Ndoto ya Rais Putin kushinda vita vya Ukraine yaponyoka

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kwa muda wa mwezi mmoja uliopita vikosi vya Ukraine vimerudisha nyuma jeshi la Urusi na kutwaa tena sehemu kubwa za maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu.

"Ukweli uko upande wetu na ukweli ni nguvu!" Vladimir Putin alizungumza kwa kipaza sauti kwenye Bustani ya Red Square wiki iliyopita, baada ya sherehe kubwa ambapo alitangaza sehemu kubwa nne za eneo la Ukraine kuwa sehemu ya Urusi.

"Ushindi utakuwa wetu!"

Lakini katika ulimwengu wa kweli, mambo yanaonekana tofauti sana.

Hata wakati rais wa Urusi alipotia saini mikataba yake ya unyakuzi kinyume cha sheria huko Kremlin, vikosi vya Ukraine vilikuwa vinasonga mbele ndani ya maeneo ambayo alikuwa ameyateka.

Mamia ya maelfu ya wanaume wamekuwa wakitoroka Urusi badala ya kuandikishwa kupigana katika vita vinavyozidi kuongezeka.

Na mambo yanaenda vibaya sana kwenye uwanja wa vita hivi kwamba Bw Putin na wafuasi wake sasa wanarekebisha kile walichodai kuwa ni "de-Nazification" ya Ukraine na ulinzi wa wazungumzaji wa Kirusi kama mapambano dhidi ya mataifa yote ya Magharibi.

Huo ndio ukweli na hakuna hata moja iliyo upande wa Urusi.

Mwathirika wa mfumo wake

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Vladmir Putin

"Yeye yuko katika eneo la wasioona. Inaonekana haoni kinachoendelea," mhariri wa Riddle Russia, Anton Barbashin, anahoji kuhusu rais wa Urusi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kama ilivyo kwa wengi, mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa anaamini kwamba Bw Putin alijipata katika hali ya switofahamu kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa Ukraine, pamoja na upinzani mkali wa Kyiv dhidi ya uvamizi.

Anapotimiza umri wa miaka 70 leo, baada ya zaidi ya miaka 20 madarakani, inaonekana kiongozi wa Urusi amekuwa mwathirika wa mfumo wake mwenyewe. Mtindo wake wa kiimla unamzuia kufahamu ukweli uliopo .

"Huwezi kuhoji mawazo yake," anaelezea Tatyana Stanovaya, mkuu wa kampuni ya uchambuzi ya R.Politik.

 "Kila mtu anayefanya kazi na Bw Putin anajua picha yake ya dunia na ya Ukraine, wanajua matarajio yake. Hawawezi kumpa taarifa zinazokinzana na maono yake. Hivyo ndivyo ilivyo."

 Hotuba ya hivi punde ya rais, aliyoitoa chini ya vinara vya Kremlin vilivyopambwa kwa dhahabu, ilieleza tena maono yake ya utaratibu mpya wa dunia.

Inahusisha Urusi yenye nguvu, ulimwengu wa Magharibi uliotawaliwa ambao umelazimishwa kujifunza heshima na Kyiv kuitii tena Moscow.

Ili kufikia hilo, Ukraine ndio uwanja wa vita uliochaguliwa na Bw Putin.

Hata kama matarajio yake yanaonekana kuwa ya uwongo, yeye haonekani katika hali ya kurudi nyuma.

"Mahesabu mengi makubwa ambayo Kremlin ilikuwa ikifanya kazi nayo hayakufaulu na haionekani kama Putin ana mwpango mwengine, zaidi ya kuendelea kuwasukake katika mstari wa mbele wa vita na kutumaini kwamba idadi kubwa itaizuia Ukraine kusonga mbele zaidi. "Anton Barbashin anaamini.

Warusi wasiotaka kwenda vitani

Warusi wanaotoroka kwenda vitani

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Raia wa Urusi wanaotoroka kwenda vitani

"Kusukuma watu katika mstari wa mbele wa vita" sio jambo dogo.

Vladimir Putin anaendelea kuuita uvamizi wake "operesheni maalum ya kijeshi" - akiifanya kuwa ndogo na ya muda mfupi.

Warusi wengi waliweza kukubali hilo – na hata kuunga mkono – kwasababu haikuwaathiri moja kwa moja. Lakini usajili wa wanajeshi wa akiba umegeuza kitu kisichoeleweka kuwa hatari ya karibu sana na ya kibinafsi.

Wanasiasa wa kanda wanajizatiti katika kinyang'anyiro cha mtindo wa Kisovieti ili kutimiza matakwa ya Putin kwa kupita kiasi, wakiwaita wanaume wengi iwezekanavyo.

"Kwa Warusi wengi, vita vilianza wiki chache zilizopita," Anton Barbashin anasema.

"Katika miezi ya kwanza, watu wanaokufa walikuwa wengi kutoka pembezoni na vituo vidogo. Lakini usajili wa wanajeshi wa ziada utabadilisha hilo, kwani majeneza yatarudi Moscow na St Petersburg."

Hali ngumu

.
Maelezo ya picha, Maeneo yaliokombolewa na Ukraine na maeneo yalio chini ya udhibiti wa Urusi Ukraine

Kamsa hiyo ya usajili wa wanajeshi wa ziada imezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii na wake na akina mama wa waajiriwa wapya - wale ambao hawakukimbilia mipakani wakati usajili ulipotangazwa.

Baadhi ya machapisho yao - na video za wanaume wenyewe - zinaonyesha hali mbaya: chakula duni, silaha kuukuu na ukosefu wa vifaa vya msingi vya matibabu. Wanawake wanajadili kupeleka taulo za usafi ili kuweka katika viatu hivyo vya wanaume na tamponi za kufunga majeraha yao.

Gavana wa mkoa wa Kursk ameelezea hali katika vitengo kadhaa vya kijeshi kama "mbaya tu", ikiwemo ukosefu wa wa sare za kijeshi.

Ugunduzi kama huo unafichua mianya katika moja ya madai ya kujivunia ya Vladimir Putin: kwamba amelijenga upya jeshi la Urusi kuwa jeshi la kitaalamu la kupigana ambapo raia wazalendo watataka kuhudumu.

Lakini kwa sasa, wake wengi wa walioandikishwa wanaonekana kuwaunga mkono wanajeshi wao.

"Tuko katika hatua ambayo sehemu kubwa ya jamii ya Urusi bado inaamini kuwa 'Urusi ni nguvu kubwa katika kupambana na Nato nchini Ukraine' na kutuma tamponi, soksi na miswaki kwa waliosajiliwa ni ishara ya uzalendo," Anton Barbashin aliandika kwenye Twitter wiki hii. .

Vita 'takatifu' dhidi ya Magharibi

Hata rais aligusia matatizo wiki hii, akielezea hali katika mikoa iliyojumuishwa kuwa "ya utulivu".

Lakini kuna msukumo mkubwa wa hatua ya Urusi miongoni mwa nchi za Magharibi ambazo zinaunga mkono Ukraine.

Waandishi wa vyombo vya habari vya serikali sasa wanaelezea unyakuzi wa ardhi nchini Ukraine kama jambo kubwa zaidi, na inaonekana kulichochea taifa hilo kupigana vita vikubwa zaidi.

"Ni vita vyetu dhidi ya Ushetani kamili," Vladimir Solovyov aliwaambia watazamaji wiki hii.

"Hii haihusu Ukraine. Lengo la nchi za Magharibi liko wazi. Mabadiliko ya serikali na kuikata Urusi, ili Urusi isiwepo tena," alifoka.

Huo ndio "ukweli" ambao Vladimir Putin anaamini na ndiyo sababu wakati huu wa udhaifu wa malengo ya Urusi pia ni wakati wa hatari.

"Vita hivi ni muhimu kwa Urusi na kwa hivyo kwa Putin, ushindi lazima uwezekane," Tatyana Stanovaya anasema.

Na "ana silaha za nyuklia", anasema bila kuficha.

"Nadhani anatumai kuwa katika kiwango fulani cha ongezeko la nyuklia, nchi za Magharibi zitaondoka Ukraine."

Sio yeye pekee aliyeona sauti ya Bwana Putin ya kuwa mkali zaidi na ya kimasiya.

"Anahisi kwamba hivi ndivyo anaamini: kwamba huu ni msimamo wa mwisho wa Dola ya Urusi, vita vya pande zote na Magharibi," anasema Anton Barbashin.

"Kwamba tuko kwenye mstari wa kumalizia, iwe Urusi itafanikiwa au la."

Bila shaka, huo pia ni "ukweli" ambao Vladimir Putin sasa anahitaji Magharibi kuamini, zaidi ya hapo awali.