Je Rais William Ruto atafanikiwa kumnyamazisha Raila Odinga?

Na Abdalla Seif Dzungu

BBCSwahili

Tangu tangazo la kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kwamba hamtambui Rais William Ruto na serikali yake kumekuwa na makabiliano ya kisiasa, kiasi kwamba mgeni yeyote anayewasili Kenya angedhani kwamba taifa hili linaelekea katika uchaguzi.

Cha kushangaza ni kwamba taifa hili ambalo linaendelea kuzongwa na hali ngumu ya kiuchumi limetoka katika uchaguzi miezi sita tu iliopita.

Licha ya kuwasilisha kesi ya kupinga uchaguzi wa Rais William Ruto mahakamani baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa 2022 na baadaye kesi hiyo kutupiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi, Raila Odinga hakuridhika na uamuzi wa mahakama hiyo.

Yeye na Muungano wake wa Azimio walifanya uchunguzi wao kuhusu matokeo ya uchaguzi huo na majibu ya uchunguzi huo yanadai kwamba alimshinda rais Ruto kwa zaidi ya kura milioni mbili.

Hata hivyo mtu anayedaiwa kujitolea na kufanya uchunguzi huo kwa mujibu wa Raila alikuwa mfanyakazi aliyejitolea wa Tume Huru ya Uchaguzi na Ukaguzi wa Mipaka, IEBC ambaye jina lake hakulikutajwa.

Akizungumza katika uwanja wa Jacarandá jijini Nairobi baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi huo, Raila Odinga alitoa wito kwa Rais William Ruto na serikali yake kujiuzulu mara moja huku akisisitiza kwamba tume yote ya uchaguzi ivunjiliwe mbali na kufanyiwa ukaguzi.

Raila pia alimuonya Rais William Ruto kuhusu ushawishi wake wakati wa utawala wa rais Moi huku akimtaka kiongozi huyo na naibu wake kutilia maanani anayoyasema.

''Ruto na Gachagua wamekuwa wakinitisha wakisema mambo mengi kunihusu, nataka kumwambia Ruto hutujui. Nenda ukamuulize bwana nyayo, nguvu za raia ni sauti ya Mungu’’, alisema bwana Odinga.

Kiongozi huyo ambaye amekuwa akifanya mikutano katika sehemu mbali mbali za nchi kwa lengo la kuwahamasisha wafuasi wake kuhusu hatua yake ya kuipinga serikali iliopo hata hivyo hakukosa majibu kutoka kwa Rais William Ruto.

Akimjibu katika mkutano mmoja wa kidini huko Kirinyaga, Ruto alimwambia bwana Odinga kwamba hatokubali upinzani kuhujumu serikali yake kwa maslahi yao ya kibinafsi.

"Hawawezi kushikilia nchi hii mateka, tena. Kwa miaka mingi, yeye (Bw Odinga) amekuwa na maandamano na kufaidika. Unataka kunipangia maandamano? endelea, lakini sitajikita katika kusuluhisha masuala ya mtu mmoja,” aliongeza.

“Wakenya wasiwe na wasiwasi. Sitaruhusu watu wachache kwenda kwenye kona moja kupanga jinsi ya kututisha kupitia maandamano ya kutufanya tukengeuke katika kushughulikia mahitaji ya Wakenya. Wanataka tuangazie maslahi yao lakini tumewazoea. Tunawaambia kwamba mwisho umefika. Ridhika na ulichopata hapo awali kutokana na vitisho na utuwache tuwahudumie Wakenya,” Dkt Ruto alisema.

Alidai kwamba Bw Odinga alikuwa akijaribu kupanga maandamno kwa lengo la kumshiniiza amruhusu katika serikali yake, madai ambayo kiogozi huyo wa upinzani ameyakana.

Ruto 'kumdhoofisha' Raila

Huku Raila akishikilia msimamo wake mkali dhidi ya serikali, Ruto anaonekana kubuni mpango wa kumtenga kiongozi huyo mkongwe wa upinzani kwa lengo la kumuacha akitapatapa kisiasa.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni mpango wa kuimarisha ubabe wake mamlakani, Ruto amekuwa akiwalenga wabunge na magavana wa mrengo wa upinzani (Azimio) kwa ahadi za heri na miradi ya maendeleo.

Huku kiongozi huyo wa ODM na wenzake wa Azimio Martha Karua na Kalonzo Musyoka wakianzisha mikutano ya nchi nzima kuwataka Wakenya kukataa serikali ya Kenya Kwanza, Rais amekuwa na shughuli nyingi kukutana na wabunge wa sasa na wa zamani kutoka Luo Nyanza, Magharibi, eneo la Kisii na Pwani.

Tangu alipotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi uliopita, Rais Ruto amekuwa akiwashawishi viongozi wa upinzani kujiunga na serikjali yake kwa lengo la kupata wabunge wengi ili kupitisha miswada ya serikali.

Hatua hiyo inaijiri baada ya kubainika kwamba idadi ya wabunge na maseneta wa pande pinzani zilikuwa zinakaribiana.

Wachambuzi wa kisiasa hatahivyo wanadai kwamba Ruto amekuwa akicheza kadi mbili za kisiasa, kudhoofisha upinzani na vile vile kutafuta uungwaji mkono katika uchaguzi ujao wa 2027.

Na ili kuthibitisha hatua hiyo , kiongozi huyo amekuwa akitafuta uungwaji mkono kutoka kwa ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga .

Ruto 'avamia' ngome ya upinzani

Wakati wa ziara yake ya hivi majuzi huko Nyanza, ambayo ndio ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga, Rais William Ruto ambaye alipata mapokezi mema aliahidi kuwafanyia mambo mengi wananchi wa eneo hilo – hatua inayoonekana na waachambuzi wa kisiasa kama chambo cha kuwavutia ili wamuunge mkono..

Lakini hatua yake ya hivi majuzi ya kukutana na viongozi tisa wa chama cha ODM kinachoongozwa na kiongozi huyo wa upinzani katika ikulu ya Rais ndio iliowaacha wengi vinywa wazi.

Licha ya viongozi hao tisa kudai kwamba walikutana na kiongozi huyo kwasababu ya masuala ya maendeleo, wengi wanasema kwamba ulikuwa mkutano wa kuwavutia viongozi hao kushirikiana na serikali bungeni.

Akizungumza baada ya mkutano huo , kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliwataja viongozi waliokutana na rais William Ruto kuwa wasaliti na kuongezea kwamba rais huyo alikuwa anatumia kila njia kuudhofisha upinzani kulirudisha taifa hili katika uongozi wa kidikteta wa chama kimoja.

Chama cha Jubilee chajiunga na muungano wa serikali

Laini hatua hiyo ya kumdhoofisha Raila na upinzani ka ujumla haikukomea hapo. Hivi majuzi rais William Ruto alifanya ‘mapinduzi ya ndani kwa ndani’ katika chama cha Jubilee ambacho ni miongoni mwa vyama vinavyounga mkono Muungano wa upinzani wa Azimio.

Baada ya kukutana na viongozi 32 wa chama hicho walioapa kushirikiana na serikali yake , hatua iliopingwa na katibu mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni , baadhi ya viongpozi wa chama hicho walifanya mapinduzi katika chama hicho.

Mapinduzi hayo yanayoonekana kujitokeza muda mfupi baada ya barua za kinidhamu kuibuka ambapo Kioni aliwataka wabunge waliomtembelea Rais William Ruto katika Ikulu ya Ikulu kuonyesha sababu za hatua yao.

Mrengo wa chama cha Jubilee unaoegemea upande wa rais Ruto ambao ulimtaja Mbunge wa EALA Kanini Kega kuwa Kaimu Katibu Mkuu ulishirikisha wanachama wanne wapya katika Halmashauri Kuu ya Kitaifa (NEC) katika hatua inayotarajiwa kudhoofisha zaidi mrengo wa Kioni.

Kundi linaloongozwa na Kega lilimuondoa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika orodha ya maafisa waliofukuzwa.

Akizngumza baada ya mapinduzi hayo katibu mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni alisema kwamba hatua hiyo inakusudiwa kuua maoni yoyote kinyume na kuhakikisha kuwa hakuna sauti dhidi ya maovu ya serikali ya William Ruto.

Hatahivyo wanachama wa cham hicho Jeremiah Kioni na David Murathe sasa wanaweza kupumua baada ya Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) kutengua kwa muda azimio la kamati kuu ya kitaifa ya kuwasimamisha kazi kama Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa Kitaifa.

Je Ruto atafanikiwa 'kumnyamazisha' Raila Odinga?

Na Mchambuzi wa masuala ya kisiasa David Burare

Kulingana na Burare hatua ya kumnyamazisha Raila Odinga huenda isifue dafu kwani iwapo Rais William Ruto atatumia vitengo vya usalama kuharibu mikutano yake na hivyo basi kumnyamazisha, umaarufu wa kiongozi huyo huenda ukaongezeka zaidi.

‘’Kawaida Raila amekuwa akiongeza umaarufu wake serikali iliopo madarakani inapokabili mikutano yake kwa kutumia vitoa machozi. Hatua hiyo humuongeza nguvu bwana Odinga na kufanikiwa kutuma ujumbe kwa jamii ya kimataifa kwamba kuna tatizo nchini ambalo linahitaji utatuzi’’,alisema bwana Burale.

Vile vile mchambuzi huyo anasema kwamba ni vigumu kumkabili Raila kwa sababu ni mwanasiasa mkongwe wa upinzani anayejua kuandaa mikutano ya kisiasa na kusukuma ajenda yake.

Kwa mujibu wa Burare, Raila alikuwa akitafuta njia ya kumpeleka kwa raia na hivyobasi akatumia ripoti ya uchunguzi wa matokeo ya uchaguzi iliotolewa na mtu aliyejitolea anayedaiwa kufanya kazi na tume ya uchaguzi IEBC.

''Uwezekano kwamba raia wataunga mkono madai ya Raila ni mkubwa kwa sababu idadi kubwa ya watu wamekuwa wakihudhuria mikutano yake’’.

Serikali zilizokuwepo madarakani zimefanikiwa kumtuliza Raila kupitia ushirikiano wa 'handshake'. Kwa sababu Raila asiye na kazi ni 'hatari' kwa serikali yoyote, na ndiposa unaona Rais Mwai Kibaki na mwenzake Uhuru Kenyatta walifanikiwa kumtuliza kwa kushirikiana naye’’, aliongezea mchambuzi huyu.

Je Ruto amekuwa akikabili vipi shutuma za Raila?

Kwa mujibu wa bwana Burare, Rais William ametengeneza ujumbe ambao umekuwa ukigeuza fikra za Wakenya.

‘’Kila mara Raila anapomshtumu, Ruto amekuwa akimjibu Raila kwamba kila Mkenya atalipa ushuru’’ .

Kulingana na Bwana Burare, kupitia ujumbe huu Ruto anawaelezea Wakenya kwamba sababu ya Raila na Uhuru kulalamika ni kwamba hawataki kulipa kodi.