Rishi Sunak:Kizungumkuti katika chama Conservative kilivyotikisa siasa za Uingereza

Na Ahmed Rajab

Mchambuzi

Kwa muda sasa, siasa za Uingereza zimekuwa zikionekana kama za mzaha. Wanasiasa wakuu katika nchi za Ulaya ya Magharibi wamekuwa wakiviangalia vituko vya siasa za Uingereza kwa mshangao mkubwa.

Wakati huo huo, viongozi wakuu wa chama kinachotawala cha Conservative wamekuwa vikaragosi — vichekesho katika baadhi ya nchi za Ulaya, hususan Ufaransa na Ujerumani. Wamekuwa wanaonekana na wenzao kuwa ni watu wasiojua wanataka nini au wanafanya nini.

Demokrasia nayo imepungua katika Uingereza, nchi inayojigamba kwamba ndiyo “mama wa demokrasia” katika dunia ya leo. Tumeshuhudia mawaziri wakuu watatu Boris Johnson, Theresa May na Liz Truss wakichaguliwa na wanachama wa chama chao tu cha Conservative.

Jumatatu ya tarehe 24 Oktoba tumeshuhudia tukio la ajabu kushinda maajabu yote ya kizungumkuti cha siasa za Uingereza — waziri wa zamani wa fedha Rishi Sunak, alichaguliwa na wabunge wa chama chake awe kiongozi wa chama na Waziri Mkuu bila ya kupigiwa kura hata moja.

Hapakuwa na haja kwa sababu Sunak aliungwa mkono na wabunge zaidi ya mia moja na hakukabiliwa na mpinzani. Kufikia Jumatatu, siku tatu baada ya Truss kujiuzulu, wabunge wawili wa chama chake — Waziri Mkuu wa zamani Johnson na Penny Mordaunt — walioonesha nia ya kupambana na Sunak.

Wakati huo Sunak alikwishatangaza kwamba atapigania tena uongozi wa chama na uwaziri mkuu. Mara yake ya kwanza kufanya hivyo, Sunak alibwagwa na Truss katika hatua ya mwisho wanachama wa chama chao walipotakiwa wamchague kiongozi wao.

Ingawa Sunak akiongoza wagombea hao walipopigiwa kura na wabunge walipotakiwa wanachama wachague, walimchagua Truss.

Ilivoonesha ni kwamba kilichomponza Sunak ni rangi ya ngozi yake. Ingawa amezaliwa Uingereza, Sunak ana asili ya India walikozaliwa babu na bibi yake. Baba yake amezaliwa Kenya na mama yake Tanganyika.

Chama hicho kiliundwa kutoka chama cha Tory. Chama cha conservative kinajulikana mitaani Uingereza kwa jina hilo hilo la utani, la Tory, jina ambalo katika karne ya 19 lilikuwa na maana ya matusi.

Ingawa chama hicho cha Conservative kilikuwa na nguvu sana karne ya 19 hadi ya 20 ambapo kilikuwa kikiiongoza serikali ya Uingereza wakati Uingereza lilipokuwa taifa lenye nguvu zaidi dunia na lililokuwa likimiliki makoloni chungi nzima hasa katikamabara ya Afrika na Eshia. 

Hii leo, hadhi ya chama hicho, pamoja na siasa za Uingereza kwa jumla, imeporomoka. Kwa hakika, hadhi hiyo ilianza kuporomoka mwaka 2016 wakati wa kampeni ya Brexit ya Uingereza kujitoa kutoka Muungano wa Ulaya (European Union).

Kampeni hiyo ilikuwa ni ya kura ya maoni ambayo hatimaye iliiwezesha Uingereza ijitoe kutoka Muungano wa EU.

Aliyeiongoza kampeni hiyo alikuwa Boris Johnson, mwanasiasa mshupavu wa chama cha Conservative. Matokeo ya kura ya maoni yaliupa ushindi upande wa Johnson. Waingereza kweli wakitaka nchi yao iondoke kutoka EU.

Matokeo yalipotangazwa hata Johnson mwenyewe hakuamini kwamba upande wake ulishinda. Alianzisha kampeni ya Brexit kama mchezo, kama mzaha.

Hapo ndipo siasa za Uingereza zilipoanza kugeuka na kuwa za mzaha. Licha ya kuwa Waziri

Mkuu Johnson naye akagueka na kuwa mchekeshaji mkubwa katika jukwaa la siasa za Uingereza. Johnson na wenzake walizicheza siasa mithili ya watoto wa skuli wanavyocheza michezo yao.

