Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'ICC yalaani vikwazo vya Marekani na kuapa kuendelea 'kutoa haki'
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeahidi kuendeleza majukumu yake ya kisheria baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusaini amri ya kuwawekea vikwazo wafanyakazi wake.
Kwa mujibu wa ICC "inasimama imara" na wafanyakazi wake na itaendelea kutoa "haki na matumaini", ikiongeza kuwa amri hiyo inalenga kuharibu kazi yake "huru na isiyo na upendeleo".
Amri ya Trump inaituhumu ICC kwa "vitendo vya kibadhirifu na visivyo na msingi vinavyolenga Marekani na mshirika wake wa karibu Israel".
Mwaka jana, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, ambapo Israel inakana tuhuma hizo. ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa kwa kamanda wa Hamas.
Katika tamko lake, ilisema: "ICC inalaani utoaji wa amri iliyotolewa na Marekani inayolenga kuwawekea vikwazo maafisa wake na kuingilia uhuru wake na kazi yake isiyokuwa na upendeleo.
"Mahakama inasimama imara" na wafanyakazi wake na itaendelea kutoa "haki na matumaini", kwa mamilioni ya waathiriwa wa ukatili duniani kote, katika hali zote'' iliongeza.
Katika miaka ya hivi karibuni, pia imetoa hati za kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita nchini Ukraine, viongozi wa Taliban kwa "kutesa wasichana na wanawake wa Afghanistan" na kiongozi wa jeshi la Myanmar kwa uhalifu dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Marekani na Israel si wanachama wa mahakama hiyo lakini zaidi ya nchi 120 ni wanachama, ikiwemo Uingereza na mataifa mengi ya Ulaya.
Trump alisaini kipengele hicho wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akitembelea Washington.
Vikwazo hivi vinaweka vizuizi vya kifedha na hati ya kusafiria kwa watu binafsi na familia za wanaosaidia katika uchunguzi wa ICC dhidi ya raia wa Marekani au washirika wake.
Majaji wa mahakama walisema kulikuwa na "sababu za msingi" kwamba Netanyahu, waziri wake wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant, na Mohammed Deif wa Hamas kuwajibika kwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."
Kifo cha Deif katika shambulio la anga la Israel mwaka jana kilithibitishwa na Hamas.
Uholanzi, iliko mahakama hiyo, ilisema inahuzunishwa na amri ya Trump.
"Kazi ya mahakama ni muhimu katika vita dhidi ya kutohukumiwa," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Caspar Veldkamp kupitia mtandao wa X.
Hati hiyo ya White House iliyosambazwa Alhamisi ilishutumu Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu (ICC) kwa kutekeleza hatua iliyokosa maadili na ya aibu kwa kutoa hati za kukamatwa kwa wakati mmoja kiongozi wa Hamas na Israel.
Agizo la utendaji la Trump lilisema kuwa vitendo vya hivi karibuni vya ICC "vimehatarisha raia wa Marekani kwa kuwaweka katika hatari ya "kudhalilishwa, kunyanyaswa na uwezekano wa kukamatwa''.
"Tabia hii mbaya inatishia kuingilia uhuru wa Marekani na kudhoofisha kazi muhimu za usalama wa taifa na sera ya kigeni za serikali ya Marekani na washirika wetu, ikiwemo Israel," agizo lilisema.
Katika chapisho kupitia mtandao wa X siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alisema alipongeza agizo la utendaji la Trump.
Alidai kuwa vitendo vya ICC ni "visivyo vya kimaadili na havina msingi wa kisheria", akishutumu mahakama hiyo kwa kutofanya kazi "kwa kufuata sheria za kimataifa".
Marekani imepinga mara kwa mara mamlaka ya chombo hicho juu ya maafisa au raia wa Marekani, na imeishutumu ICC kwa kuweka vikwazo juu ya haki ya Israe kujilinda, huku ikipuuzilia mbali Iran na makundi yanayopinga Israel.
Huku Marekani ikiwa si mwanachama wa ICC, aliyekuwa afisa mwandamizi wa mashtaka wa kwanza wa mahakama hiyo alionya kuwa vikwazo hivyo vinaweza kuwa na "athari kubwa za kiutekelezaji" kwenye operesheni zake.
"Vikwazo... vina uwezo wa kufungia mali, pamoja na kuzia maafisa wa ICC na familia zao wasiingie nchini Marekani," Zachary Kaufman aliambia BBC World Service.
Katika muhula wake wa kwanza madarakani mwaka 2020, Trump aliweka vikwazo kwa maafisa wa ICC waliokuwa wakichunguza iwapo vikosi vya Marekani vilifanya uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.
Hii ni pamoja na marufuku ya kusafiri na kuzuiwa kwa mali dhidi ya mwendesha mashtaka mkuu wa zamani Fatou Bensouda.
Vikwazo hivyo viliondolewa na utawala wa Rais Joe Biden.
Mwezi uliopita, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipiga kura ya kuwekea vikwazo ICC, lakini mswada huo uliasisiwa katika Seneti.
Katika kukabiliana na jitihada za kile walichokitaja kama majaribio la kupinga mamlaka ya ICC, mataifa tisa - ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na Malaysia - yalianzisha kile yalichokiita 'the Heague group' mwezi uliopita katika jitihada za kutetea mahakama na maamuzi yake.
Amri ya Trump ilisema kwamba "mataifa yote mawili [Marekani na Israel] yanastawi kwa demokrasia yenye wanajeshi ambao wanafuata kikamilifu sheria za vita".
Katika kipindi cha wiki za mwisho madarakani, Rais Biden pia alikosoa hati ya ICC ya kukamatwa kwa Netanyahu, akiitaja hatua hiyo "ya kuchukiza" na kusema hakuna usawa kati ya Israel na Hamas.
Suala la mwendesha mashitaka wa ICC dhidi ya Netanyahu na Gallant ilipata sababu za msingi za kuamini kwamba "kila mmoja anawajibika kwa uhalifu utakaobainika kama wahusika wengine katika kutekeleza vitendo hivyo: uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama silaha ya vita; na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa mauaji, mateso, na vitendo vingine vya kikatili".
Pia ilipata sababu za kuridhisha kwamba "kila mmoja atawajibika kwa makosa ya jinai kama viongozi wa uhalifu wa kivita wa kuelekeza mashambulizi dhidi ya raia kimakusudi".
Kutia saini kwa amri ya Trump hivi karibuni,kunafuatia tangazo lake wakati wa mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri mkuu wa Israel siku ya Jumanne kuhusu mpango wa Marekani "kuichukua" Gaza, kuwapa makazi Wapalestina na kugeuza eneo hilo kuwa "Riviera ya Mashariki ya Kati".
Baada ya viongozi wa Kiarabu na Umoja wa Mataifa kushutumu hatua hiyo, rais wa Marekani alirejelea tena uamuzi huo kwenye jukwaa lake la mtandao wa kijamii siku ya Alhamisi.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Lizzy Masinga