu, tembo wa Asia mwenye umri wa miezi 18, kutoka kwa Rais wa Sri Lanka, Jayewardene mwaka wa 1984.
Dwight D. Eisenhower alipokea Dzimbo, tembo wa Kiafrika mwenye uzito wa pauni 440, kutoka maeneo ya Ufaransa magharibi mwa Afrika ya kati mwaka wa 1959.
Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill alimkabidhi Franklin D. Roosevelt mchoro wa Msikiti wa Koutoubia huko Marrakech mnamo mwaka 1943. Mwigizaji wa Hollywood Brad Pitt alinunua kazi hiyo huko New Orleans kwa $2.95 milioni kama zawadi kwa mke wake wa wakati huo Angelina Jolie, ambaye aliiuza muongo mmoja baadaye kwa $ 11.5 milioni.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Richard Nixon alipokea zawadi ya panda wawili wakubwa kutoka China mwaka 1972 kufuatia ziara ya rais wa Marekani katika nchi hiyo ya Kikomunisti. Panda wa kike Ling-Ling na mwenzi wake wa kiume Hsing-Hsing walikabidhiwa Mbuga ya Wanyama ya Kitaifa huko Washington DC.
Mnamo mwaka 1997, Rais Bill Clinton na mkewe Hillary walipokea zawadi ya zulia lililotengenezwa kwa mikono lenye picha zao kama zawadi kutoka kwa kiongozi wa Azerbaijan Heydar Aliyev. Zulia hilo la futi sita kwa tano lilitengenezwa kwa siku moja na timu ya wanawake 12, kulingana na ripoti.
John F. Kennedy alizawadiwa farasi kwa ajili ya Mama wa Taifa Jacqueline na binti yao, Caroline, kutoka kwa Rais wa Pakistani Ayub Khan mwaka wa 1962.
Mnamo Machi 1904, simba kutoka kwa Mfalme wa Ethiopia Menelik II aliwasili kwa Theodore Roosevelt na baadaye akapelekwa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Wanyama.
Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert alimpa Rais George W. Bush zawadi ya baiskeli mwezi Mei 2008 baada ya rais kufichua kuwa miaka ya awali hangeweza kukimbia kwa sababu ya magoti yake kuuma.
Bush pia alipokea mtoto wa mbwa kutoka kwa Rais wa Bulgaria Georgi Parvanov.
Moja ya zawadi za kifahari na zilizozua utata ni kisanduku chenye dhahabu na almasi aliyopewa Benjamin Franklin baada ya ziara yake ya kidiplomasia ya Ufaransa.
Licha ya mjadala kama zawadi hiyo ilichangia ushawishi wa kigeni usiofaa, Franklin alisisitiza kuhifadhi zawadi hiyo. Matokeo yake, ilichangia kupitishwa kwa Kifungu katika Katiba ya Marekani, ambacho kinakataza maafisa wa serikali ya shirikisho kupokea zawadi yoyote kutoka kwa mwakilishi wa nchi ya kigeni bila idhini ya Bunge.
Sheria ya shirikisho inawahitaji maafisa wakuu kufichua zawadi yoyote kutoka kwa serikali ya kigeni yenye thamani ya $480 au zaidi.
Marais wanaruhusiwa kuweka zawadi ili kuonyeshwa kwenye maktaba ya rais, lakini hawawezi kuziweka kwa matumizi ya kibinafsi isipokuwa walipe bei sawa na kitu husika sokoni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama marais wengine, maktaba ya urais ya Barack Obama ina maelfu ya zawadi alizopewa ikiwa ni pamoja na vifungo vya shati vya fedha, mapambo ya Krismasi na kifaa cha kunoa penseli kilichoundwa mfano wa basi la ghorofa mbili.
Marehemu Mfalme wa Saudia Salman pia aliwapa wanandoa hao jozi ya sanamu za farasi zilizopakwa dhahabu na almasi.
Zawadi hizo za kifahari zote zilikabidhiwa Hifadhi ya Taifa ya Marekani kwa mujibu wa sheria za Marekani.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa zawadi ya Trump ya ndege mpya, hakuna chochote ambacho Marekani itatoa kufuatia zawadi hiyo, lakini wachambuzi wengi wanasema, itakuwa ni ujinga kutarajia kwamba familia ya kifalme ya Qatari, itatoa zawadi kubwa bila masharti yoyote.
Katiba ya Marekani inazuia maafisa kukubali "zawadi yoyote, Malipo, Ofisi, au Cheo, cha aina yoyote ile, kutoka kwa Mfalme, Mwanamfalme, au Nchi ya kigeni."
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump aliandika, "Ni MPUMBAVU pekee ndiye ambaye hatokubali zawadi hii kwa niaba ya nchi yetu".
Ikulu ya Marekani imesema, ndege hiyo itatolewa zawadi kwa serikali ya Marekani.











