Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, shinikizo la Marekani linaweza kuleta mapatano ya amani kati ya Israel na Hamas huko Gaza?
Na Hugo Bachega ,
Mwandishi wa habari wa Mashariki ya Kati, Jerusalem
Maelewano kati ya Israel na kundi la Wapalestina la Hamas huko Gaza hayatakuwa rahisi kamwe. Wiki za mazungumzo zimeshindwa kuleta makubaliano. Lakini shinikizo la kimataifa linaongezeka.
Labda ishara kubwa zaidi ni utawala wa Biden kumtuma William Burns, mkuu wa CIA, kwa duru ya hivi karibuni ya mazungumzo huko Cairo.
Hamas, hadharani , imeshikilia matakwa yake ya awali ya usitishaji wa kudumu wa vita , kuwaondoa kabisa wanajeshi wa Israel na kuwarejesha Wapalestina waliokimbia makazi yao katika maeneo ya kaskazini mwa eneo hilo bila vikwazo.
Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasisitiza kuwa Israel itaendelea na mapigano hadi Hamas iangamizwe na mateka wanaoshikiliwa na kundi hilo waachiliwe.
"Kuna shinikizo kubwa zaidi kutoka Marekani kwa Israel, na kwa Misri na Qatar kuweka shinikizo kwa Hamas. Hilo ni dhahiri," anasema Gershon Baskin, ambaye alisaidia kufanya mazungumzo na Hamas kwa ajili ya kuachiliwa kwa mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit mwaka 2011.
"Ukweli kwamba mkuu wa CIA alijitokeza, ambayo itahitaji wapatanishi wote wa ngazi ya juu kuwa huko ni dalili ya kuongezeka kwa shinikizo la Marekani."
Lakini hiyo haimaanishi kuwa makubaliano yanakaribia kuafikiwa.
Maafisa wa Israel wameonyesha nia ya kufanya makubaliano huku kukiwa na hali ya kufadhaika kati ya washirika wakuu wa nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na Marekani. Mapema wiki hii, waziri wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, alipendekeza kuwa sasa ulikuwa wakati mwafaka wa mapatano.
Makubaliano yoyote yanatarajiwa kushuhudia kuachiliwa kwa baadhi ya mateka waliotekwa katika mashambulizi ya Hamas kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa katika jela za Israel, ambayo ilikuwa msingi wa mapatano yaliyosababisha kusitishwa kwa mapigano kwa muda mwezi Novemba. Kwa mujibu wa mamlaka ya Israel, watu 133 wamesalia mateka huko Gaza, ingawa takriban 30 tayari wamethibitishwa kufariki.
Chini ya pendekezo la hivi punde la Marekani, awamu ya awali ya usitishaji vita wa wiki sita itaifanya Hamas kuwaachilia mateka 40 ambao wako hai, huku kipaumbele kikipewa mateka wa kike wakiwemo wanajeshi, wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na wale walio na matatizo ya kiafya.
Israel nayo itawaachilia huru Wapalestina 700, wakiwemo takriban 100 wanaotumikia kifungo cha maisha jela kwa kuwaua Waisraeli, jambo ambalo limeonekana kuwa na utata nchini Israel hapo awali.
Lakini Hamas imeripotiwa kuwaambia wapatanishi kuwa haiwashikilii watu 40 katika kundi hili, na kuongeza wasi wasi kwamba mateka wengi zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali wamekufa au kwamba wanaweza kuwa mikononi mwa makundi mengine yenye silaha, kama vile Palestina Islamic Jihad.
Nchini Israel, fursa ya Bw Netanyahu ya kufanya maamuzi inazidi kubawana na imepunguzwa na shinikizo kutoka sehemu mbalimbali za jamii na siasa. Wakati wananchi wengi wa Israel wanasalia kuunga mkono vita hivyo, kuna wito unaozidi kumtaka aafikie makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka hao.
Familia hizo zimefanya maandamano makubwa, zikimshutumu waziri mkuu kwa kutofanya urejeshaji wa mateka kuwa kipaumbele na kujali zaidi maisha yake ya baadaye kisiasa. Wito wa kumtaka Bw Netanyahu ajiuzulu pia unaongezeka.
Mgawanyiko umeongezeka ndani ya muungano unaoongoza wa Bw Netanyahu, ambao unajumuisha washirika wa siasa kali za mrengo wa kulia, ambao wanakataa makubaliano na Hamas na kusisitiza kwamba vita lazima viendelee.
Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich alimwambia waziri mkuu kwamba kuongezeka kwa shinikizo kwa Hamas ndiyo njia pekee ya kuwarudisha mateka na kuliangamiza kundi hilo, huku Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben Gvir akitishia kumwangusha Bw Netanyahu mwenyewe ikiwa hataendelea na mashambulizi yaliyoahidiwa sana katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza.
Maafisa wa Israel wanasisitiza kuwa ni muhimu kuingia Rafah, ambako, wanasema, Hamas ina brigedi nne zinazofanya kazi huko na viongozi wake wakuu huenda wanajificha katika mji huo.
Lakini karibu kila mtu nje ya Israel anapinga mashambulizi katika mji huo, ambapo Wapalestina wapatao milioni 1.5 wanaishi kwenye mahema, makazi duni na kambi zilizojaa watu, kutokana na wasiwasi wa athari mbaya ambayo inaweza kuwa nayo kwa raia.
Katika kile kinachoweza kuwa jaribio la kukabiliana na ukosoaji wa ndani, siku ya Jumatatu, Bw Netanyahu alisema tarehe tayari imepangwa kwa ajili ya operesheni ya Rafah, bila kutoa maelezo zaidi."Kuna uasi unaoendelea sasa hivi serikalini, na ndani ya [chama cha Bw Netanyahu] Likud, dhidi ya Netanyahu kufanya aina yoyote ya makubaliano ambayo hawafikirii yanafaa kufanywa," Bw Baskin alisema.
"Netanyahu hayupo huru tena . Yeye mwenyewe ni mateka ndani ya serikali yake."
Kwa upande wake Hamas bado haijatoa jibu rasmi kwa pendekezo la hivi punde, lakini ilisema kwamba ingawa ina nia ya makubaliano "ambayo yanakomesha uchokozi kwa watu wetu", pendekezo hilo halikukidhi matakwa yake.
"Msimamo wa Israel haujabadilika ," kundi hilo lilisema katika taarifa.
Ikulu ya White House ilielezea majibu ya kundi hilo kama "yasiyotia moyo".
Uamuzi wa mwisho pengine utatolewa na Yahya Sinwar, kiongozi wa Hamas huko Gaza ambaye anadhaniwa kujificha kwenye mahandaki ya chini ya ardhi akizungukwa na walinzi na mateka. Lakini mawasiliano naye ni magumu na inasemekana kuhusisha watu kadhaa na kudumu kwa siku kadhaa.
Kundi hilo, Bw Baskin alisema, pia lilikuwa likitaka usemi zaidi kuhusu ni wapi wafungwa wa Kipalestina wataachiliwa na kwamba halitakubali yeyote kati yao kuhamishwa hadi nchi nyingine, masuala ambayo yanaweza kuleta vikwazo katika mazungumzo.
Hamas pia inaamini kuwa bila ya kuwa na hakikisho la usitishaji wa kudumu wa vita , Israel itaendelea kulishambulia kundi hilo mara tu mateka hao watakapoachiliwa.
Uongozi wake umeshuhudia kuongezeka kwa ukosoaji wa kimataifa kwa Israeli na wanaweza kuamini kuwa wana muda wa kupata makubaliano, licha ya mahitaji makubwa na ya haraka ya raia wa Gaza wanaoteseka.
Vita vya Gaza, jibu la Israel kwa mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba ambayo yaliua takriban watu 1,200, vimeua zaidi ya Wapalestina 33,000, kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas, kuharibu sehemu kubwa za eneo hilo, na kuwaacha wengi kwenye hatari ya njaa.
"Kutokana na tajriba yangu katika kushughulika na mambo haya, matatizo makubwa ni iwapo mtoa maamuzi mkuu wa pande zote mbili yuko tayari kwa makubaliano. Hilo haliko wazi," Bw Baskin alisema.
"Si wazi kwamba Netanyahu yuko tayari kwa makubaliano, haiko wazi kwamba [kiongozi wa kisiasa wa Hamas huko Gaza Yahya] Sinwar yuko tayari kwa makubaliano. Lakini watakapofika katika hali hiyo watapata kuafikia uamuzi unaokubalika na pande zote."
Labda haishangazi,kwamba msemaji wa Hamas alihoji matamshi ya Bw Netanyahu kuhusu kupanga tarehe ya shambulio dhidi ya Rafah, akisema ilizua maswali kuhusu madhumuni ya kuanza tena mazungumzo.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah