Waridi wa BBC: ‘Wanawake wengi niliokutana nao wanatamani sana ndoa, ikilinganishwa na wanaume’

Chanzo cha picha, Mariam Mbano
- Author, Martha Saranga
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Muda wa kusoma: Dakika 4
‘‘Unakuta watu wanakutafuta, mwingine anakulilia yupo mpweke anaumia, anataka umsaidie kupata mwenza,’’anaeleza Mariam Mbano.
Mariam Mbano 37, mwenyeji wa Dar Es Salaam ni wakili, mwandishi wa vitabu na Mkurugenzi na mwanzilishi wa Mamz Relationship Hub, taasisi inayojishughulisha na mahusiano, familia na kuunganisha wenza.
Kupitia taaluma ya sheria alipata msukumo wa kuwasaidia wanawake kwa kuwapatia elimu ya sheria baada ya kukutana na baadhi ya wanawake wanaokumbwa na changamoto mbalimbali zinazochangiwa na kutojua sheria.
‘’Mtu anapokufuata kuzungumza na wewe maana yake mtu huyu ana mzigo anahitaji sehemu anayoweza kuupunguza au kuutua kwa vile amekuamini,’’anasema Mariam.
Moja ya kazi ambazo Mariam na taasisi yake wamekuwa wakifanya ni pamoja na kutafutia watu wenza.
‘’Mimi huchukulia suala la faragha na kutunza siri kuwa ni jambo la utu,’’anaeleza Bi Maria.
Katika kuunganisha wenza anasema alikutana na wanawake wengi wenye uhitaji wa wenza ukilinganisha na wanaume waliokuwa wakijitokeza
‘’Lakini pia wanawake wengi niliokutana nao wanatamani sana ndoa, wanashida sana na ndoa”
‘’Unakuta watu wanakutafuta, mwingine anakulilia yuko single anaumia umsaidie kupata mwenza nikaona kuna kila haja ya kujiimarisha upya na watendaji wangu ili kumudu uhitaji wa jamii,'' anaeleza Mariam.

Chanzo cha picha, Mariam Mbano
Kwanini aliamua kutoa huduma ya kuunganisha wenza?
Mariam Mbano anasema miongoni mwa mambo anayokutana nayo sana ni wanawake na wanaume kutafuta watu wa kuingia nao katika ndoa.
‘‘Lakini watu hawa hukutana na watu ambao hawana uhitaji kama walionao wao, hiyo kwangu ni fursa,'' anaeleza Mariam.
Je, huzingatia mambo gani?

Chanzo cha picha, Mariam Mbano
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mimi kuwa mwanasheria imenifanya nijue mitego mingi ambayo unaweza kuepuka na hata kutoingia katika lawama.
‘’Huwa ninaandaa mkataba na mchakato rasmi ambao lazima muhitaji apitie kabla ya kuunganishwa na mwenza.’’
''Pia kuna utaratibu wa kumchunguza mtu binafsi ambapo atahojiwa ili kufahamu historia na taarifa muhimu kumuhusu,’’anasema Mariam.
Ninatumia wanasheria wenzangu ambao wananizunguka kuhakikisha ninafuata utaratibu na ninazingatia weledi katika kuunganisha watu.
Hatahivyo uhitaji mkubwa wa watu wanaotafuta wenza ulimfanya asitishe kwa muda.
Anasema kuwa ataendelea tena kutoa huduma hiyo kuanzia mwakani mara baada ya kujiimarisha.
’Unapomgusa mwanamke umemgusa mtoto na hata kijana’’
Baada ya kusitisha kwa muda kutoa huduma hii ambayo anatarajia kuendelea nayo mwakani, Mariam ambaye pia ni mwandishi wa vitabu anasema ‘’Unapomgusa mwanamke umemgusa mtoto na hata kijana’’
Sasa amejikita zaidi katika kusaidia wanawake katika masuala ya kisheria ikiwemo kutoa msaada wa kisheria kwa watu ambao wana changamoto za ndoa ambazo zinahitaji kushauriwa kisheria.
‘’Kuanzia kwenye kazi yangu ya kisheria hadi kwenye shughuli za kijami ninakutana na watu tofauti’’
Mariam ambaye ana wafuasi wengi mtandaoni anasema kwa kutofahamu sheria watu wengi hukutana na changamoto nyingi na kushindwa kujikwamua.
Wapo watu kwa kutokufahamu sheria wamejikuta wakiingia katika matatizo makubwa hata kupoteza mali walizochuma kwa muda mrefu.

Chanzo cha picha, Mariam Mbano
Je, anawasaidiaje?
‘’Huwa ninaandaa makongamano na majukwaa ya mitandao ya kijami ambapo ninashirikiana na wenzangu kutoa elimu ya sheria kupitia mada mbalimbali.
Kupitia taasisi hiyo ameweza kuandika kitabu cha Kovu la Moyo ambacho kimelenga kuwasaidia watu wanaotarajia kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi au ndoa au hata wale ambao wamejeruhiwa katika mahusiano yao.
‘Wakati nashughulikia changamoto kwa upande wa sheria niligundua kwamba wenzi kuachana, kutelekeza watoto ama kugombania mali ni mambo ambayo mtasuluhisha kisheria lakini nilijiuliza vipi kuhusu hali ya afya yake ya kiakili?’
‘Je makosa aliyofanya anajifunza vipi asirudie? hapo ndipo nilianza kuandika vitabu na kuhamasisha usomaji wenye tija.’

Chanzo cha picha, Mariam mbano
Mara nyingi nikiwa na wazo la kufanya kitu humshirikisha mume wangu, ambaye mara zote amekuwa chachu ya mimi kufanya vizuri katika usimamizi wa shughuli zangu.
Anasema kazi za kisheria zimemsogeza karibu na jamii. Kuweza kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu kuibua mada na hata kuunganisha watu.
Anasema wakati mwingine hata pasipo kujua watumiaji wa mitandao wamekuwa wakimpendekeza kwenye taasisi mbalimbali zinazotambua wanawake wenye mchango chanya katika jamii.
‘‘Ninajiona mbali miaka kadhaa ijayo. Ninatamani kuihudumia jamii na kuwa na mchango chanya.’'
Imehaririwa na Seif Abdalla












