Wanamiereka wa Uganda wanaovuma mitandaoni kwa mtindo wao wa kipekee

Wanaume wawili wakiwa ulingoni

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Video za aina hii ya miereka imetazamwa na zaidi ya mara milioni 500 katika mitandao ya kijamii.
    • Author, Kelvin Kimathi
    • Nafasi, BBC Sport Africa in Mukono, Uganda
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika mji mtulivu viungani mwa jiji kuu la Uganda, kundi la vijana wa kiume na wakike wanafafanua upya mchezo wa miereka kwa njia ambayo imewafanya kupata umaarufu ambao haukutarajiwa duniani.

Hawafanyi maonyesho katika ukumbi mkubwa ulio na taa zinazoangaza, skrini ya kubwa au hata kuwa na ulingo uliofunikwa kwa turubai.

Badala yake vijiti vya mianzi na mistari miwili ya manjano iliyofifia inatumiwa kuashiria ulingo wa matope mazito, ambao pia ni jukwaa la Miereka (Soft Ground Wrestling) maarufu kama SGW.

"Hatukuwa na fedha za kununua na kutengeneza uwanja halisi wa miereka," Daniel Bumba, aliiambia BBC Michezo Afrika.

"Kwa hiyo tulibuni jukwaa letu wenyewe kwa kutumia mwani kutoka kwenye msitu ulio. Na badala ya kutumia turubai, tunatumia udongo na matope ya kawaida ili kuwakinga wachezaji wasiumie wakiangushana.

"Hilo ndilo linafanya mchezo wetu kuwa wa kipekee."

Mchezo huu umepata umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii ikiwa na zaidi ya wafuatiliaji milioni 500 kwenye TikTok, Instagram, X, Facebook na YouTube na kuwavutia mashabiki wenye shauku ambao wanafuatilia matukio huko Mukono.

"Ni watu wetu. Tunapenda wanachokifanya," alisema mmoja wa mashabiki wa kike anayefuatilia mchezo huo.

Kupata matumaini

Lamono Evelyn na Jordan Loverine ni miongoni mwa wachezaji nyota wanaoibuka mieleka ya SGW

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Lamono Evelyn na Jordan Loverine ni miongoni mwa wachezaji nyota wanaoibuka mieleka ya SGW
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya kuvutia kwenye mitandao ya kijamii, wachezaji wa SGW wamepitia mengi maishani.

Idadi kubwa ya wachezaji ni mayatima au wanalelewa na wazazi wasio na wenza, hawapokei mshahara na wanategemea michango ili kujikimu.

Wanafanya mazoezi wakati kwenye mvua au jua kali, wanapika nje, na kulala katika mabweni ya kukodi.

Akiwa na umri wa miaka 23, Jordan Loverine ameibuka kuwa mmoja wa nyota mahiri zaidi wa SGW na ni ishara ya kile ambacho mchezo huo unamaanisha ni kwa wale ambao hawana mahali pengine pa kugeukia.

"Mieleka imenipa matumaini baada ya kuacha shule," aliambia BBC Michezo Afrika.

"Nilikuwa karibu kukata tamaa maishani.

"Lakini SGW imenipa familia mpya na ndoto mpya pia - kuwa mwanamieleka mzuri, kupata umaarufu na mafanikio na kuwasaidia wengine."

Zaidi ya vijana 100 wa Uganda, wote wenye umri wa chini ya miaka 25, sasa ni wachezaji wa mieleka ya SGW.

Miongoni mwa wenye vipaji vya hali ya juu ni Lamono Evelyn kutoka Kaskazini mwa Uganda, ambaye jina lake la kisanii ni Zampi.

Alilelewa na mama yake baada ya baba yake kufariki akiwa mdogo, hakumaliza shule ya upili kwa sababu ya matatizo ya kifedha.

Lakini, kupitia mieleka, kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 amepata nidhamu na matumaini mapya.

"Kabla ya SGW, nilikuwa na matatizo ya kudhibiti hasira. Nilikuwa na kiburi," aliiambia BBC Michezo.

"Mieleka ilinisaidia kudhibiti hasira yangu. Sasa mchezo huu kwangu ni maisha. Umenibadilisha kiakili na kimwili."

Kutoka WWE hadi mwanzilishi wa SGW founder

Daniel Bumba

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Daniel Bumba, anayejulikana kama Bumbash, ni mwanzilishi wa mieleka ya aina hii

Bumba, anayefahamika kwa jina la utani kama Bumbash, ni shabiki mkubwa wa mieleka ambaye aamekuwa akiigiza watangazaji wa WWE (World Wrestling Entertainment).

"Mama yangu alikuwa akinichapa kwa jinsi nilivyokwa nikipenda mchezo wa mieleka," Bumbash, 37, anasema.

"Sikusita kuonyesha kipaji changu kwani nilianza kuiga watangazaji wa michezo ya mieleka, na hatimaye nikawa natafsiri mechi za WWE kwa Kiganda katika kituo kimoja cha televisheni nchini."

Kufikia 2023, Bumbash alibaini kuwa watu wanaopenda mchezo huo lakini hakuna miundombinu. Kwa hivyo alichukua hatua ya kuwafunza vijana mchezo huo kwa kutumia mbinu yake mwenyewe kuanzia mwanzo.

