Nini kifanywe kuliokoa jahazi la serikali ya ubia Zanzibar?

Chanzo cha picha, Ikulu Zanzibar
Na Ahmed Rajab
Hali ya kisiasa visiwani Zanzibar si shuwari hivyo. Chini kwa chini kunafukuta. Kuna dalili kadhaa zenye kuonyesha kwamba jahazi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) linakwenda mrama na pasipochukuliwa hatua za haraka litazama.
Hiyo ndiyo tathmini ya wachambuzi na wadadisi wa siasa za Zanzibar. Tathmini hiyo imewatia wasiwasi baadhi ya viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) -Taifa.
Duru zinaarifu kwamba Chama cha ACT Wazalendo, mshiriki wa CCM katika SUK, kinasubiri jawabu ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, kwa ombi lake la kukutana naye kuijadili SUK.
Kuasisiwa kwa serikali ya ubia

Chanzo cha picha, Michuzi Blog
Mfumo wa SUK — wa serikali ya ubia baina ya vyama vikuu viwili visiwani humo — ulianza kutumika tangu baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.
Serikali hiyo iliundwa kufuatia kura ya maoni iliyopigwa Julai 31, 2010, ambapo asilimia 66.37 ya wapiga kura walipendelea mfumo huo wa utawala.
Wakati huo viongozi wa vyama vikuu viwili nchini humo walikuwa Rais Amani Abeid Karume, aliyekuwa pia makamu mwenyekiti wa CCM, na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha wakati huo Civic United Front (CUF).
Viongozi hao wawili ndio waliokaa na wasaidizi wao wakuu wakaitafakari hali ya Zanzibar na wakaibuka na dhana ya SUKI. Waliona kwamba baada ya miongo kadhaa ya misuguano ya kisiasa iliyozusha mfarakano na mpasuko mkubwa katika jamii, mateso na mauaji, palikuwa na haja ya dharura ya kuliunganisha taifa.
Viongozi hao walitambua kwamba nchi yao haitoweza kuendelea bila ya kuwa na utulivu na huo utulivu hauwezi kupatikana bila ya wananchi kuridhiana na kuamua kuwa wamoja.
Wananchi walikubaliana na zingatio hilo na ndo wakapiga kura kwa wingi kuunga mkono pendekezo la kuwa na SUKI.
SUK ya kwanza iliundwa baada ya uchaguzi wa Oktoba 2010 ambapo Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea wa urais wa CUF kuridhia kwamba ushindi apewe Dkt. Ali Mohamed Shein wa CCM.
Chama cha CUF kikampendekeza Maalim Seif awe Makamu wa Kwanza wa Rais. Kwa muda wa miaka mitano mfumo huo mpya wa utawala ulifanya kazi kwa kuridhisha licha ya udhaifu na dosari zake.
Moja ya mambo yaliyokuwa yakiwafurahisha wananchi ilikuwa kuwaona wajumbe wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi walivyokuwa wakakamavu walipokuwa wakichangia katika mijadala ya Baraza hilo.
Kufutwa uchaguzi 2015

Chanzo cha picha, ZEC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfumo wa SUK ulifikwa na mtihani mkubwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Uchaguzi huo ulifutwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha Salum Jecha ilipoonekana kwamba Maalim Seif anaibuka mshindi katika mchuano wa urais. Kitendo cha Jecha kilikuwa kitendo cha uvunjwaji wa Katiba ya nchi.
Matokeo yake ni kwamba CUF iliususia uchaguzi wa marudio na hivyo kugoma kushiriki katika SUKI.
Huku nyuma, kulizuka mvutano ndani ya CUF baina ya Maalim Seif na Profesa Ibrahim Lipumba aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CUF. Lipumba alikuwa amejiuzulu uwenyekiti miezi miwili kabla ya uchaguzi wa Oktoba 2015. Baadaye alijaribu kuurejelea wadhifa wake, kitendo ambacho kilipingwa na Maalim pamoja na wengi wa wafuasi wa CUF.
Mgogoro huo uliishia katika Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo mwezi Machi, 2019 yalimpa ushindi Lipumba. Muda mfupi baadaye Machi 19 Maalim Seif akajiunga na chama kingine cha upinzani cha ACT Wazalendo.
Maalim Seif alihamia ACT Wazalendo na wafuasi wengi wa CUF.
‘Makubaliano’ ya Mwinyi na Maalim Seif
Katika uchaguzi wa 2020 CCM ilikabiliwa na upinzani uliokuwa na sura mpya ya ACT Wazalendo. Mchuano wa urais ulikuwa baina ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Maalim Seif.
Uchaguzi huo ulikuwa na mizengwe mingi. Na kama ilivyokuwa kawaida ya chaguzi za Zanzibar tangu ule wa 1995 wa mwanzo chini ya mfumo wa vyama vingi watu wengi, hasa wa upinzani, waliteswa na kuuliwa.
Kwa yaliyotokea katika uchaguzi huo, chama cha ACT Wazalendo kilikabiliwa na mtihani mkubwa wa iwapo itimize wajibu wake wa kikatiba wa kushiriki katika SUKI. Wafuasi wengi wa ACT Wazalendo na washabiki wao wakikitaka chama hicho kijitenge na ushirikiano huo.
Hatimaye, baada ya kushikwa miguu na wadau wa maridhiano ya Zanzibar wa ndani na nje, ACT Wazalendo ilikubali kushiriki katika SUK.
Makubaliano yalifikiwa baina ya Maalim Seif na Dkt. Mwinyi. Na baada ya Maalim Seif kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Desemba 2020, Maalim Seif alimuandikia barua Rais Mwinyi akitaja hoja tatu ambazo akitaka zitimizwe ili kuifanikisha SUK.
Muhimu la kuzingatiwa katika barua hiyo ni maneno ya Maalim Seif kwamba SUK sio lengo bali ni njia tu ya kulifikia lengo ambalo ni kuleta umoja halisi wa Wazanzibari.

Chanzo cha picha, Ikulu Zanzibar
Hoja ya kwanza aliyoitoa Maalim ni kutaka pafanywe uchunguzi wa kimahakama kuchunguza yote yaliyopita katika uchaguzi wa 2020 — mateso na mauaji.
Baada ya matokeo ya uchunguzi waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria na waathirika walipwe fidia.
Dhamira ya hoja hiyo ni kuepukana na utamaduni wa kujifanyia mambo bila ya kuwajibika.
Hoja ya pili ya Maalim Seif iliutaka mfumo mzima wa uchaguzi ufanyiwe marekebisho, hususan Tume ya Uchaguzi kuanzia Mwenyekiti na sekretariati yote; na pili, sheria ya uchaguzi nayo irekebishwe. Kwa mfano, uchaguzi wa mapema ufutwe.
Na hoja ya tatu ilitaka paundwe Tume ya Kudumu ya Maridhiano kuhakikisha kwamba maridhiano ni endelevu na kuyaimarisha Maridhiano kutoka juu kwa viongozi hadi chini kwa wananchi wa kawaida. Kufanya hivyo kutayaondoa Maridhidiano kutoka kuwa ya kisiasa na kuyafanya yawe ya kijamii pia.
ACT Wazalendo inadai kwamba Mwinyi aliyakubali yote hayo. Bahati mbaya miezi miwili baadaye Maalim Seif alifariki dunia. Hadi leo hoja zote hizo tatu hazikutekelezwa.
Mwezi Machi Othman Masoud Othman (maarufu OMO) aliapishwa kumrithi Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Kufika Novemba aliwasilisha kwa Mwinyi waraka mahsusi wenye hoja 26 za namna ya kufanikisha hayo Makubaliano ya hoja tatu baina ya Mwinyi na Maalim Seif
Miongoni mwayo ni njia za kujengeana imani. Kwa mfano, OMO alipendekeza kwamba kiongozi mkuu wa serikali awazuru walau baadhi ya waathiriwa wa maonevu ya wakati wa uchaguzi wa Oktoba 2020.
Waraka wa OMO ulipendekeza pia pafanywe marekebisho ya Tume na sheria za uchaguzi; marekebsho ya mfumo wa serikali za mitaa, ikiwa pamoja na uteuzi wa mashesha, na marekebisho ya mfumo wa Mahakama.
Historia ya chaguzi za Zanzibar inaonesha kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kiwango kikubwa umekuwa ukifanywa na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kwa sababu hiyo, waraka wa OMO umependekeza pafanywe marekebisho ya vyombo vya usalama pamoja na Usalama wa Taifa, na vikosi vitano vya SMZ, yaani Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Polisi, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi cha Valentia (KVZ) na Kikosi cha Zima Moto na Uokozi (KZU) na askari wa Chuo cha Mafunzo (magereza).
Mwinyi kila alipokuwa akiendewa kuhusu haja ya kuyatekeleza makubaliano yake na Maalim Seif alikuwa hakatai ila akiwaomba wabia wake wawe wavumilivu mpaka awe makamu wa CCM, wadhifa ambao sasa anaushika pia.

Chanzo cha picha, ACT Wazalendo
Mnamo Oktoba 2022 aliunde kikosi kazi Zanzibar kilichotoa mapendekezo ya namna ya kusonga mbele na kufanikisha SUKI. Hadi leo ripoti hiyo imewekwa siri na ACT Wazalendo inadai kwamba hakuna pendekezo hata moja lililofanyiwa kazi.
Mei 2023 Mwinyi alichukua hatua nyingine ya kuunda Kamati ya Maridhiano baina ya CCM na ACT Wazalendo. — ikiwa na wajumbe sita kutoka kila upande.
Desemba 2023 Kamati Kuu ya ACT Wazalendo ilikutana na iliamua kuwa hakuna lililofanywa.
Ismail Jussa, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar, ameiambia BBC, “Hatuwezi kuendelea kuburuzwa.”
“Tumeona kuwa katika chaguzi ndogo mambo yale yale yanajitokeza,” aliongeza Jussa.
Mwezi Januari mwaka huu walimpelekea barua Rais Mwinyi wakimpa miezi miwili ayatekeleze Makubaliano yake na Maalim Seif, la sivyo watajitoa kutoka SUK.
Machi 12, Khamis Mbeto, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar alinukuliwa akisema kwamba hayo Makubaliano baina ya Maalim Seif na Mwinyi si ya kikatiba.
Nini kifanyike kuokoa hali?
Mfumo wa sasa wa SUK visiwani Zanzibar una taksiri nyingi na hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya serikali iliyo kweli ya umoja wa kitaifa. Pengine kuna haja ya mfumo huo kufumuliwa na kufumwa upya.
Hata hivyo, endapo marekebisho yaliyopendekezwa kwenye waraka wa OMO yatafanyiwa kazi yatasaidia sana kujengeana imani.
Ili serikali ya aina ya SUK iweze kufanya kazi lazima pawepo nia safi kati ya washiriki wa serikali hiyo ya kutaka kidhati serikali hiyo ifanikiwe.
Ahmed Rajab ni mchambuzi wa siasa za Tanzania, kikanda na kimataifa.