Chama cha Conservative, ambacho ni kikongwe Uingereza kiliasisiwa mwaka 1834. Na ni chama kilichoongoza serikali nchini Uingereza kwa muda mrefu zaidi kushinda chama chochote chengine.

Sera za chama hicho ni za kimuhafidhina. Hilo halina shaka hata kidogo. Lakini uhafidhina wake si wa aina moja. Ni uhafidhina wa rangi moja ya buluu lakini wenye migawanyiko ya mapande kwa mapande.

Chama hiki kinachojisifu kwamba ni chama cha Benjamin Disraeli, Waziri Mkuu wa mwanzo na hadi sasa wa pekee aliyekuwa Yahudi nchini Uingereza, hakikuwahi kukumbwa na misukosuko kama hii iliyokigubika siku hizi.

Disraeli, aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka sita (1874-1880), alitwikwa jukumu muhimu la kuhakikisha kwamba chama Conservative ni cha kileo, kisichopitwa na wakati. 

Miongoni mwa hatua za mwanzo alizozichukuwa Disraeli zilikuwa zile zilizokifanya chama hicho kitambulike kuwa ni chama cha utawala wa Uingereza iliyokuwa na himaya na makoloni katika sehemu mbalimbali za dunia.

Kadhalika Disraeli aliifanya Uingereza iwe na nguvu za kijeshi za kuweza kujitanua na kujinyakulia makoloni na himaya zaidi.

Hatua zote hizo mbili ziliwavutia wapiga kura wa Uingereza.

Ni yeye Disraeli aliyezifafanua sera na misingi ya itikadi ya chama hicho. Ingawa itikadi kuu ya chama hicho ni uhafidhina lakini, kwa hakika, hakuna uhafidhina wa aina moja ndani ya chama. Mna mikondo tafauti ya uhafidhina na mapande tafauti ya kiitikadi. 

Kwa mfano, ndani ya chama hicho mna pande la “uhafidhina wa taifa moja” ambao pia unajulikana kama “utaifa mmoja” au “demokrasia ya Kitory”; kuna pande lenye kuhubiri itikadi ya sera za Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher na mna pande la “uhafidhina asilia” — ambao ni falsafa ya kisiasa na ya kijamii yenye kujikita juu ya misingi ya maadili mema, uhusiano mzuri wa familia, ada na desturi za kijamii za Uingereza.

Siasa za rangi na jinsia

Watu wengi wanajiuliza kwa nini chama cha Conservative kikawa mbele ya chama cha Leba katika upande wa kuwawezesha wanasiasa wasio na asili ya kizungu?

Nafikiri jibu ni kwamba vyama hivyo vimekuwa vikigeukia pande tafauti. Chama cha Leba kimekuwa kikitilia sana kuwawezesha wanawake, zaidi wa kizungu, katika ngazi tafauti za chama hicho. Chama cha Conservative kwa upande wake kimekuwa kikitilia mkazo kuwawezesha wanasiasa wasio wa kizungu. 

Ndio maana tunaona kwamba katika serikali ya chama cha Conservative kuna mawaziri wengi wasio wazungu. Mtindo huu ulianza tangu David Cameroon alipokuwa Waziri Mkuu hadi sasa. 

Katika serikali iliyodumu siku 44 tu ya Liz Truss tuliziona nyadhifa zote tatu kubwa serikalini zikishikwa na watu wasio wazungu — wizara ya fedha, wizara ya mambo ya nje na wizara ya mambo ya ndani.

Hali hiyo haina maana kwamba mawaziei hao wasio wazungu ni watu wataowasaidia wenzao wa rangi moja na wao. Ushahidi unaonesha kwamba mawaziri hao wamekuwa wagumu zaidi katika kuwa na sera laini zitazowasaidia wahamiaji kutoka Afrika, kwa mfano, kwingineko.

Jambo jingine tunalojifunza kutokana na kadhia hii iliyomuangusha Truss na kumpandisha juu Sunak ni hili: kwamba masoko ya fedha hayajali kiongozi wa taifa ni wa rangi gani.

Katika mfumo uliopo wa kibepari masoko ya fedha yanajali sera na sera tu, hasa zile zinazowapatia faida kubwa mabepari. Ndio maana thamani ya sarafu ya pauni ilianguka wakati wa kipindi kifupi cha Truss na sasa imeanza kupanda wakati wa Sunak.

Masoko ya fedha yaliutia adabu uchumi wa Uingereza wakati wa sera mbovu za kiuchumi na za kifedha za Truss na sasa yanasaidia kuunyanyua uchumi huohuo kwa sababu ya sera bora au muelekeo wa sera bora za Sunak.