Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kivuko cha Rafah ni nini na kwa nini ndicho kivuko pekee 'kinachoipa uhai' Gaza?
Raia wa kwanza kutoka Ukanda wa Gaza wamevuka mpaka wa Rafah na kuingia Misri tangu kuanza kwa vita vya Israel na Gaza.
Makumi ya Wapalestina waliojeruhiwa vibaya walichukuliwa kwa ambulensi na mamia ya wamiliki wa pasi za kigeni walivuka Jumatano.
Awali Misri ilisema itaruhusu zaidi ya majeruhi 80 na zaidi ya raia 500 wa kigeni na wa nchi mbili kwa jumla, katika makubaliano ambayo inasemekana kusimamiwa na Qatar.
Huu ni uhamishaji wa kwanza wa aina hiyo kufanyika tangu mzozo huo uanze zaidi ya wiki tatu zilizopita. Haijabainika mpaka huo utasalia wazi kwa muda gani.
Tayari imefunguliwa kwa zaidi ya siku 10 kuruhusu misaada kuingia Gaza. Hadi sasa, zaidi ya malori 200 yamevuka mpaka, lakini mengi zaidi yanahitajika.
Kivuko cha Rafah ni nini?
Ni sehemu ya kusini ya kutoka Gaza na inapakana na rasi ya Sinai ya Misri.
Kuna vivuko vingine viwili tu vya mpaka kutoka na kuingia Ukanda wa Gaza - Erez, kivuko cha watu na Israeli kaskazini mwa Gaza, na Kerem Shalom, makutano ya bidhaa za kibiashara pekee na Israeli kusini mwa Gaza. Zote mbili zimefungwa.
Kwa nini ni muhimu?
Watu wenye silaha kutoka kundi la wapiganaji wa Kipalestina Hamas, linaloongoza Gaza, walishambulia kivuko cha Erez tarehe 7 Oktoba wakati wa shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel na kuua zaidi ya watu 1,300.
Siku kadhaa baadaye, Israeli ilitangaza Erez na Kerem Shalom kufungwa hadi ilani nyingine, na kuacha mpaka wa Rafah kama njia pekee ya kuingia na kutoka kwa Ukanda kwa watu.
Rafah sasa pia ndio kivuko pekee cha misaada ya kibinadamu.
Wiki iliyopita, wizara ya mambo ya nje ya Misri ilisema inaelekeza safari za ndege za misaada ya kimataifa kuelekea Gaza hadi uwanja wa ndege wa El-Arish kaskazini mwa Sinai, na makumi ya malori ya kubeba mafuta na bidhaa za kibinadamu yameegeshwa upande wa Misri wa kivuko cha Rafah.
Ni nini kinachoendelea katika kivuko hicho?
Taarifa zinazokinzana zimesambaa kuhusu hali ya Rafah. Hamas na Misri zinadhibiti ni nani anaweza kupita, lakini operesheni zimetatizika tangu Israel ilipoanza kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Gaza kama hatua ya kulipiza kisasi shambulio la Hamas.
Vyombo vya habari vya Misri vilisema kivuko hicho kilifungwa kufuatia mashambulizi matatu ya Israel tarehe 9 na 10 Oktoba, ambayo ilisema yalisababisha majeruhi katika pande za mpaka wa Misri na Palestina.
Tarehe 12 Oktoba, serikali ya Misri iliitaka Israel kusitisha mashambulizi karibu na kivuko cha mpaka cha Rafah ili iweze kutumika kama "msaada wa kuokoa maisha" kwa watu wa Gaza, na iliweka wazi kwamba haitafungua njia hiyo hadi kuwe na hakikisho la usalama. ya wafanyakazi wake.
Nchi za Magharibi pia zinashiriki kujaribu kupata njia salama kupitia Rafah kwa wamiliki wa pasipoti za kigeni huko Gaza na misaada ya kibinadamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly na mwenzake wa Marekani, Antony Blinken, wote walisema wanafanya kazi na Israel, Misri na "sauti nyingine kuu za kisiasa katika kanda" kufungua tena kivuko hicho.
Wiki iliyopita, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema raia wa Marekani walikuwa wakiambiwa waelekee Rafah kwa sababu "huenda kukawa na arifa fupi sana ikiwa kivuko kitafunguliwa na kinaweza kufunguliwa kwa muda mfupi tu".
Siku ya Jumatatu, umati wa watu ulikusanyika Rafah kufuatia ripoti kwamba kivuko hicho kitafunguliwa tena kwa muda wakati vita vitakapositishwa kwa muda mfupi, lakini Israeli na Hamas walikanusha ripoti hiyo.
Kwa nini vivuko vimefungwa?
Israel na Misri zimezuia usafirishaji wa bidhaa na watu kuingia na kutoka Gaza tangu Hamas ilipochukua udhibiti wa eneo hilo mwaka 2007. Nchi hizo mbili zinasema kuwa kizuizi chao kinahitajika kwa sababu za kiusalama.
Kama sehemu ya majibu yake kwa shambulio baya la Hamas, waziri wa ulinzi wa Israel aliamuru "kuzingirwa kabisa" kwa Gaza tarehe 9 Oktoba, na kuongeza: "Hakutakuwa na umeme, chakula, mafuta, kila kitu kimefungwa."
Na ingawa Misri inaonekana kuwa tayari kufungua tena kivuko cha Rafah ili kuruhusu wenye hati za kusafiria kutoka nje na misaada ya kibinadamu kuingia, inahofia wimbi kubwa la wakimbizi wa Kipalestina wanaokimbia vita.
Rais wa Misri alionya tarehe 12 Oktoba kwamba kuhama kutoka Gaza kunahatarisha "kukomesha" kadhia ya Palestina na kuwataka Wapalestina "kusalia imara katika ardhi yao".
Pia ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa wanamgambo wa Kiislamu kuingia nchini humo, baada ya kukabiliwa na uasi wa kijihadi huko Sinai kwa takriban muongo mmoja.
Je, kivuko cha Rafah kinatumikaje kwa kawaida?
Si rahisi kwa Wapalestina kuondoka Gaza kupitia Rafah. Wapalestina wanaotaka kutumia kivuko hicho lazima wajiandikishe kwa mamlaka ya eneo la Palestina wiki mbili hadi nne kabla na wanaweza kukataliwa na mamlaka ya Palestina au Misri bila onyo au maelezo machache.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mnamo Agosti 2023, mamlaka ya Misri iliruhusu watu 19,608 kutoka Gaza na kuwanyima watu 314 kuingia.