Alipoweka mtandaoni mechi yao ya kwanza wakimenyana kweney tope matokeo yalikuwa chanya. Wataalamu wa Mieleka wa WWE na AEW waliwasiliana naye na hata baadhi yao kuwasilisha ombi la kutoa msaada.

Mtandao wa kijamii unaendelea kuwa kiungo muhimu, kwani baadhi ya wachezaji walisajiliwa kupitia mtandao wa TikTok.

Licha ya umaarufu wa SGW mtandaoni, Bumbash ilianza kuchuma mapato kutokana video zao hivi majuzi tu na inawapa chini ya dola 1000 za Kimarekani kwa mwezi.

Kipato hiyo kinasimamia sehemu ndogo tu ya gharama zao za uendeshaji, na Bumbash huusimamia gharama zingine kupitia mchango wake binafsi kama mtangazaji wa Runinga ili kufadhili malazi, chakula na gharama zingine.

"Sehemu kubwa ya mshahara wangu inaenda kwa wachezaji hawa chipukizi. Sina akiba yoyote," alisema.

"Wananiita Baba. Wananitegemea kwa kila kitu. Nwalisha, kuwapa makaazi na kuwatunza."

Kupambana pande zote

Picha iliyopigwa kutoka angani inawaonesha mashabiki waliozunguka uwanja wa mieleka nchini Uganda

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Kulingana na Bumbash takriban watu 5,000 huhudhuria mechi yao ya mieleka siku za Ijumaa

Usalama unasalia kuwa suala la dharura katika mieleka ya SGW.

Ingawa pigano linapangwa na kufanyiwa mazoezi, visa vya wachezaji kuvunjika au kujeruhiwa shingo hutokea.

"Tunajitahidi sana kupata vifaa vya huduma ya kwanza, dawa na vifaa kinga kwa wachezaji," Bumbash alisema. "Lakini changamoto sana sana hutokana na suala la upatikanaji wa fedha."

Sio kawaida kuona jeraha la kumaliza kazi angalau mara moja kwa mwezi.

"Wakati mwingine washiriki wanakabiliw ana maumivu ya mgongo au shingo," Bumbash aliongeza. "Wakati mwingine mchezaji chipukizi huvunja.

"Tunajaribu kuwahudumia waliojeruhiwa, lakini ni vigumu bila ya kuwa vifaa vinavyofaa."

Licha ya hatari, shauku bado haijapungua miongoni mwa wachezaji.

"Yataka moyo," Loverine alisema.

"Lazima uache mambo mengi nyuma - marafiki wanaokukatisha tamaa, nafasi za kazi - na kuzingatia mieleka."

Zampi aliongeza: "Kucheza kwenye matope ni ngumu sana. Lakini ikiwa kweli unataka kitu, unaweza kukifanya."

Hatimaye SGW juhudi zao zilimvutia nyota wa WWE Cody Rhodes, ambaye aliwasaidia kupata jukwaa la kitaalamu ulobadilisha mchezo wa kundi hilo mapema mwaka huu.

"Sasa tunaweza kushindana katika ngazi ya kimataifa," alisema Bumbash.

Licha ya kupata jukwaa la kitaalamu, wachezaji bado wanajivunia walikotoka.

"Napenda jukwa hili la kisasa, lakini napendelea kucheza kwenye tope," Zampi alisema huku akitabasamu.

"Inaashiria tamaduni zetu za Kiaafrika."

Mchezo huo unapoendelea kupata umaarufu, ndoto ya Bumbash ni kuimarisha mustakabali wa siku zijazo za wanamieleka wa SGW, kwanza kwa kuwajengea makazi ya kudumu.

Uwanja unaotumiwa kwa mazoezi umekodishwa, na SGW huenda wakapoteza makazi yake kama hatafanikiwa kuchangisha dola 40,000 kuununu.

"Tukifanikiwa kununu ardhi hii tunaweza kujenga mabweni na sehemu ya kufanyia mazoezi ya viungo na kituo cha matibabu," alisema Bumbash.

"Tunataka kuandaa shindano la kwanza la dunia la mieleka barani Afrika, kusafirisha vipaji katika jukwaa la kimataifa."

Huku wakiendelea kucheza mieleeka kwenye matope, kufanya mazoezi kwenye mvua wakiwa na ndoto ya kufika katika jukwaa la kimataifa, wanamieleka wa Uganda wa Soft Ground Wrestling wanadhihirisha wazi kuwa utukufu unaanzia mbali.

Takribana wanaume 30 wanaonekana wakifanya mazoezi kwenye matope katika uwanja mmoja nchini Uganda.

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Wanamieleka wa SGW wakiwa mazoezini
Wacheza mieleka hutumia muda kuboresha mbinu zao kabla ya kumenyana mbele ya umati wa mashabiki

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Wacheza mieleka hutumia muda kuboresha mbinu zao kabla ya kumenyana mbele ya umati wa mashabiki
Crazy Dominions ndio mabingwa wakuu wa timu ya wanaume ya SGW

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa

Maelezo ya picha, Crazy Dominions ndio mabingwa wakuu wa timu ya wanaume ya SGW

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi